Read UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI text version

Uhakiki wa Kazi za Fasihi

Mwenda Ntarangwi, Ph.D.

UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI

Mwenda Ntarangwi, Ph.D. Augustana College, Rock Island, IL 61201 2004

2

Yaliyomo................................................................ Utangulizi ....................................................... Sura Ya Kwanza 1.0 1.1 1.2 1.3 1.4 1.5 1.6 1.7 1.8 2.0 2.1 2.2 2.3 2.4 Fasihi Ni Nini? .............................................. Fasihi Kama Sanaa Itumiayo Maneno ............. Fasihi Kama Sanaa: Nadharia Ya Umithilishaji... Dhana Ya Ubunilizi .......................................... Dhana Ya Muundo ............................... Nadharia Ya Uhalisia-Nafsi ................................. Nadharia Ya Mguso ............................................. Hitimisho ............................................................. Nadharia Za Uhakiki .................................... Uhakiki Ni Nini? ....................................... Vigezo Vinavyozingatiwa Katika Uhakiki ........... Nadharia Za Uhakiki ............................................

3 5 7 10 12 15 16 17 19 24 27 28 30 35 37 39 40 43 48 52 54 54 59 65

Fasihi Na Jamii ...................................................... 21

Sura Ya Pili

Pana Njia Halisi Ya Kuhakiki? ............................... 32

2.4:1 Nadharia Ya Ki-Marx .......................................... 2.4:2 Nadharia Ya Uasilia ............................................ 2.4:3 Nadharia Ya Umuundo ...................................... 2.4:4 Nadharia Ya Umuundo-Mpya ............................. 2.4:6 Nadharia Ya Uhalisia ............................................ 2.4:8 Hitimisho .............................................................. Sura Ya Tatu 3.0 3.1 3.2 3.3 Maendeleo Ya Fasihi Andishi............................... Tamthilia ............................................................. Riwaya .................................................................. Mashairi................................................................

2.4:5 Nadharia Ya Ufeministi ......................................... 45 2.4:7 Nadharia Ya Uhalisia-Nafsi (Tathimini-Saikolojia) 49

3

3.4 4.0 4.1 4.2 4.3 4.4

Hitimisho

......................................................... 69 73 73 78

Sura Ya Nne Uhakiki Wa Kazi Za Fasihi.................................... Utangulizi............................................................ Misingi Ya Kuzingatiwa Katika Uhakiki .........

Jukumu La Mhakiki................................................ 75 Hitimisho................................................................. 108 Tamati .................................................................... 109 Marejeleo............................................................... 112

Sura ya Tano

4

UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI

UTANGULIZI Kuhakiki kazi ya fasihi ni jambo ambalo huzingatiwa sana na wanafunzi na walimu shuleni, vyuoni na katika taasisi nyingine ambapo somo la fasihi hushughulikiwa. Kitendo cha kuhakiki kazi za fasihi si kipya ulimwenguni hata ingawa zaidi kimehusishwa na fasihi-andishi. Uhakiki umekuwepo tangu binadamu awe na uwezo wa kuzungumza na kuadhiri maoni na maisha ya wengine. Hivyo basi uhakiki umekuwepo hata wakati ambapo fasihi-simulizi ndiyo iliyokuwa fasihi ya kipekee katika jamii ya wanadamu (yaani kabla ya taaluma ya kuandika na kuchapisha kuzua fasihiandishi). Kama ilivyo na mazungumzo au matumizi yoyote ya lugha biaina ya wanadamu huwa panaulizwa maswali ya kutaka kupata fafanuzi na maelezo zaidi kuhusu jambo husika. Hadhira huuliza maswali ya ufafanuzi kuhusu kazi wanayoshuhudia au hata kupinga na kukosoa msimulizi wa kazi ile iwapo wanafahamu muktadha, muundo, mwelekeo, maudhui, na mengineyo ambayo yanajenga usimulizi huo. Hivyo ndivyo ilivyo na kazi yoyote ya fasihi. Kazi ya fasihi inakusudiwa hadhira fulani, na ili iwe ya manufaa kwa hadhira hiyo, ni lazima iwe yazingatia kaida fulani zinazochukuana na utamaduni wa hadhira hiyo. Kwa hivyo kazi ya fasihi haina budi kutimiza inachotarajiwa kutimiza. Yaani kutunga kuna kaida na misingi maalum inayotokana na utamaduni wa jamii husika, ambayo humwezesha yeyote anayeipokea, isoma, au isikiza kuikadirisha, kuibainisha kama nzuri, mbaya, au mwafaka. Lakini ni vipi tunafahamu kwamba hilo limetokea? Kutimiza au kutotimizwa kwa kaida hizo hutokea kwa kuzingatia kazi husika katika kitendo cha kuihakiki. Uhakiki ndio unaotuwezesha kudhibitisha iwapo kazi ya fasihi inatimiza kaida inazopaswa kutimiza. Na hivyo basi kudhihirisha kwamba utunzi wa kazi ya fasihi si jambo la kubahatisha bali huwa limefungwa na kaida maalum. Na kaida hizo ndizo zinazomwongoza mhakiki. Isitoshe, uhakiki hutuwezesha kuielewa na kuieleza kazi ile ipasavyo. Ni wazi kwamba mtu hawezi kuhakiki kitu ambacho yeye hakifahamu au hana habari kukihusu. Ni nia yetu kabla ya kuingilia swala la uhakiki, tuangazie macho dhana

5

ya fasihi ambacho ndicho kiini cha uhakiki. Mswada huu unatarajia kushughulikia mambo matatu muhimu; kudondoa mambo muhimu kuhusu fasihi, kubainisha nadharia mbali mbali za fasihi na kuzingatia maendeleo ya mada mbali mbali za fasihi.

6

SURA YA KWANZA

1.0

FASIHI NI NINI? Fasihi kama dhana, imeelezwa na wengi kwa kuegemea nadharia na mitizamo

mbali mbali. Hata hivyo ni muhimu tufahamu ya kwamba maana inayopewa dhana au kitu fulani, huwa inachukuana na matumizi ya dhana yenyewe, watu wanaohusika, mahali dhana hiyo inamotokea, na hata kipindi au wakati husika. Hii ndiyo sababu twapata maana mbalimbali zikitolewa kuhusu fasihi. Kwa mfano, waandishi wengi wa Kimagharibi wamesisitiza kwamba fasihi yahusu tu kazi zilizoandikwa. Ndiposa Okot P' Bitek (1973:18) anasema: Katika usomi wa kimagharibi, fasihi humaanisha maandishi ya wakati au nchi fulani, hasa ile yenye kupewa thamani ya juu katika mtindo na uendelezaji wake. Ufafanuzi huu unaotilia mkazo uandishi walenga kueleza kwamba fasihi ni amali ya jamii zilizovumbua sanaa ya uandishi.[tafsiri yetu] Kwa hivyo, fasihi, kulingana na mtizamo huo wa kimagharibi, imechukuana na uandishi, na hivyo basi fasihi si fasihi mpaka iandikwe. Bila shaka mtizamo kama huu hupuuza fasihi-simulizi. Ama kwa hakika hiyo hatua ya kuihusisha fasihi na maandishi ni ya maksuudi inayodhamiriwa kuonyesha fasihi kama amali ya jamii yenye taluma ya kusoma na kuandika. Ni kile kitendo cha kibinafsi au cha kubagua ambacho hudhamiria kuonyesha jamii ambazo hazina taaluma ya uandishi kama jamii duni. Ukweli ni kwamba pamewahi kuwepo na bado zipo kazi za fasihi za hali ya juu kutoka kwa jamii ambazo hazikuwa na taaluma ya kusoma na kuandika. Isitoshe, pana mifano kemkem ya kazi zilizokuwa katika masimulizi hapo awali, lakini sasa zimehifadhika katika maandishi na huratibiwa kama kazi za fasihi. Kazi nyingi za ushairi

7

wa Kiswahili ni mifano ya kazi kama hizo. P'Bitek (1973:20) kwa kuipinga kauli ya kutengea fasihi jamii fulani anasema; Tunashurutika kukataa ufafanuzi huu unaotenga na kubagua; na badala yake kuunda ufafanuzi wa kimapinduzi utakaoionyesha fasihi kama inayochukua kazi zote za kubuniwa za wanadamu zinazoelezwa kwa maneno. [tafsiri yetu] Maneno haya ya P'Bitek ni maneno ya kuvutia lakini huenda yasiwe na dharura yoyote katika wakati huu maana pana kazi kemkem za fasihi katika tamaduni zetu ambazo wakati wa awali hazingeorodheshwa kama kazi za fasihi. Lakini bado hatujatoa mwongozo thabiti wa kuonyesha ni kazi zipi zinaratibiwa kama za fasihi na ni zipi zinazoingia katika kikundi chengine. Ni dhamira ya mswada huu kuangazia jambo hili macho ili kuchanganua ni kazi za aina gani zapaswa kuchukuliwa kama kazi za fasihi iwe andishi au simulizi. Waandishi wengi wameandika kuhusu swala hili la fasihi, na maoni yao huwa kwa njia moja au nyengine yanadhihirisha kutotosheka kwao na yaliyosemwa na wengine kuhusu swala hilo, wengine wakijaribu kubainisha utunzi uliopo, na wengine wakifafanua zaidi maelezo yaliyopo. Ameir Issa Haji (1983:30) anasema kuwa fasihi ni: Sanaa itumiayo maneno ili kutoa picha halisi ya mwanadamu akiwa maishani mwake; mahusiano yake na viumbe wengine, migogoro yake na mazingira, shida zake, raha zake, matumaini yake na jinsi anavyopiga hatua katika maendeleo yake. Mtizamo kama huu waitizama fasihi kama kazi inayoendelezwa kwa maneno, iwe andishi au simulizi [kuandika na kusimulia ni mtambo tu wa kuiwasilisha kazi hiyo]. Kuandika sawa na kuchonga au kuchora ni njia ya kueleza dhana tu, na jinsi ambavyo mchoraji hutumia rangi katika kazi yake, mtunzi wa kazi ya fasihi hutumia maneno kueleza dhana na hisia zake. Maneno hayo huenda akayaandika, akayaimba au akayazungumza. Kwa hivyo, fasihi iwe imeandikwa au imesimuliwa bado ni fasihi.

8

Naye Odaga (1985:xxi) anasema kwamba; Fasihi ni sanaa ambayo mtambo wake ni neno na kiini chake ni binadamu. (Tafsiri yetu) P'Bitek (kama hapo juu) anasema; Fasihi husimamia kazi zote bunifu anazozitumia mwanadamu kujieleza kwa maneno ambayo yaweza kuimbwa, kusemwa, au kuandikwa. (Tafsiri yetu) Toleo la kumi na nne la Compton's Encyclopedia (1974:305) yaeleza fasihi kwa njia pana huku fasihi ikichuliwa kama; iliyo zaidi ya lugha. Ni dhana na hisia zilizovingikwa katika muziki wa lugha. Na huchukua umbo la maneno na picha zilizowekwa pamoja na ubunifu. Fasihi ni jinsi ya kuona, kuhisi, kufahamu. (Tafsiri yetu) Kwa muhtasari twaweza kusema kwamba pana kauli hizi za kimsingi ambazo hujitokeza katika fafanuzi za wataalam hawa na wengine wengi kuhusu dhana ya fasihi: - Fasihi ni sanaa inayodhihiri ubunifu - inayotumia maneno kuwasilisha mambo yake - na ambayo hulenga binadamu kama kiini chake n.k. Kama tulivyotaja hapo awali maana ya neno au dhana yoyote hutegemea mambo mengi na hivyo basi fasili hii yetu ya fasihi huenda isichukuane na maoni ya mwingine anayechagua kuitazama fasihi kwa njia tofauti. Lakini hata mhakiki atumie mtizamo gani, fasili yake pamoja na hitimisho lake litategemea anachukua fasihi kumaanisha nini

9

pamoja na jukumu la mtunzi wa fasihi hiyo. Katika misingi hii, huenda likawa jambo mwafaka kuzingatia baadhi ya vigezo vilivyowahi kutumiwa katika kufafanua fasihi ili tupate msingi wa kufanya uhakiki. Pametokea vigezo tofauti vya kuifafanua fasihi kutegemea msisitizo anaotaka kuweka mfasili pamoja na maendeleo na mabadiliko ya maisha kihistoria. Kuna wale wanaosisitiza umbo la nje la fasihi ambao wamekita nadharia zao katika muundo huo ilhali wengine wanasisitiza umbo lake la ndani. Pana wale wanaochagua kuzingatia wahusika katika kutungwa kwa kazi hiyo, yaani mtunzi, hadhira yake na hata athari za jamii. Ndiposa twapata vigezo vilivyotumiwa ama vyalenga maumbo ya fasihi, maudhui yake au yote mawili. Ni muhimu kueleza kwamba hivi vigezo tutakavyovitaja hapa, mara nyingi vimejitokeza katika utanzu wa uhakiki, hivi kwamba maelezo ya 'fasihi ni nini' yanatumiwa kutathimini kutimizika kwa masharti yanayozingatiwa na mtunzi anapotunga kazi yake. Kwa hivyo kama utunzi wa fasihi husisitiza maudhui mbali mbali basi huenda mhakiki akatumia kigezo hicho hicho katika kazi yake ya uhakiki kubainisha kufaulu kwa kazi hiyo katika lengo hilo. Sasa tuangalie baadhi ya vigezo vinayotumiwa katika kuifafanua fasihi. 1.1 FASIHI KAMA SANAA ITUMIAYO MANENO Aghalabu, wataalamu wametumia kigezo cha `neno' kama njia ya kutofautisha fasihi na sanaa nyingine kama vile uchoraji na uchongaji. Wanasema kwamba fasihi ni sanaa inayotumia maneno ili kuwasilisha maudhui na hoja zake. Wataalamu wanaoshikilia kigezo hiki ni wale wanaopinga kauli ya kimagharibi ya kuhusisha fasihi na taaluma ya maandishi. Kwa hivyo, tunaposema kwamba fasihi ni sanaa inayotumia maneno huwa tayari tumeliacha wazi swala kuhusu maneno yaliyoandikwa au yaliyosimuliwa. Neno, liwe limeandikwa au limetamkwa, ni neno. Lakini sio kila neno huenda likaorodheshwa kama fasihi. Fasihi huwasilishwa kwa maneno lakini maneno hayo hutumiwa kwa njia maalum ili kuyatenganisha/kuyabainisha na maneno ya kawaida. Kwa hivyo lazima pawe na sura maalum zinazounda maneno ya fasihi ili kuyatofautisha na maneno ya kawaida. Ili kujitandua kutoka katika utata huu, ni muhimu kuichukulia fasihi sio kama maneno bali

10

kama sanaa itumiayo maneno. Na matumizi ya maneno hayo katika fasihi huashiria usanii wa namna fulani. Usanii huo ndio unaofanya maneno ya fasihi yawe tofauti na maneno ya kawaida japo mofolojia na fonolojia yake ni sawa. Maneno yanayotumiwa katika fasihi ni maneno zaidi ya maneno mengine kwani yanatumiwa kisanaa. Lakini hamna maneno maalum yaliyotengewa fasihi na ambayo hayapatikani katika utanzu mwingine wowote wa maisha ya jamii. Ukweli ni kwamba katika fasihi, maneno ya kawaida hutumiwa kisanaa. Kirumbi P.S (1975:10) anatutolea mfano wa jinsi maneno yanaweza kutumiwa kisanaa. Ametutolea mifano miwili ya shukrani zilizotolewa na watu wawili tofauti; wa kwanza anasema: Ndungu mpenzi, Nimepokea msaada wako nami umenisaidia sana sikutazamia kupata msaada katika shida hii iliyonikuta. Ama Mungu mkubwa. Ndugu, asante sana kwa msaada wako. Kwa kweli nakushuru sana tena sana. Mungu akubariki. wa pili naye anasema: Ndugu, Sijasikia mkono ukipewa shukrani na mguu kwa kuutoa mwiba - lakini ni ujinga wa mguu kufikiria unastahili kutolewa mwiba, maana kuna miili isiyo na mikono, na miguu hiyo ichomwapo na miiba hutaabika sana. Hivyo sioni kustahili kwangu bali ni rehema na neema kuwa na ndugu, nami nimepata na kujifunza zaidi upendo wako. Watu hawa wawili wametendewa jambo la kuwafaa na wote wametumia maneno kutoa shukrani zao. Hata ingawa ujumbe wa maneno yao ni mmoja, twaona kuwa maneno ya mmoja ni ya kisanaa ilhali ya mwingine ni ya kawaida. Maneno hayo yanapatikana katika msamiati wa jamii husika lakini jinsi yalivyoteuliwa na kutumiwa ndipo tofauti inatokea. katika mfano wa pili kwa mfano, mtunzi anachagua kufananisha kitendo

11

alichotendewa na ndugu yake na kitendo cha mkono kuondoa mwiba mguuni. Mguu unapochomwa ni mwiba huumia na huhitaji kuondelewa (kusaidiwa), kwani hauwezi kujitoa mwiba ule wenyewe. Hivyo ndivyo ilivyo katika fasihi; kwamba maneno hutumiwa kwa njia maalum (ya kisanaa) inayotoa mguso fulani kwa hadhira. Wakati mwingine kazi ya fasihi huweza kuendelezwa kwa matendo badala ya maneno. Kwa mfano tamthilia huhusisha maneno na matendo pamoja ili kuwa kamili. Bila matendo, tamthilia haijakamilika. Kwa hivyo huenda maneno yakawa nguzo moja tu ya fasihi na kama sivyo, tamthilia itaachwa nje ya fasili ya fasihi. Lakini ni muhimu kukumbuka kwamba hata hayo matendo katika tamthilia huweza kueleweka katika misingi ya maneno. Kwa hivyo kiini cha fasihi ni maneno. Na maneno hayo yanatumiwa kisanaa.

1.2

FASIHI KAMA SANAA: NADHARIA YA UMITHILISHAJI Njia moja ambayo pengine ni kongwe sana na iliyopata kutumiwa kufafanua

fasihi kama sanaa ni ile ya kuiona fasihi kama aina ya umithilishaji. Kwa mtizamo huu, fasihi hufafanuliwa katika uhusiano wake na maisha; kwa kuiona kama njia ya kujenga tena au kuhuisha tukio au hali fulani ya maisha kwa kutumia mchoro na rangi. Huu ni mtizamo ulioendelezwa na Aristotle na kufuatiliwa na wafuasi wake. Abrams M.H (1981) anasema hivi kuhusu umthilishaji; Katika kazi yake ya `Poetics', Aristotle anaeleza ushairi kama umithilishaji wa vitendo vya mwanadamu. Kwa `umithilishi' anamaanisha `uwakilishi', kwa msingi yake. [tafsiri yetu] Kwa hivyo kwa maoni ya Aristotle, shairi humithilisha kwa kuchukua kitendo fulani cha mwanadamu na kukionyesha upya katika `mtambo' mpya - ule wa maneno. Mtizamo huu wa kuiona fasihi kama sanaa ya umithilishaji waweza kufasiriwa kwa njia mbili kuu; kwanza, twaweza kuuchukulia kijuujuu na kupendekeza kwamba fasihi hujaribu kuiga na kumithilisha maisha; yaani maudhui ya fasihi ni tajiriba za watu

12

waishio. Lakini pendekezo kama hili lazua matatizo kwani hatusemi mengi kuhusu fasihi kwa vile hatutilii maanani kile kinachofanyiwa hayo maudhui. Pia kwa kutumia neno `maisha' twaweza kuuchukulia kijuujuu na kupendekeza kwamba fasihi ni tajiriba za watu waishio. Pia kwa kutumia neno `maisha' twazua utata mkubwa kwani maisha ni kitu tofauti kwa watu tofauti kwani kila mmoja japo wanishi katika mazingira sawa, aghalabu huguswa na mambo kwa njia tofauti. Pili, twaweza kusema kwamba maisha yanaigwa kwa njia ambayo yanaumbwa upya na kutafsiriwa upya kwani hapawezekani kuondoa kitu kutoka mtambo mmoja na kukiingiza katika mtambo mwingine bila kukiadhiri au kukibadilisha. Dhana hii ya pili inakaribiana na mojawapo ya sura muhimu katika fasihi; ile ya kwamba malighafi ya fasihi huundwa upya na hata kubadilishwa. Lakini bado hatuonyeshi ni mambo gani ya maisha humithilishwa. Kuhusiana na hali hii welleK na Warren (1949:95) wanasema; Iwapo inachukuliwa kwamba fasihi, kwa wakati wowote ule, humulika hali ya kijamii iliyopo kwa uhalisi wake, basi hiyo si kweli; ni wazi, vile vile, kwamba si kweli kusema fasihi hudhihirisha baadhi ya uhalisi uliopo katika jamii. [tafsiri yetu] Kwa hiyo, kwa maoni ya wataalamu hawa wawili kauli ya kuiona fasihi kama umithilishaji wa maisha ni ya kupotosha. Wanaendelea kutaja kwamba; Fasihi kwa hakika si picha ya mkondo wa maisha, bali ni ufupisho na muhtasari wa historia nzima. [tafsiri yetu] Wanalosisitiza hapa ni kwamba fasihi si picha ya moja kwa moja ya maisha bali ni muhtasari wa maisha na matukio yake. Lakini na wao hawatuelezi ni vipi fasihi yatofautiana na kumbukumbu iliyoandikwa kuhusu maisha na mwanahistoria. Ni kwamba kazi ya fasihi huzingatia kaida maalum zinazotawala kila utanzu wa fasihi na kuibainisha na kazi ya mwandishi wa historia kwa mfano. Hata hiyo Wellek na Warren (1949:102) wanakiri kwamba, "hatuwezi kupuuza wazo kwamba picha fulani ya maisha huweza kupatikana katika fasihi [tafsiri yetu]."

13

Pana kauli moja ambayo yajitokeza katika kigezo hiki cha kuiona fasihi kama sanaa inayomithilisha maisha. Katika umithilishi huu mtunzi anatumia maneno. Lakini katika dhana hii ingawa yasemekana kwamba fasihi huhusu maisha, hatuambiwi ni kwa kiwango gani. Hata hivyo mfumo huu unaotokana na nadharia ya umithilishaji umekuwa nguzo kwa kazi nyingi za fasihi na zisizo za fasihi. Abrams, M.H (1981) anasema; Hata ingawa nadharia ya umithilishaji ilififia, ilichukuliwa tena ni R.S Crane na wahakiki wengine wa Chicago waliotumia misingi ya kiaristotle katika tathimini zao. Wahakiki wengi wa ki-marx huiona fasihi kama umithilishaji. (Tafsiri yetu) Kwa hivyo hata ingawa pana wale wanaopinga kuwa fasihi ni umithilishaji, kauli hii inatoa nguzo kwa mitizamo mingine kuhusu fasihi. Twaweza kusema kwamba pana uhusiano mkubwa kati ya umithilishaji na uhalisia (jambo ambalo huhimizwa sana katika baadhi ya kazi muhimu za fasihi). Kazi nyingi za fasihi huweza kuhusishwa na umithilishaji. Methali na vitendawili ni tanzu za fasihi simulizi ambazo zinatumiwa sana na jamii kwa shughuli mbali mbali. Twapata kwa hakika kwamba jinsi methali zilivyo ni mfano halisi wa umithilishaji kwani dhana inayosimamiwa na methali huwakilisha hali halisi ya maisha. Maneno yanayojenga methali, vitendawili na hata misemo ni mfano wa aina fulani ya umithilishaji. Methali kama vile `mwamba ngoma ngozi huivutia kwake' imeundwa kama mithili ya moja kwa moja ya maisha ya mwanadamu. Kwamba mtu anapovuta ngozi wakati anapounda ngoma huwa anaivutia upande wake, (huo ni ukweli wa mambo) na hawezi kuivuta ikaendea mwenzake kwani itapuuza dhana ya kuvuta. Kwa hivyo kiini cha methali hii ni ukweli halisi wa mambo. Hivyo basi pana hali ya umithilishaji katika utanzu huo wa fasihi. Kwa jumla twaona kwamba fasihi ni sanaa ambayo yaweza kuelezwa kama inayomithilisha. Umithilishaji huu hata hivyo si wa moja kwa moja kwani kama ingekuwa hivyo, basi hapangekuwa na tofauti kati ya fasihi na historia. Hapo ndipo twaingilia kigezo cha tatu cha kuieleza fasihi.

14

1.3

DHANA YA UBUNILIZI Hata ingawa kazi ya fasihi kwa kawaida huwa yamithilisha au kujaribu kuumba

upya maisha kwa njia moja au nyengine, twatambua ukweli kwamba yaliyotungwa si maisha halisi moja kwa moja. Kwa mtizamo huu yaelekea kwamba fasihi si maisha halisi bali ni tokeo la ubunifu wa mtunzi, yaani mtunzi ana uwezo wa kubuni visa na wahusika wake kwa njia ambayo haikanganyi hali halisi ya maisha. Hata hivyo, ubunifu huu lazima uongozwe na kaida za hali halisi ya maisha yaani kama asemavyo Horace (1975:103): Chochote utakachochagua kwa minajili ya kupendeza, hakikisha kwamba kipo karibu na ukweli. [tafsiri yetu] Yaani mtunzi anapaswa kuufanya ulimwengu wake wa kubuni kuwa picha halisi ya maisha katika ukamilifu na ukweli wake, hata ingawa alivyoyashughulikia ni ya kubuni tu. Horace (1975:95) anafafanua zaidi kauli hii asemapo kwamba; Washairi na wachoraji wamekuwa wakifurahia uhuru wa utunzi na kufanya majaribio jinsi watakavyo. Hili nalifahamu, na mimi kama mshairi hufurahia uhuru huo; lakini si kwa kiwango ambacho kwacho viumbe visivyotangamana vinawekwa pamoja, hivi kwamba ndege na nyoka wanawekwa pamoja, wanakondoo pamoja na simba marara. [tafsiri yetu] Anachosisitiza Horace ni kuwa, hatuwezi kumnyima mtunzi uhuru wa kubuni, lakini mtunzi akumbuke kwamba ubunifu wake usikiuke kaida zinazotawala maisha halisi ya jamii. Kumpa mtunzi uhuru wa ubunifu na kisha umtarajie afuate kaida fulani ni kumnyima uhuru kamili. Kama mtunzi atakanganya hali halisi ya maisha kama mbinu yake ya kutunga, basi na tumpe uhuru huo alimradi kazi yake twaielewa kwa mtizamo huo. Kwa hivyo, fasihi si kazi inayohusu mambo ya kipekee bali ni uwasilishaji wa

15

maisha ya jamii kwa njia bunifu isiyo ya moja kwa moja. Ndiposa Aristotle (1975:103) anasema: Ni wazi kwamba, si jukumu la mshairi kuendeleza yaliyotokea bali huendeleza yanayoweza kutokea-yaani kinachoweza kutokea katika msingi ya haja au uwezekano. [tafsiri yetu] Hapo ndipo fasihi hutofautiana na historia kwani wakati fasihi huendeleza linaloweza kutokea, historia huendeleza kilichotokea; na fasihi ikieleza lililotokea hulieleza kisanaa, sio moja kwa moja. Hivyo basi, fasihi ni utanzu unaoendeleza maisha kwa njia bunifu iliyojikita katika msingi na kaida zinazotawala maisha halisi. 1.4 DHANA YA MUUNDO Ili kueleza maana ya fasihi, wataalamu wengi wamejaribu kuzingatia baadhi ya vigezo vinavyoitambulisha, hasa ikiwekwa katika mkabala mmoja na tanzu nyengine za maisha ya jamii. Twaweza kusema kwamba dhana ya ubunilizi ni njia nzuri ya kutofautisha fasihi na uhalisia pamoja na ulimwengu halisi. Lakini kupitia kwa dhana hii hatujaelezwa hasa kinachofanyiwa malighafi ya kazi ya fasihi. Ili kutimiza hilo, dhana nyengine imependekezwa; kwamba kazi ya fasihi yapaswa kuchukuliwa kama muundo, kama mpangilio maalum. Kila kazi imepangwa kwa hali ya juu sana na viungo vyake vinategemeana hivi kwamba kazi kamilifu huwa ni mwafaka zaidi kuliko kiungo chake kimoja. Aristotle amelizungumzia swala hili hata ingawa anazingatia zaidi ploti. Aristotle (1975:29) anasema: Chombo kizuri, kiwe kiumbe au kitu kizima kilichojengwa kwa vipande. kazi ya fasihii yapaswa kutolewa kama kitu kimoja. Ploti, kama mithili ya kitendo, lazima imithilishe kitendo kimoja; na muungano wa vipande vya kitu kizima uwe hivi kwamba kipande kimoja kikiondolewa pale, kile kitu kizima hutengana. Kwani kipande ambacho hakitoi athari kiondolewapo, bila shaka si kipande halisi cha kizima. [tafsiri yetu]

16

Tukitizama fasihi kwa njia hii, tunatambua umoja na uwiano wa kila kazi unaoifanya ieleweke na iwe na muundo maalum. Hivyo basi kazi ya fasihi ni muundo wa vipande vinayopatana na kuhusiana ili kujenga kitu kimoja. Hivyo basi kipande kimoja cha kazi hiyo huwa hakina maana yoyote kivyake mpaka kihusishwe na vingine. Kama ambavyo dhana ya ubunilizi hutusaidia kutofautisha fasihi na matukio halisi maishani, dhana ya muundo hutuwezesha kutofautisha fasihi na matumizi mengine ya lugha. Inatutolea ile hali ya usababishano, kwamba kazi ya fasihi ni utungo ulioundwa kwa visa vinavyowiana hivi kwamba kimoja hutangulia chengine. Pia, kisa kimoja hutokea ili kusababisha chengine na vyote vinahusiana kwa njia ambayo kimoja hakiwezi kueleweka bila chengine. Haya yote yanawezekana kupitia lugha inayotumiwa. Kwa hivyo katika muundo, tunazingatia jinsi lugha inavyotumiwa. Kwa ufafanuzi zaidi kuhusu lugha katika fasihi rejelea sehemu ya `fasihi kama sanaa itumiayo maneno'. Mpaka sasa tumekuwa tukizingatia vigezo vya kuainisha fasihi ambavyo twaweza kuviita vya umbo la ndani. Sasa tutaingilia umbo la nje la fasihi hasa kwa kuzingatia mtunzi wake pamoja na hadhira yake. 1.5 NADHARIA YA UHALISIA-NAFSI Kigezo kingine kinachotumiwa katika kuianisha fasihi ni kuiona fasihi ile kama zao la mtunzi binafsi. Fasihi kwa mtizamo huu huzingatia saikolojia na sifa za mtunzi huyo. Kigezo hiki kimezingatiwa hasa katika nadharia ya tathimini saikolojia . Ni wazi kwamba chanzo cha kazi ya sanaa ni yule anayeiumba, yaani mtunzi wake, na hivyo basi maelezo yanayopatana na hulka na maisha ya mtunzi yamezingatiwa kwa muda mrefu sana kama nguzo moja ya kueleza maana ya fasihi. Waitifaki wa nadharia hii hushikilia kwamba kazi ya fasihi yaweza kuelezeka tu iwapo itazingatiwa kwa mkabala mmoja na maisha ya mtunzi wake. Hivyo basi fasihi huonekana kama kielelezo cha uhalisia wa maisha, jinsi yanvyotafsiriwa na nafsi ya mtu bila kujali ukweli kama unavyodhihiri kwa nje. Jinsi mtunzi anavyojieleza kupita kazi ya fasihi linakuwa jambo muhimu katika nadharia hii. Katika mtizamo huu huu, fasihi imezingatiwa kama hisi; yaani ni kielelezo cha hisi za mtu binafsi (mtunzi). Jinsi mtu anavyoona na kuyahisi maisha linakuwa jambo la kuzingatiwa kama fasihi. Wataalam wa jadi wa fasihi kama vile Aristotle wanashikilia

17

wazo hili hili kuhusu fasihi. Aristotle aliamini kwamba fasihi au ushairi hasa ni utanzu ambao kwao binadamu hutoa hisia zake za ndani kuhusu maisha. Hivyo basi ushairi ukawa ni kielezo cha uhalisia wa nafsi ya mtunzi, jambo ambalo limezingatiwa katika kueleza fasihi ni nini. Hata wahakiki wanaozingatia nadharia ya tahakiki-saikolojia kama vile Sigmud Freud wanashikilia kwamba kazi ya fasihi ni kielezo cha ndoto na matamanio yasiotimizwa ya mtunzi. Yaani kazi ya fasihi si chengine bali imejaa ndoto za mtunzi pamoja na majaribio ya kutimiza matamanio yake. Kwa mtizamo huu, fasihi ni hisi, hisia na mataminio ya mtunzi; yaani maisha yake. Hapa ndipo twapata hata biografia zikichukuliwa kama kazi za fasihi. Mtizamo kuu kuhusu fasihi haujapokelewa kwa mikono miwili na baadhi ya wataalam. Jefferson (1982:99) anasema: Utunzi na usomaji wa fasihi hauna uhusiano wowote na nafsi halisi ya mtunzi na fasihi huwepo bila kutegemea mazingara halisi pamoja na hulka ya mtunzi. [tafsiri yetu] Kwa hivyo, kazi ya fasihi haina uhusiano wowote na nafsi ya mtunzi wake. Anasema kuwa kazi ya fasihi hujisimamia yenyewe kama kazi ya fasihi na haihitaji kuhusishwa na mtunzi wake ili kueleweka ama kutungwa. Lakini hatuwezi kulitupilia mbali wazo hilo kwani kila kitendo cha kutunga hutokana na fikira, maoni, tajiriba, na hisia za mtunzi, jambo ambalo lina ubinafsi maalum unaodhihiri, japo kwa kiwango duni, hulka ya mtunzi huyo. Nao Wellek na Warren (1949:78) wana maoni haya kuhusu mtizamo huo wa fasihi: Wazo kwamba sanaa kwa ujumla ni uhalisia-nafsi unaotoa hisi na tajiriba za mtu, ni la kupotosha. Hata panapotekea uhusiano wa karibu sana kati ya sanaa na maisha ya mtunzi, hili lisichukuliwe kumaanisha kwamba sanaa ni mwigo wa

18

maisha. Mtizamo huu husahau kwamba kazi ya sanaa ni kazi kivyake wala si kusanyiko la tajiriba za mtunzi. [tafsiri yetu] Maoni ya wataalum hawa yanadhihirisha wazo la awali kwamba fasihi ni kazi inayojisimamia na iliyo na kaida zinazoitawala. Hivyo basi, tamthilia, riwaya au shairi huwa zinaongozwa na kutawaliwa na kaida za kifasihi zinazohusu kila utanzu. Tukichunguza mtizamo huu kuhusu fasihi twaona kwamba unapuuza baadhi ya hoja halisi za kimantiki. Kazi ya sanaa huenda ikawa si maisha halisi ya mtunzi bali ni maoni au mtizamo wake kuhusu maisha. Huenda ikawa pia ni kinyago cha kuficha nafsi yake halisi au huenda ikawa picha ya maisha anayotaka kuyakimbia. Isitoshe, tusisahau kwamba huenda tajiriba ya maisha halisi ya mtunzi ikawa tofauti na ile ya sanaa; yaani tajiriba halisi maishani hutizamwa kwa jinsi ambavyo zitafaa fasihi na huwa kwa kiasi fulani zimeongozwa na kuathiriwa na kaida za kisanaa zinazotawala kazi yake. Ama kweli kazi ya fasihi inayoorodhesha matukio kama yalivyo bila usanii si sanaa bali ni kumbukumbu au historia. Hata hivyo hatuwezi kupuuza kabisa kigezo hiki kwani kinachangia katika kueleza fasihi ni nini. Lililo muhimu kutambua ni kwamba kigezo hicho hakiwezi kutumiwa peke yake kueleza fasihi ni nini. Ni lazima kihusishwe na vigezo vingine mbali mbali ili kutoa picha kamili na pana ya fasihi. 1.6 NADHARIA YA MGUSO Mtizamo mwingine kuhusu fasihi ambao twaweza kuuita wa umbo la nje ni kuitizama fasihi katika uhusiano wake na umma wake ambapo msisitizo unatiliwa mguso unaotolewa na kazi ya fasihi kwa hadhira yake. Kila kazi ya fasihi hulenga kwa njia moja au nyengine mtu au watu fulani (hadhira) hata kama hadhira hiyo ni nafsi ya mtunzi husika. Kazi ya fasihi hutoa mguzo wa aina fulani kwa hadhira ili ifikirie na kujiuliza maswali au hata kutoa funzo fulani. Kwa kuunga mkono maoni haya, Vasquez, A.S (1973:113) anasema: .... kazi ya sanaa huathiri watu na inachangia katika kuhimiza au kupuuza dhana zao, maazimio yao, hata maadili yao - ina msukumo wa kijamii ambao huathiri watu kwa nguvu

19

zake za kihisia na kiitikadi. Ama kwa hakika, hakuna anayebaki vile vile baada ya `kuguswa' na kazi ya halisi ya sanaa. [tafsiri yetu] Kuna nyakati ambapo imependekezwa kwamba hadhira hutekwa kabisa na wahusika katika kazi ya fasihi mpaka hadhira hiyo ikajitambulisha na wahusika hao kiasi cha kupoteza utambulishi wake asilia, hata kama ni kwa muda tu. Hata Wellek na Warren (1949:102) wana maoni yayo hayo wasemapo: Watu wamewahi kubadilisha mienendo yao katika maisha kwa kuathiriwa na wahusika wa kubuni katika fasihi. [tafsiri yetu] Tunachokisisitiza hapa ni wazo lile lile kwamba kazi ya fasihi hutoa mguso kwa hadhira yake, na huu mguso ndio unaotumiwa kama kigezo cha kueleza maana ya fasihi. Ndiposa twapata wataalamu wengine wakisema kuwa fasihi ni kazi ya kufurahisha. Horace (1975:103) anasema "washairi hulenga kusaidia au kufurahisha msomaji, au kusema kile kinachopendeza na wakati huo huo kusema kinachofaa [tafsiri yetu]." Tatizo linalozuka katika mtizamo huu ni kwamba ni vigumu kusema kama kweli pamesababika au kutokea mguso wowote kwa hadhira baada ya kusikiza, kuona au kusoma kazi ya fasihi. Mguso aghalabu ni jambo la kihisia na kibinafsi na huwa vigumu sana kutathiminiwa. Isitoshe, yahitajika kupima na kutathimini kiwango cha mguso huo, kama upo, ili kupata hitimisho lenye mashiko. Jambo hili huenda likawa gumu sana kutimizwa. Lakini iwapo ni watu ambao tunawafahamu ni rahisi kuthibitisha kama wamebadili maoni au mienendo yao kuhusu jambo fulani ambalo limegusiwa katika kazi ya fasihi. Baada ya kuorodhesha vigezo hivi mbali mbali vinavyotumiwa kueleza fasihi, pana jambo ambalo linadhihirika kila mara na katika kila kigezo -- kwamba fasihi ina uhusiano mkubwa na jamii, na hakuna fafanuzi moja inayoweza kusimamia kazi zote za fasihi, kila moja yategemea muktadha na dhamira ya mfafanuzi. Haya tuliyoyatoa hapa ni maongozi ambayo yanaweza kusaidia katika kuielewa fasihi kama dhana pana lakini iliyo na sura maalum zinazotambulika. Tungependa kupitia dhana hii ya fasihi na jamii

20

kwa sababu mbali na kuwa muhimu katika kazi yetu, dhana hii imetumiwa pia katika kueleza maana ya fasihi. 1.7 FASIHI NA JAMII Fasili nyingi za fasihi zimeegemea kuileza katika uhusiano wake na jamii. Fasili hizi zimeonyesha kwamba fasihi ni taasisi ya jamii na uhusiano wake na jamii hauwezi kupuuzwa. Mmoja wa wanaounga mkono dhana hii ni Escarpit, R (1974:4) anayesema kwamba: Fasihi lazima ichukuliwe kama iliyo na uhusiano usiotatanika na maisha ya kijamii.[tafsiri yetu] Fasihi ni taasisi ya kijamii, inayotumia lugha (ambalo ni zao la kijamii) kama mtambo wake. Isitoshe, imesemekana (na ni kweli) kwamba fasihi huwakilisha maisha. Maisha kwa upana wake huhusu uhalisi wa kijamii, hata ingawa ulimwengu halisi na hata ulimwengu wa ndani wa mtu binafsi ni mambo yanayoweza kuzingatiwa katika fasihi. Mbali na hayo twafahamu kwamba iwapo fasihi hulenga watu fulani, basi bila shaka hiyo fasihi yahusu jamii fulani lau sivyo hapana haja kutungia watu kazi isiyowahusu ndewe wala shikio. Jambo lingine la kutaja hapa ni kwamba mtunzi mwenyewe ni mwanajamii kwa ambavyo ana nafasi na tabaka fulani katika jamii yake; yeye hutambuliwa na jamii kama mmoja wao. Hawezi kuepuka nafasi hiyo yake katika jamii wala hawezi kukwepa athari ya jumuiya katika utunzi wake kwani kama mtoto mchanga yeye anafundishwa maadili na itikadi za jamii yake ili kuweza kuenea katika jamii hiyo. Na kama ambavyo tumetaja tayari, mtunzi hulenga hadhira fulani hata iwe ndogo vipi. Mara nyingi fasihi hutokana na uhusiano wa karibu sana na taasisi maalum za kijamii. Taasisi za kiuchumi, kisiasa, na kijamii zimekuwa na uhusiano mkubwa sana na utoaji wa fasihi na kila kazi ya fasihi kwa njia moja au nyengine, hudhihiri ukweli huu. Maendeleo na mabadiliko ya jamii yametokea kuwa maendeleo na mabadiliko ya fasihi hivi kwamba hatuwezi kutenganisha fasihi na jamii inamoibukia. Uhusiano huu unatokea kwa sababu pindi maisha ya jamii yabadilikapo, mielekeo, tamaduni na hata maadhili ya

21

jamii hubadilika pia. Aidha, mabadiliko ya fasihi toka simulizi hadi andishi ni zao la mabadiliko katika maisha ya jamii ambapo taaluma ya kusoma na kuandika ilitokea. Kwa hivyo fasihi inalo jukumu kuu katika jamii ambalo sio la kibinafsi, bali ni la kijamii. Katika kuiunga mkono kauli hii, Wellek na Werren (1949:95) wanasema kwamba: Uhusiano kati ya fasihi na jamii hujadiliwa kwa kuanza na kaulo aliyoitoa De Bonald kwamba `fasihi ni kielelezo cha jamii'.[tafisiri yetu] Kwa hivyo ni muhimu kuichukulia fasihi kama zao la jamii ambalo pia huathiri na kuathiriwa na jamii. Hata katika nyingi za tahakiki za fasihi ambazo twaweza kuziita za kijamii (kama za Ki-marx) pamesisitizwa kauli kwamba mtunzi anapaswa kuendeleza maisha ya wakati wake kwa ujumla wake; kwamba anapaswa kuwa kiwakilishi cha wakati wake na jamii yake. Kwa maoni ya waitifaki wa tahakiki hizi, `uwakilishi' huelekea kumaanisha kuwa mtunzi anapaswa kutambua na kuona hali halisi za maisha katika jamii yake na kuzizingatia katika utunzi wake. Maoni ya Hegel na Taine katika Wellek na Warren (1949:95) ni mfano unaochangia zaidi kauli hii wanaposema: Katika uhakiki wa Kihegel na hata ule wa Taine, utukufu wa kijamii na wa kihistoria huenda sambamba na utukufu wa kisanaa. Msanii huendeleza ukweli, na huo ukweli ni wa kijamii na kihistoria. [tafsiri yetu] Tunaloweza kuongeza ni kwamba pana tatizo linalokumba juhudi yoyote ya kujaribu kutenganisha fasihi na jamii kwani fasihi huathiriwa na mandhari ya kijamii pamoja na mabadiliko na maendeleo yake. Isitoshe, mtunzi ni mwanajamii anayetumia lugha ya jamii kutunga kazi yake ili kuwafifikia wanajamii husika. Ukweli huu wanaogusia waandishi hawa utategemea mtizamo, matarajio, na tajiriba za anayehusika kwani hali mbali mbali katika jamii hutoa maana mbali mbali kwa watu mbali mbali hata kama ni wa jamii moja. Hivyo basi ukweli hubainika tu kimuktadha. Wale wanaosisitiza kigezo cha fasihi na jamii katika kuieleza fasihi, wametoa kauli kwamba pana aina mbali mbali za fasihi ambazo zinachukuana na jamii

22

mbalimbali. Dhana kama vile fasihi ya kirusi, fasihi ya kiafrika, fasihi ya kiingereza n.k. ni baadhi ya mifano ya kazi za fasihi zinazohusishwa na jamii fulani. Fasihi kama hizi hulenga jamii fulani pana zenye kaida na maadili yanayopatana katika muundo wa kijumla kwani katika jamii hizo huwa kuna vijamii vidogo vidogo. Kwa mfano katika fasihi ya Kiafrika pana fasihi ya jamii ya nchi mbali mbali ambazo zimeibuka kihistoria kwa jinsi maalum ambao ni tofauti na ya nchi nyengineo. Na katika nchi hizo pana vijamii vingine vidogo vidogo vinavyobainishwa na lugha, mazingira, na itikadi. Hivyo kutaja kwamba pana fasihi ya kirusi ni kutoa kauli ya kijumla tu. Vile vile pana fasihi zinazochukuana na mifumo mbali mbali ya maendeleo ya kijamii kama vile fasihi ya kibwanyenye, fasihi ya kisosholisti, fasihi ya kikapitolisti n.k. Ama kwa hakika mojawapo ya majukumu ya fasihi ni kule kuihifadhi historia ya jamii husika. Yaani kwa kuitizama kazi ya fasihi twaweza kupata picha maalum ya historia ya jamii husika. Kwa mfano katika fasihi ya kiswahili twaweza kupata vipindi maalum vya kihistoria. Dunia Mti Mkavu (Said A. Mohamed) ni mfano wa kazi inayoonyesha historia ya unyonyaji na unyanyasaji wa mufumo wa ukoloni, Mashetani (Ebrahim Hussein) ni mfano wa Kipindi cha Ukoloni-Mamboleo, na utenzi wa AlInkishafi (Sayyid Nassir) ni kielelezo cha historia ya Mji wa Pate. Hivyo basi twaona kwamba kauli kuwa fasihi ina uhusiano mkubwa na jamii ni dhana yenye mashiko sana. Hata hivyo hatulengi kusema kwamba kazi ya fasihi ni hitoria kwa kule kuhitajika kutoa picha halisi ya maisha ya wakati husika, kwani japo mada ni matukio halisi ya kihistoria, namna ya kusawiri mada hizo na matini maalum (kati ya mengi) yaliyozingatiwa, ndiyo yaibainisha kama kazi ya fasihi. Maoni yaliyotolewa hapa ni mwongozo wa kuitizama fasihi katika vigezo ambavyo bila shaka huathiri fasihi. Iwapo tutakubali kwamba kazi ya fasihi si amali ya mtu binafsi, basi tutakuwa tayari tumeonyesha kwamba fasihi na jamii ni vitu visivyotengana. Na hata pakitokea kwamba maisha ya mtu binafsi yametumiwa kama nguzo ya kutunga kazi ya fasihi, hatuwezi kusahau kwamba tajiriba zake zimepaliliwa na maisha yake kama mwanajamii, awe anichukua au kukiuka maadili na matarajio ya jamii hiyo.

23

1.8

HITIMISHO Baada ya kutizama mitizamo na vigezo mbalimbali vilivyotumiwa katika kueleza

fasihi ni nini, twaweza kutoa muhtasari wa kauli muhimu zilizotokea ili kupata fasili ya fasihi. Baadhi ya maoni yaliyotolewa kuhusu fasihi, yameathiriwa sana na historia. Kwamba matarajio na majukumu yaliyowekewa fasihi yanabadilikabadilika ili kuchukuana na mabadiliko ya kihistoria. Kwa mfano kule kuiona fasihi kama amali ya jamii zenye taaluma ya maandishi lilikuwa tokeo la kiburi cha wanajamii waliotaka kutenga jamii yao `iliyostaarabika' na jamii za `kishenzi' ambazo hazikuwa na ujuzi wa kusoma na kuandika. Vile vile, kule kuanza kuitizama fasihi kama uhalisia-nafsi wa mtunzi ni matokeo ya juhudi ya binadamu kuingia katika ubinafsi na upweke ulioletwa na mabadiliko katika mkondo wa maisha. Hapo awali, wanajamii waliishi kwa pamoja na kushirikiana, lakini baada ya idadi ya watu kuongezeka pamoja na jamii kupiga hatua katika sayansi, dhana ya umoja katika jamii ilitoweka na badala yake pakaingia ubinafsi. Hivyo basi badala ya mtunzi kulenga mambo yanayohusu jamii nzima katika kazi yake, akaanza kuitumia fasihi kama chombo cha kuendeleza maisha yake ya kibinafsi na kuondoa upweke. Kwa upande mwingine twapata katika nyakati za umwinyi na ukoloni (ambapo watu wachache waliwakalia walio wengi katika jamii) fasihi ilitumiwa kuburidisha watawala na wenye nguvu na ilipata kuhimizwa sana kwa kutumia hizo nguvu. Bila shaka hili halikufaa kwani fasihi haibagui katika athari zake. Ndiposa palitokea mawazo kwamba fasihi yapaswa kuzingatia hali halisi ya maisha ya wakati wake. Ikawa basi katika ukandamizi huo palizuka fasihi ya upinzani ya walio wengi kupinga unyanyasaji na dhuluma. Kwa hivyo, mawazo yote yaliyotokea kuhusu `fasihi ni nini' hayakutokea kwa sadfa bali ni kwa kufuatana na mabadiliko ya maisha kihistoria. Jambo lingine muhimu ambalo tungelitaja hapa ni kwamba baadhi ya kazi nyingi za kufasili maana ya fasihi zimeathiriwa sana na maoni ya wasomi wa kimagharibi na wasomi wengi wa Kiafrika kwa mfano huwa wanaifasili fasihi mara nyingi kwa kulenga maoni ya hao wasomi wa kimagharibi. Nayo maoni ya wasomi wa kimagharibi wameegemeza maoni yao kuhusu fasihi na jamii kwa jumla katika falsafa na maoni ya wataalamu mbali mbali.

24

Mikutano kati ya jamii mbali mbali za kilimwengu iliyosababishwa na usafiri, biashara, na utawala (hususa ukoloni) na pia mabadiliko ya kijamii kihistoria yalichochea fikira za wasomi wengi hasa wa kimagharibi ambao walivutiwa na swala la mabadiliko ya kijamii. Maoni ya kuendelea kwa jamii toka hali ya duni (ushenzi) hadi ya juu (ustaarabu) iliyofafanuliwa na wasomi kama vile Darwin iliwatia moyo sana wasomi wa kimagharibi ambao walitaka kuchunguza hali hiyo kwa kuzitafiti jamii ambazo `hazikuwa zimeendelea.' Nadharia hii ya Darwin ilidai kwamba jamii hizi zitaendelea na kufikia kiwango hicho cha juu na hivyo basi wasomi walipapia kuzitafiti jamii hizi duni kabla ya kupata maendeleo. Masomo kama vile anthropolojia yalizuka kuzingatia hali hiyo ya utafiti ambao ulizingatia kuorodhesha maisha ya watu wa jamii za hali ya chini kabla hayajaangamizwa na maendeleo. Ndiposa palizuka utafiti linganishi ambao ulitumia umagharibi kama kioo cha kuzitizama jamii nyinginezo hasa za Kiafrika, kiesia, na za wamarekani asilia. Hivyo basi utafiti katika karne ya kumi na tisa uliegemea zaidi jamii hizo ambazo zilionekana kuwa na maisha ya hali ya chini (ama yaliyo karibu na ya wanyama). Maswala muhimu wakati hua yakawa ni kutizama tofauti kati ya ujumuia na ubinafsi, dini na ukosefu wa dini, usosholisti na ukapitolisti, na himaya za kifalme na za kidemokrasia ambayo yaliadhiriwa sana na maoni ya wasomi wa kisosholojia kama vile Emile Durkheim na wa ulimbikaji mali kama vile Karl Marx. Hata wasomi wa Kiafrika waliendeleza kauli hii kwa kukimbia kurekodi mila na tamaduni zao ambazo waliziona zinaadimika na nafasi zao kuchukuliwa na `maendeleo' ya kimagharibi. Haya yote yalidhihirisha msimamo wa wasomi hawa wote kuhusu jamii na utamaduni. Ni wazi kwamba walichukulia utamaduni kuwa kitu finyu ambacho chaweza kuopolewa na kuhifadhiwa. Mwelekeo huo ni hatari kwani unapuuza hali kwamba watu daima hubadili maoni, maadili, na kaida zao ili kuchukuana na mazingira yao ambayo hugeuka kila wakati. Hivyo ndivyo ilivyokuwa na usomi kuhusu fasihi. Hata hivyo tukirejelea vigezo tulivyotumia kuieleza fasihi hapo juu, twapata hoja kuu zifuatazo zikijitokeza: * Fasihi hutegemea jamii. * Fasihi hutumia maneno kama njia ya kuwaisilisha mambo yake .

25

* Fasihi huhusu maisha ya jamii huska lakin si kwa kutoa * picha ya moja kwa moja kama historia. * Fasihi hulenga hadhira fulani ambayo huiathiri. * Fasihi hutawaliwa na kaida na masharti ya kisanaa. * Mtunzi hutumia ubunilizi wake katika kuitunga kazi ya fasihi. Kwa hivyo kwa kutumia hoja hizi tutajaribu kutoa fasili ya dhana ya fasihi ambayo tutaizingatia katika kazi hii yetu. Kwa maoni yetu, fasihi ni sanaa inayotumia ishara (maneno au matendo) kutoa picha halisi ya maisha kwa njia bunifu na inayofuata mpangilio maalum na lugha ya kifasaha ili kuiathiri hadhira husika. Fasili hii inadhamiria kuchukua tanzu zote za fasihi--fasihi andishi na simulizi. Hata hivyo twafahamu kwamba sio kila kazi ya fasihi hutimiza viwango hivyo tulivyovipitia. Vile vile sio kila kazi ya fasihi huratibiwa kwa kiwango kimoja cha ubora, pana kazi nzuri kisanaa, kimaudhui au vyote viwili. Vigezo tulivyovitoa hapo juu ni mwongozo kwa mhakiki na mwanafunzi wa fasihi anayekabiliana na swala la fasihi na uhakiki. Kwa kuhitimisha tutataja kwamba mitizamo na vigezo mbali mbali tulivyovitaja kuhusu kueleza fasihi vyaweza kutumiwa katika baadhi ya nadharia za uhakiki wa kazi za fasihi. Kwamba iwapo kigezo fulani kitatumiwa kueleza fasihi, basi kigezo hicho hicho kitatumiwa kuihakiki fasihi. Kwa mfano iwapo fasihi imeelezwa kama uhalisia nafsi, basi katika uhakiki wa kazi hiyo maswala ya maisha na saikojia ya mtunzi yatatiliwa maanani. Tungependa kukiri kwamba dhana ya fasihi inazua utata mwingi sana na kamwe hatudai tumetatua utata huo. Katika sehemu hii tumejaribu kuangazia macho baadhi ya vigezo ambavyo bila shaka huchangia katika kuelewa fasihi ni nini. Pamekuwepo na pataendelea kuwepo misingi mbali mbali ya kueleza fasihi kulingana na msisitizo anaochagua mhusika. Pana wale wanaochagua mtindo wa fasihi peke yake. Pana wale wanaochagua maudhui ya fasihi peke yake. Pana wale wanaochanganya vyote viwili; na wote huwa wana haki ya kufanya vile na kujihimili kwa kauli zao mbali mbali. Hivyo basi mjadala u wazi na uanendelea.

26

SURA YA PILI

2.0

NADHARIA ZA UHAKIKI Swala la uhakiki kama fasili ya fasihi ni swala ambalo limeendelea na kukua sana

kihistoria. Ni swala pana sana na ni swala lenye utata mwingi. Uhakiki ni swala lililoendelea kwa sababu kila kuchapo panatokea nadharia au maelezo mapya kulihusu. Kwa mfano, hapo jadi palikuwa na uhakiki uliohusu umithilishi, uasilia, na urasmi. Lakini baadaye pakaingia uhalisia, uhalisia wa kijamii, na ulimbwende. Baadaye pia pakaja umuundo, ufeministi, uhakiki-saikolojia na uhakiki- mamboleo [post-modernism]. Hii ni mifano tu, kwani kila mara panatokea nadharia mpya ya kuhakiki kazi za fasihi na hata zile za awali kuboreshwa. Vile vile, swala la uhakiki ni pana kwa sababu pana nadharia na mitizamo kemkemu ya uhakiki. Kwa mfano, katika nadharia ya uhalisia peke yake, twapata uhalisia wa kijamii na uhalisia wa ujamaa. Swala la uhakiki halikadhalika ni lenye utata kwa sababu mpaka leo hakuna nadharia hata moja inayoweza kuchukuliwa kama inayoweza kueleza kikamilifu uhakiki ni nini na unapaswa kuzingatia nini. Yaani kila nadharia ina upungufu wake pamoja na ubora wake. Isitoshe, hapana njia yoyote halisi ya kuihakiki kazi ya fasihi. La muhimu ni kuzingatia mhakiki analenga kudhihirisha nini na anatumia vigezo gani. Licha ya mambo haya yote swala la uhakiki hutokea kuwa muhimu sana katika kila sura ambapo fasihi huingizwa. Na hatuwezi kutenganisha fasihi na uhakiki kamwe. Ndiposa katika utangulizi wao wa toleo la pili la Modern Literary Theory, wahariri wanakiri kwamba hapo awali uhakiki wa fasihi ulichukuliwa kama uwanja duni mbele ya fasihi lakini kwa hivi sasa, ni uwanja muhimu sana katika fasihi.

27

Nia yetu katika sehemu hii ni kujaribu kueleza uhakiki ni nini huku tukitoa kwa muhtasari mifano ya baadhi ya nadharia zinazotumiwa katika uhakiki wa fasihi. Kwanza pana maswali matatu ambayo twapaswa kuzingatia katika jukumu hili letu: * Uhakiki ni nini? * Ni vigezo vipi huzingatiwa katika uhakiki? * Je, pana njia halisi ya kuhakiki? 2.1 UHAKIKI NI NINI? Uhakiki sawa na fasihi ni dhana ambayo imeelezwa kwa njia tofauti na wataalamu mbali mbali. Hata hivyo, wote wameeleza dhana ya uhakiki kwa kuihusisha na fasihi. Tutaanza kwa kunukuu maoni ya wataalum mbali mbali kisha tuyaunganishe pamoja ili kutoa fasili moja itakayotuongoza katika kuelewa dhana hii ya uhakiki. Peck na Coyle (1984) wanasema; Uhakiki huchukuliwa kama utathimini, ufasili na uainishi wa kazi za fasihi. Haimaanishi 'kuitafutia makosa' kazi hiyo. Uhakiki kama kitendo cha kiakedemia humaanisha maoni ya msomaji kuhusu kinachotendeka kitabuni [tafsiri yetu]. Hapo twaona kwamba uhakiki unahusu tathimini na tafsili ya mambo yanayopatikana katika kazi anayoizingatia mhakiki. Lakini pia twaona maoni yao finyu yanayoiona kazi kama ya kiakademia na pia kuihusisha na fasihi-andishi. Naye Hough (1966:5) anasema kwamba; Uhakiki kuhusu kazi nyingi, ikiwemo haja ya kuuliza, kutathimini, kuweka katika mpangilio sawa na kulinganisha. [tafsiri yetu] Coombes (1953:7) amezingatia zaidi kazi ya mhakiki huku akionyesha kazi ya mhakiki bora anaposema kwamba;

28

Kwa jumla twaweza kusema kuwa mhakiki bora awapo katika shughuli yake huwa anazingatia mambo mawili, au moja ya hayo mawili; hutupatia maoni yake kamili na yaliyo wazi kuhusu mtunzi, tamthilia, riwaya, shairi au tungo ili kutuwezesha tufurahie kazi ile pamoja na kuelewa tajiriba iliyomo katika utunzi pamoja na ile inayozingira utunzi huo. Au kwa kutathimini kazi ile kwa makini, hudhihirisha vipembe vinavyoipa thamani. [tafsiri yetu] Coombes hakomei hapa bali anaendelea kusema kwamba: Uhakiki wa kifasihi si chengine zaidi ya mguso aupatao mhakiki katika kazi ya fasihi anayoizingatia. [tafsiri yetu] Kulingana na Coombes, kazi ya kuhakiki haiongozwi na hoja za kisayansi bali hujikita katika hisia. Kwa hivyo twapaswa kuihakiki kazi yoyote ile ya sanaa kwa misingi ya athari inayotoa kwa hisia zetu halisi. Naye Abrams (1981) anasema kwamba Uhakiki ni somo linalohusika na kueleza, kuainisha, kutathimini na kupima kazi za fasihi. [tafsiri yetu] Kwa hivyo uhakiki ni somo; na ni somo linalolenga kueleza na kuchungua kwa makini kazi ya fasihi. Linalodhihirika tunapochunguza maelezo ya wataalamu hawa kuhusu swala la uhakiki ni kwamba pana kauli kuu wanazozitoa. Wanaelekea kukubaliana kwamba uhakiki ni: * Kuthamini na kueleza * Kuainisha na * Kutoa maoni

29

Kwa kuzingatia maoni haya yao tutajaribu kutoa fasili moja ya uhakiki tutakayoizingatia katika kazi yetu. Uhakiki kwa maoni yetu utakuwa ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Tumeingiza hoja ya kaida hapa kwa sababu twafahamu kuwa uhakiki hautokei katika ombwe tupu bali huongozwa na kaida na masharti maalum yaliyopo. Fasili hii yaweza kutumiwa kulenga kitendo cha hadhira inayohakiki shairi lilokaririwa na mwenzoa bila kuandikwa au kitendo cha kiakademia kinachofundishwa shuleni au chuoni. Hapa tutatoa mifano zaidi inayoelemea kuhakiki katika kiwango cha kiakedemia ambapo pana somo halisi la uhakiki. Hata hivyo pana kiwango chengine cha uhakiki ambacho twaweza kukiita cha kimsingi ambacho huzingatiwa na wasomaji wengi wa jumla. Uhakiki ni jambo la kawaida katika maisha ya mwanadamu. Hata tusomapo magazeti kwa mfano, huwa panatendeka kiwango fulani cha uhakiki. Ndiposa Hough (1966:7) akasema kwamba Yoyote anayelinganisha kile akipatacho katika kitabu na maudhui ya tajiriba yake maishani, yeyote anayelinganisha kitabu kimoja na chengine, kuwa amaeanza kuwa mhakiki [tafsiri yetu]. Bila shaka kitendo asilia anachokifanya ni kuisoma ile kazi ya fasihi. Hicho ni kitendo cha kawaida kabisa kwa mtu aliye na uwezo wa kusoma. Ni katika kitendo cha kutua na kujaribu kuielewa na kujibu maswali kama vile kwa nini, nani, na vipi ambapo uhakiki huanza. Kwa hivyo uhakiki ni shughuli iliyozingatiwa kwa makini sana hasa kiakedemia. Tumeamua kuzingatia kiwango hiki cha uhakiki kwa sababu katika uhakiki kama somo kinyume na uhakiki wa kujumla, pana kaida maalum zinazomwongoza mhakiki afanyapo kazi yake. 2.2 NI VIGEZO VIPI HUZINGATIWA KATIKA UHAKIKI? Kazi ya uhakiki haifanyiki kisadfa bali huwa imepangwa kutokea. Ifahamike kwamba kile anachokisema mhakiki kuhusu kazi yoyote ya fasihi hutegemea kwa kiwango kikubwa mtizamo wa kihakiki anaoufuata. Hivi ni kumaanisha kwamba uhakiki

30

huanza kwa maoni ya msomaji (mhakiki) kuhusu kazi anayoizingatia na hivyo basi huenda akatoa uhakiki wa kimvuto au kimguso. Kwa jumla, uhakiki unapaswa uzingatie tathimini halisi huku mbinu zilizotumiwa katika kazi ya fasihi pamoja na maudhui yake zikijadiliwa. Uhakiki bora hivyo basi hujishughulisha na uteuzi wa maudhui muhimu ya kazi husika na kisha kuona jinsi kazi yenyewe inavyoyatoa na kuyaendeleza maudhui hayo. Ni muhimu kushikilia kwamba tajiriba halisi au matukio yanayozingatiwa katika kazi ya fasihi ni kielelezo cha tajiriba za kijumla za binadamu. Kwa hivyo inatokea kwamba mhakiki anahitajika kuipitia kazi anayoizingatia ili kuona ni aina gani ya tajiriba za kawaida, hisia au shida zinazozingatiwa pale. Halafu baada ya hapo, ili kuzungumzia matini yenyewe, lazima kuonyesha jinsi mambo aliyoyateua mtunzi - kwa mfano, maelezo au fafanuzi alizozitoa au maneno aliyoyatumia-husaidia kufafanua, kuendeleza au kutoa mwelemeo mpya kuhusu yanayochukuliwa kama mambo muhimu. Tahakiki hupata uzito zaidi iwapo mbinu alizotumia mtunzi katika kukabiliana na maswala yake hudhihirishwa. Hapo ndipo tahakiki hutofautiana na muhtasari wa kazi nzima. Ikumbukwe kwamba kati ya majukumu yatekelezwayo na uhakiki, lile muhimu zaidi ni kuifasiri kazi ya fasihi. Kabla kazi yoyote ya fasihi kuhakikiwa au hata kuhusishwa na vitendo vingine vya kibinadamu, ni lazima kazi hiyo ieleweke ipasavyo. Tafsiri na maelezo ni dhana zinazojenga kitendo cha kuhakiki. Dhana ya kuifasiri kazi ya fasihi yaweza kuelezwa kwa njia mbili; kwanza, ni kudhihirisha kusudio la mtunzi kwa kuondoa vikwazo vyovyote ambavyo vyaweza kutatiza uelewaji: yaani kueleza msamiati, misemo na mpangilio wa maneno, ili kuwezesha kuweka wazi maana iliyokusudiwa. Pili, ni kwenda zaidi ya hatua hiyo ya kwanza na kuiona kazi ile kama fumbo ambalo halieleweki hata baada ya kutoa maana ya maneno na misemo. Hivyo basi mhakiki analo jikumu la kupambanua fumbo au mafumbo katika kazi hiyo. Mafumbo hayo wakati mwingine hutokea bila mtunzi kukusudia vile. Kwa muhtasari basi twaweza kusema kwamba vigezo vya kuhakiki vyaweza kuainishwa kulingana na wajibu unaohitajika kutelekelezwa na kazi ile. Hata hivyo vigezo vifuatavyo ni baadhi ya vigezo ambavyo vimezingatiwa na wahakiki wengi;

31

* Kuhalalisha kazi za fasihi au kuifafanua ili kueleweka kwa hadhira husika. * Kufasiri kazi za fasihi kwa wasomaji ambao huenda wasiielewe ipasavyo. * Kuratibu kazi za fasihi kwa kutumia vigezo sanifu vya tathimini. * Kugundua na kutumia kanuni zinazoeleza nguzo za sanaa bora. Hata hivyo ni wazi kwamba kazi yoyote ya uhakiki huwa imejengeka katika misingi ya kujaribu kuunda kundi la istilahi, kanuni na vigezo vya kutumiwa katika kufasiri kazi za fasihi, pamoja na kutoa viwango na maadili ambayo kwayo kazi hizi na watunzi wake huratibiwa. 2.3 JE, KUNA NJIA HALISI YA KUHAKIKI? Kiini cha swali hili ni je, pana nadharia ya fasihi inayoweza kuchukuliwa kama iliyo mwafaka zaidi ya zote? Ukweli ni kwamba hakuna! Hii ndiyo sababu inayofanya somo la uhakiki kuwa gumu hali kadhalika la kusisimua. Kazi ya fasihi imekuwa chanzo cha maoni na mijadala isiyoisha huku wahakiki wakijaribu kutoa njia zenye uzito zaidi za uhakiki lakini hakuna ile iliyo kamili. Kwa maoni ya Hough(1966:7) Hakuna kazi ya uhakiki iliyo kamili. Uhakiki haufanyiki mara moja na kukamilika kwani huwa inategemea mkondo wa kihistoria na hali ya maendeleo ya kijamii. Kila patokeapo mabadiliko kihistoria, fasihi ya awali huhitaji kuelezwa upya [tafsiri yetu]." Kwa hivyo kazi ya uhakiki ni fululizi hivi kwamba haina kikomo na hakuna uhakiki unaojisimamia kivyake. Kila siku kazi mpya za fasihi huingizwa katika jamii ili kuchukuana na maisha ya jamii ya wakati wake. Na kazi hiyo huhitaji kutathiminiwa kwa misingi inayochukuana na hali hiyo. Tunachokisema ni kwamba hata ingawa kimsingi kazi ya uhakiki huweza kuchukuliwa kama kazi nafsia (kwamba kila mahakiki huona kazi ile kivyake), mtizamo wa kila mhakiki huathiriwa na mazingara ya kijamii pamoja na utamaduni ambamo kazi ile inatokea. Kama wanavyosema Peck na Coyle (1984:150)

32

Hadi kufikia karne ya kumi na nane, mtizamo mkuu wa fasihi ulikuwa ni kuichukulia kama "funzo la kuvutia", na hivyo basi uhakiki ulihusishwa na jinsi kazi hiyo ilivyofanikiwa kutoa funzo kwa msomaji. Katika kipindi cha ulimbwende, hali hii ilibadilika. Walibwende walisisitiza umuhimu wa ubinafsi, na hivyo basi uhakiki wa kilimbwende uliegemea upande wa thamani ya alichokisema mtunzi kama mtu binafsi [tafsiri yetu]." Kwa hivyo kila uhakiki huchukuana na kipindi cha kihistoria cha wakati wake, na hivyo tahakiki hubadilika kadri jamii husika inavyobadilika. Pana hata wengi wanaopinga kabisa kitendo cha kuhakiki huku wakidai kwamba uhakiki ni kitendo cha kuishushia fasihi hadhi yake halisia. Okot P'Bitek (1973:22) ni mmoja anayeona hapana haja ya kuwa na uhakiki na hata kuendelea kudai kwamba hapana haja ya kuzingatia fasihi kama somo. Anasema; Fasihi kamwe haiwezi kuwa somo la kutahiniwa kwa sababu hisia ndizo hujenga maelezo na sio elimu katika maelezo hayo. Waombolezaji katika mazishi hawalii ili kupata cheti. Swali sio "unajua nini kuhusu muundo wa wimbo?" bali ni " "umeufurahikia kwa kiasi gani? Umekugusa Kivipi?" [tafsiri yetu] Linalodhihirika katika kauli hii ya P'Bitek ni kwamba fasihi hulenga hisi za hadhira. Jambo ambalo halizingatii ni ukweli kwamba sio kila mwanajamii anaweza kuwa mtunzi bora wa kazi ya fasihi lakini wanaofaidika kwa kazi hiyo ni wengi. Vile vile fasihi hulenga mambo mengi zaidi ya hisia; yaani ina majukumu mengi kwa jamii yake. Pia sio kila kazi inayotokea katika jamii huweza kuratibiwa kama fasihi au sanaa. Kwa nini pasiwe na kanuni za kuzingatiwa ili kuhakikisha mambo hayo na mengine mengi yamelainishwa? Bila kutukuza wala kupinga kauli ya P'Bitek ningependa kutaja kwamba fasihi yaweza kushughulikiwa kwa kuzingatia njia mbali mbali na uhakiki ni mojawapo wa njia hizo. Vile vile kuhisi na kuathiriwa na kazi ya fasihi ni njia nyengine ya kuizingatia

33

fasihi; hivyo basi yategemea jukumu la anayehusika. Ama kwa hakika, katika kila kitendo kinachohusu fasihi uhakiki hufanyika, iwe ni kumkumbusha msanii majina ya wahusika, iwe ni kumhimiza anapotoa hadithi na kadhalika; yaani hapana utunzi bila kuhakiki hata wa kibinafsi. Kutambua kwamba waombolezaji wanalia kwa sababu ya kuguswa na kinachoendelea pale katika maombolezo ni kitendo cha kuhakiki kwani kinahusisha tokeo na sababu. Naye McGilhrist, I(1982:21) anasema; Uhakiki unazingatia zaidi maoni ya wengine kuliko fasihi yenyewe. Tunawaona watunzi wetu kupitia nadharia za fasihi ambazo hutukuza maoni yetu kuliko kile tunachodhamiria kugundua. [tafsiri yetu] Maoni ya mtaalamu huyu ni kwamba uhakiki kwa msingi wake huwa na kaida na masharti ya kuuongoza, na kile anachofanya mhakiki ni kutizama kama kazi anayoizingatia inatimiza kaida hizo. Yaani, kwanza mhakiki haioni wala kuichunguza kazi ile kwa misingi yake [japo ni vigumu kutenga ubinafsia wa mhakiki na kazi anayofanya] bali hujaribu kuzingatia kaida maalum. Ndiposa McGilhrist(1982:38) anaendelea kusema "lazima uhakiki uheshimu ubinafsi wa kazi ya sanaa pamoja na `maana' ya mtunzi[tafsiri yetu]." Na kama ambavyo pana maana ya mtunzi huenda pia pakawa na maana ya mhakiki ambayo anaiona katika kazi ya fasihi anayoipitia. Ukweli ni kwamba huenda mhakiki, kwa kuongozwa na kaida za uhakiki wake, akazua mambo ambayo hakuyataja mtunzi asilia wa kazi ile. Yaani wakati mwingine mhakiki huzua mambo fulani ambayo mtunzi asilia hakuyafahamu au kuyatilia maanani katika kazi yake. Kauli hii yatuongoza katika hoja kwamba maoni yote ya binadamu hujikita katika tajiriba mbalimbali ambazo huzua fasihi mbalimbali na hivyo basi kutoa hitimisho tofauti. Hapana njia yoyote maalum ya kuhakiki au kuelewa kazi ya fasihi kwani yote huadhiriwa na mambo mbali mbali ambayo tumejaribu kudhihirisha katika kazi hii. Hali hii yapendekeza tujiulize ukweli ni upi kama upo?

34

2.4

NADHARIA ZA UHAKIKI Kile anachokisema mhakiki kuhusu kazi yoyote ya fasihi hutegemea, kwa

kiwango kikubwa, mtizamo wa kihakiki anaouzingatia pamoja na nadharia anayoifuata. Katika kila jamii pana misingi ambayo huwaongoza wahakiki hivi kwamba wanafanya kazi yao huku wakifahamu kuwa wao sio wa kwanza wala wa mwisho kushirikisha kitendo hicho. Kama asemavyo Elliot (1975:476) Hakuna mshairi wala msanii aliye na maana ya kivyake. Umuhimu wake na tathimini yake ni zao la uhusiano wake na washairi na watunzi waliomtangulia. Hawezi kusimama kivyake, ni lazima kumfananisha na kumtofautisha na waliotangulia. [tafsiri yetu] Kwa hivyo twaweza kuona kwamba Elliot anapendekeza wazo kwamba pana kanuni ambazo tayari ziliwekwa ambazo hutumiwa au zapasa kutiliwa maanani katika uhakiki wa kazi mpya za fasihi. Ndiposa pengine twapata mashairi ya kimapinduzi katika kiswahili yanahakikiwa kwa kulinganishwa na ya kale (ya kimapokeo). Vile vile twaweza kuchukuwa dhana ya Elliot kwa mwanga mwingine kama tutakubali kwamba mahusiano anayopata mhakiki katika maisha yake kwa jumla ni adhari kuu katika mtizamo wake wa fasihi na wa maisha kwa jumla. Hivyo basi kila maoni huwa yanadhiriwa na kuadhiri yaliyokuwako, yaliyopo, na yajayo. Hivyo basi wakati mwingine twapata kwamba nadharia mpya za fasihi huzuka baada ya zile zilizopo kushindwa kukabiliana na matakwa ya kifasihi au kwa kuzingatia mitizamo mipya kuhusu maisha na wanajamii. Kwa mfano upungufu wa nadharia ya umuundo wa kuona fasihi kama kiungo chenye mpangilio halisi usiotatanika na usiotegemea mambo mengine ya nje, ndio uliosababisha kuzuka kwa nadharia ya Umuundo-mpya (post-structuralism). Pia, uhakiki kama somo la kiakedekia, ni tofauti na uhakiki wa kijumla kwa ambavyo badala ya mhakiki kufurahia kazi anayoizingatia, huwa anaanza kazi yake kama tayari anafahamu anachotafuta kitabuni mle katika misingi ya nadharia anayozingatia.

35

Kwa jumla, nadharia za uhakiki hugawika katika makundi matatu makuu; kuna kundi linalosisitiza kinachosemwa (maudhui) kundi lingine husisitiza kinavyosemwa (mtindo/fani) na kundi lile linatosisitiza ni nani anayesema nini na kama nani (mtunzi na hadhira). Kwa muhtasari ni kwamba nadharia inayosisitiza mtunzi na hadhira huwa inazingatia nafsi ya mtunzi na msomaji (hadhira) wake, kiwango chao cha ujuzi, historia ya maisha ya mtunzi katika jamii, nafasi anayoitamalaki katika jamii n.k. Katika nadharia kama hii, msomaji hachukuliwi kama mtu binafsi bali huchukuliwa kama kiumbe chenye jukumu lililojikita katika misingi ya kihistoria na kitamaduni; kwani jinsi ambavyo kazi za fasihi husomwa na kueleweka hutegemea hali ya kitamaduni na kihistoria ya hadhira yake. Isitoshe, tajiriba za kitamaduni na za kifasihi walizonazo hadhira, huathiri jinsi vitabu vya fasihi huandikwa -- havitokani na ombwe tupu bali hutokea ili kurekebisha au kuchukuana na utamaduni wa wasomaji. Mara nyingi imesemekana kwamba sio tu mtunzi wa kazi ya fasihi anayeamua maana ya kazi hiyo bali hata msomaji hutekeleza jukumu la kati kabisa katika kujenga maana hiyo. Yaani mtunzi huwa anafikiria hadhira yake kama mwongozo wa maana ya kazi aitungayo. Nadharia inayosisitiza mtindo au muundo wa kazi ya fasihi hukataa wazo kwamba kazi ya fasihi yaweza kuelezwa kwa kuhusishwa na mtunzi au hadhira yake au hata na mambo yaliyo nje ya kazi hiyo. Nadharia hii husisitiza kwamba lugha ndicho kitovu cha kazi ya fasihi na maudhui hutokea tu kwa sababu pana lugha. Kwa hivyo shughuli ya nadharia hii ni kuona jinsi lugha ilivyotumiwa na kupangwa. Nadharia inayosisitiza maudhui au kinachosemwa hushikilia kwamba kazi ya fasihi huwa fasihi kwa sababu ya maudhui yake. Nadharia hii hupiga hatua zaidi na kupendekeza aina ya maudhui yanayopaswa kuzingatiwa na fasihi. Huamini kwamba fasihi ni kioo cha jamii kinachopaswa kuchora picha halisi ya maisha ya jamii husika. Mifano ya aina hizi mbali mbali za nadharia itajitokeza katika sehemu inayofuata ya mifano ya nadharia za fasihi. Hatulengi kuzingatia kila nadharia ya fasihi bali tutatoa mifano ya baadhi ya nadharia za fasihi zilizopo pamoja na maelezo ya kimuhtasari ya nadharia hizo kama tunavyozielewa. Nyingi za nadharia tulizochagua kuzingatia zinaegemea kwa kiwango fulani sosholojia ya fasihi. Dhana ya sosholojia ya fasihi hutumiwa kueleza kazi za kihakiki na

36

kihistoria ambazo lengo lake la kimsingi ni jinsi mtunzi anavyoathiriwa na tabaka lake, itikadi yake ya kijamii, hali ya kiuchumi ya kazi yake, na aina ya hadhira anayoilenga. Wahakiki wa aina hii huiona kazi ya fasihi kama inayofungwa (katika maudhui yake, tathimini za maisha inayoyazingatia na hata mtindo wake) na hali ya kijamii na nguvu za wakati wake. Mfano wa mhakiki aliyezingatia dhana hii ni Hippolyte Taine(1863) katika History of English Literature. Hata hivyo mfano mwafaka zaidi wa tahakiki zinazozingatia dhana ya sosholojia ya fasihi ni nadharia za Ki-marx. 2.4.1 NADHARIA ZA KI-MARX Anachokisema mhakiki kuhusu kazi anayoizingatia, hutegemea kwa kiwango kikubwa, dhana anazozileta katika kazi hiyo. Aghalabu, dhana hizi haziwi za moja kwa moja, lakini mhakiki anayeegemea uhakiki wa Ki-marx huwa anafahamu kwa hakika anachokizingatia kwani kazi yake itaongozwa na falsafa fulani zilizopo. Kazi yake itaongozwa na mtizamo wa Ki-marx kuhusu historia, ambapo mikinzano ya kitabaka huwa jambo muhimu na vile vile uhusiano kati ya fasihi na muundo wa Kiuchumi katika jamii husika lazima udhihirishwe. Kwa jumla, twaweza kusema kwamba mhakiki wa Ki-marx hukita nadharia yake kwenye itikadi za Karl Marx na Fredrick Engels, na hasa kwenye madai ya hao wawili kuwa, katika tathimini ya mwisho kabisa maendeleo ya historia ya binadamu pamoja na taasisi zake, yatakuwa ni tokeo la mabadiliko katika njia za kimsingi za uzalishaji mali. Kwamba mabadiliko kama hayo husababisha mageuko katika muundo wa matabaka ya kijamii ambayo katika kila kipindi huendeleza kung'anga'aniwa kwa uwezo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii; na kwamba dini, fikra na utamaduni wa jumuiya yoyote (zikiwemo sanaa na fasihi kwa kiwango fulani) huwa ni `itikadi' na miundo maalum ya `kitabaka' ambayo ni zao la miundo na matabaka ya kijamii yaliyomo wakati huo. Umarx huchukua kwamba jamii zote za kitabaka huzalisha mkururo wa miundo ya urazini inayokinzana na kushindana. Katika jamii ya kikapitolisti, kwa mfano, aina tofauti za mitizamo kuhusu maisha huwakilisha haja tofauti za kitabaka ambazo hutegemea hasa mikinzano kati ya mapato na nguvu za kutenda kazi. Kwa hivyo Umarx huhusisha itikadi na uzalishaji mali na jukumu lake katika mivutano ya kisiasa katika jamii. Jinsi watu binafsi wanavyoelewa msingi wa maisha yao hutokea kuwa kamba ya

37

mvutano ambapo wanaweza ama kubadilika au kuendelezwa. Kwa mfano, chini ya mfumo wa kikapitolisti, wafanyakazi wanashurutishwa kuuza uwezo wao wa kufanya kazi kwa wale wanaotawala mazao pamoja na huduma. Katika mpangilio huu, wanaotawala nguzo za uzalishaji mali hunufaika kupitia kwa dhamani ya ziada iliyozalishwa na wafanyakazi. Hii ni kati ya mali inayobakia baada ya kuondoa matumizi ya malighafi, mashine, na nguvukazi. Aidha faida hupatikana kwa kuwalipa wafanyakazi malipo ya chini kuliko dhamani ya kazi waliyofanya. Uhakiki wa ki-marx hujishughulisha na tabaka la kiuchumi na sababu za kiitikadi zinazotawala jinsi mtunzi hufikiria na kuandika, lakini hasa huzingatia uhusiano wa kazi ya fasihi na uhalisi wa kijami uliopo wakati huo. Kama tokeo basi uhakiki wa Ki-marx hudai kwamba watunzi wanapaswa kumithilisha hali halisi ya maisha ya jamii wanazotungia. Wazo hili lilipingwa hata na wafuasi wa Marx. Mmoja kati yao ni mtaalam kutoka Hungary, George Lukac aliyekuwa na maoni kuwa badala ya fasihi kuimithilisha hali ya maisha, fasihi na sanaa zapaswa kuwa `picha ya uhalisi'. Ambapo picha hiyo inakiuka misingi ya kuiga moja kwa moja uhalisi. Mhakiki wa Ki-marx, hivyo basi, tayari ametolewa picha halisi ya maisha. Shida aliyo nayo ni jinsi ya kuikabili na kuihakiki fasihi. Wahakiki wa ki-marx aghalabu wameiona fasihi kama iliyo halisi, hivi kwamba mtunzi wake huwa anajitenga na kuonyesha makosa katika jamii. Mbinu inayotumiwa na wahakiki wa jadi wa ki-marx ni kuunda tena mtizamo kuhusu yaliyopita kutokana na ithibati za kihistoria kisha wakadhihirisha uhalisi wa kazi fulani kama kielelezo cha jamii na kama njia ya kuelewa uhalisi wa kijamii. Kwa jumla uhakiki wa ki-marx huhusisha kazi ya fasihi na mtazamo wa uhalisia wa kijamii wa wakati kazi hiyo ilitungwa. Vile vile uhakiki huu zaidi huzingatia maudhui katika fasihi huku pakitolewa uhakiki wa maadili, na njia za kuyaboresha maisha zilizoshughulikiwa. Ni muhimu kutaja kwamba pana aina mbali mbali za nadharia za uhakiki za ki-marx. Lakini licha ya wingi wa nadharia hizi, nadharia zote za ki-marx zina nguzo moja iliyo sawa; kwamba fasihi hueleweka tu katika msingi wa uhalisi wa kijamii hasa katika umilikaji mali. Wahakiki wa ki-marx hushikilia kwamba nadharia yoyote inayozingatia fasihi kwa kuitenga (kwa mfano kama kazi ya kimuundo au kama zao la mkondo wa fikra za kibinafsi za mtunzi) na kuiweka katika hali hiyo huku

38

ikitenganishwa na jamii na historia, huwa ni pungufu katika uwezo wake wa kueleza hasa fasihi ni nini. Kwa wahakiki wa ki-marx uhalisi wa kijamii si chombo ovyo ambamo fasihi hujengeka na kutokea bali huchukuliwa kama ulio na umbo maalum, na umbo hili hupatikana katika historia ambayo kwa maoni yao ni mkururo wa mivutano kati ya matabaka yanayokinzana na njia za kiuchumi za kuzalisha mali ambazo zinazingatiwa katika jamii husika. Umbo hilo hupatikana pia katika hali yoyote ile ya jamii kwani mahusiano maalum ya kitabaka na hali halisi za kisiasa, kitamaduni na kijamii huchukuana na mfumo uliopo wa kuichumi kwa njia husishi. Upungufu wa nadharia hizi hutokea katika kuchagua kiwango cha maisha kitakachozingatiwa kwani ni vigumu kwa kazi ya fasihi kuzingatia maisha ya jamii katika ujumla wake. Kwa mfano iwapo mtunzi atachagua kuonyesha starehe na buraha ya maisha ya tabaka tawala bila kuonyesha uchochole wa tabaka linalotawaliwa, atakuwa anakiuka misingi ya kutoa picha halisi ya maisha ya jamii? Ufinyu wa mtizamo wa kimarx ni muweka jamii katika vikundi viwili kuu ambavyo yamkinika ni sawa. Yaani yaelekea kuwa wanatabaka la juu wote wamefanana kwa njia zote, na vivyo hivyo kwa wanatabaka la chini. Hapa ndipo ahakiki wa kifeministi wanaposema kwamba umarx unaepuka kuona kwamba hata katika maisha ya tabaka la juu wanawake hawakuwa na uhuru/nafasi sawa na wanaume. Hata hivyo tutaje kwamba msisitizo wa nadharia za ki-marx kuhusu umuhimu wa mikinzano na migongano ya kitabaka umeathiri wahakiki wengi wa kijamii ambao hawazingatii itikadi za ki-marx. 2.4.2 NADHARIA YA UASILIA Nguzo ya nadharia ya uasilia ni maisha kama yalivyokuwa - yaani maisha asilia. Kwa hivyo lengo la kimsingi la uhakiki huu ni kutoa picha ya maisha kama yalivyokuwa (kwa ukweli wake wote) ili kueleza misingi ya maisha yalivyo sasa. Wakati mwingine imesemekana kwamba uasilia hutoa picha halisi zaidi ya uhalisia. Nadharia ya uasilia huchagua maudhui maalum ya kuzingatia. Fauka ya hayo, nadharia hii ni aina ya ubunifu wa kifasihi ulioendelezwa na kundi la waandishi waliokuwa na tasnifu maalum ya kifalsafa. Tasnifu hii, iliyokuwa zao la maoni yaliyotokana na mtaalamu wa biolojia

39

Charles Darwin katikati ya karne ya kumi na tisa, ilishikilia kwamba binadamu alikuwa chini ya himaya ya maisha ya asilia na kamwe hakuwa na roho (soul) au uhusiano wowote wa kidini uliokiuka kaida za ulimwengu halisi. Hivyo basi binadamu alichukuliwa kama mnyama wa tabaka la juu ambaye tabia na maisha yake hutegemea uzawa wake na mazingira yake. Ni kwamba binadamu hurithi tabia zake za kibinafsi pamoja na haja zake za kiasilia na huwa anafuata, bila hiari, nguvu za kijamii na kiuchumi katika familia, tabaka na kundi alimozaliwa. Waandishi wanaufuata nadharia hii aghalabu huzingatia maswala asilia ya kisayansi katika maisha huku wakiwasawiri wahusika wao kama walio na nguvu na mivuto ya kinyama kama vile ulafi na hamu kubwa za kufanya mapenzi. Hatima au mwisho wa riwaya ya kiasilia aghalabu huwa ni tanzia. Watunzi waliotunga kazi zao kwa kuzingatia nadharia hii wameshikilia ama mkondo wa kimaumbile, ambapo wamesisitiza hali ya kinyama aliyo nayo binadamu au mkondo wa uchumi wa kijamii ambapo binadamu anasawiriwa kama aliyeshiriki katika kujaribu kuishi katika ulimwengu asioulewa vilivyo. Kwa hivyo mara nyingi binadamu anaongozwa ni majaaliwa kwani hivyo ndivyo alivyopaswa kuwa. Hivyo basi mhakiki anayezingatia nadharia hii hana budi kuona kama kweli visa vilivyo katika kazi anayoipitia vinaonyesha binadamu katika hali halisi ya kimaumbile na uasilia. Uasilia basi huwa ni kueleza chanzo cha maisha, hulka, mitazamo, na mipangilio ya maisha ya binadamu kama tuionavyo leo. Kwa mfano masomo mbali mbali yametumia mtizamo huu zikiwemo falsafa zilizoongoza ufemisnisti ambapo wengi walijaribu kuchunguza asili ya tofauti za kijamii kati ya mme na mke na kwa nini mme akatukuzwa huku mke akidunishwa. Huu ni mtizamo unaochukulia maisha ya binadamu kama fululizi yakiwa yanaanza na kiwango cha chini (cha kinyama) hadi cha juu (cha ustaarabu). Nyingi za hadithi na visa asili vya tamaduni zetu vyaweza kuchunguzwa kwa kuelemea mtizamo huu. 2.4.3 NADHARIA YA UMUUNDO Katika miaka ya kwanza ya karne hii, mwanaisimu kwa jina Ferdinard De saussure alipendekeza mtizamo mpya kuhusu lugha. kinyume na wataalamu wengine walioshughulikia historia na sura maalum za lugha fulani, Saussure alivutiwa na miundo

40

inayohimili lugha zote, huku akijaribu kuonyesha kwamba lugha zote za ulimwengu zaweza kutathiminiwa kwa kaida maalum za umuundo. Alizua istilahi `parole' na `langue' kueleza maoni yake: `Parole' au uzungumzi ni lugha katika matumizi na hiki ndicho walichokizingatia wanaisimu wa awali, lakini Saussure alivutiwa na mfumo wa kinadharia unaounda lugha zote au `Langue' - yaani masharti au kaida zinazoiwezesha lugha kuwepo na kuweza kufanya kazi. Kazi hii ya Saussure ndiyo iliyozaa mkondo unaojulikana hivi sasa kama umuundo. Muundo waweza kuelezwa kama mtizamo wa kitathimini ambao huzingatia zaidi miundo inayojenga kazi binafsi. Hata hivyo, kazi ya Saussure ilikuwa imetengewa wanaisimu peke yao. Katika miaka ya 1950, mtizamo huo wa Saussure ulianza kusambaa katika masomo mengine hasa wakati mawazo yake yalipozingatiwa na Mwanaanthropolojia Claude Levi-strauss. Kwa kuchukua maoni ya isimu ya Saussure na kuyaingiza katika sayansi ya kijamii . Hasa alichotaka kuendeleza ni dhana ni kwamba pana viwango viwili katika kuelewa maisha ya jamii, isimu, lugha na chochote kingine kile. Viwango hivi ni cha juu juu (surface) na cha ndani (deep). Kwa hivyo twaweza kuangalia jamii katika muundo wake wa kijuu juu na kuielewa lakini tukitaka kupata maana mwafaka lazima tuchunguze muundo wake wa ndani ambao hupatikana katika kila jamii ya wanadamu. Dhana hii ya uwili ilijitokeza katika nadharia nyingine za kijamii kama vile katika kazi ya Sigmund Freud ambaye aligawa mambo katika kiwango cha juu juu (manifest) ambacho chonekana na kila mmoja na kiwango cha ndani (latent) ambacho hupatikana kwa uchunguzi zaidi na ambacho ndicho hasa hueleza maana halisi; vile vile kazi ya Marx ilidhihiri uwili huu alipoeleza dhana ya juu juu ya ukengeushi (false consciousness) na hali halisi ya mambo ya unyonyaji (exploitation). Kwa ujumla twaona usomi wa kuitizama jamii kwa uwili unaokinzana (binary opposition) ambao ulisambaa katika nyanja nyingi za usomi. Awali ya hapo, anthropolijia ilizingatia makundi au makabila maalum ya watu ambayo yalizingatiwa kivyao, mifuma ambayo ilidhaniwa kwamba haibadiliki, lakini Levi-strauss alijishughulisha na mifumo inayohimili jamii zote. Strauss alidai kwamba pana muundo maalum ambao waweza kutumia kueleza jamii zote za ulimwengu, kama vile ilivyo na somo la hisabu au la uchumi ambapo pana njia (formula) ambayo yaweza kueleza maswala mengi katika somo hilio. Hapo ndipo dhana za umuundo zilipoingia

41

katika masomo mbali mbali hasa yale ya sayansi ya jamii na fasihi. Saussure alitoa maelezo ya nadharia changamano kuhusu lugha, na ni misingi ya nadharia zake inayotoa nguzo ya mbinu za umuundo. Ingawa huwa tunatumia lugha kuzungumza kuhusu maisha, Saussure hakulizingatia jambo hilo bali alisisitiza kwamba lugha ni kiungo kamili kinachojisimamia. Kwamba ni kiungo kilicho na masharti na sheria zake. Hivyo basi kuwepo kwa vitu duniani hakuathiri aina ya lugha iliyopo. Isitoshe, alidhamiria kudai kwamba lugha kwa kujisimamia haibadiliki wala vipande vyake haviadhiriwi na mabadiliko yoyote ya kijamii. Katika mkabala huo, neno ni ishara huru inayoelezwa kwa kutofautishwa na nyengine. Lugha ni mfumo wa uhusiano kati ya viungo kadhaaa vinavyoijenga; ni muundo, sio kitu. Dhana hii yaweza kueleweka zaidi tukizingatia maneno ya Saussure ya `kionyeshi' na `kinachoonyesha'. Neno katika lugha ndilo `kionyeshi' na dhana inayorejelewa ni neno hilo ndiyo `kinachoonyeshwa'. Vyote viwili haviwezi kutenganishwa, lakini umuundo hujishughulisha zaidi na uhusiano wa vionyeshi na jinsi vinavyofanya kazi kuliko kuangalia nje ya mfumo wa lugha, yaani kinachonyeshwa. Kwa msingi kabisa, Saussure alizingatia zaidi mpangilio wa ndani wa lugha, ule muundo wake na sio mahusiano ya vipande vyake. Wahakiki wanoegemea mkondo wa Saussure huzingatia kwamba matini husika ni mfumo unaojisimamia na hivyo basi huwa hamna haja ya kutumia mambo ya nje ili kuhakiki kazi ya fasihi. wahakiki huzingatia matini kama kiungo kamili kinachoweza kuhakikwa kivyake. Hivyo basi mhakiki wa umuundo hujaribu kuweka sarufi ya matini pamoja na sheria za jinsi matini hiyo hufanya kazi. Mhakiki anayezingatia zaidi muundo wa lugha ya matini bila shaka hupuuza dhana ya jadi kuhusu kile matini hiyo huweza kutueleza kuhusu maisha; na hivyo basi hufanya mtindo wa kazi yenyewe kiini cha uhakiki wake. kwa hivyo wahakiki wanaotumia nadharia ya umuundo hujaribu kuzingatia matini peke yake huku wakiepuka kuifasiri kazi ile kulingana na kaida zilizowekwa kuhusu jinsi matini hufanya kazi. Hata hivyo, huenda njia hii isiwe ya kufaa sana kwa sababu huwa inachukulia kwamba kila kitu kimeundwa katika mpangilio halisi usiotatanika na usiotegemea mambo mengine yaliyo nje yake. Ama kwa hakika, hata lugha yenyewe haiwezi kabisa kufanya kazi bila kuathiriwa na mambo mengine kama vile mazingira yake. kama

42

tulivyotaja katika utangulizi wa sehemu hii hapana nadharia inayojitosheleza na isiyo na upungufu fulani. Upungufu wa nadharia hii ndiyo uliochochea kuzuka kwa Umuundompya. 2.4.4 NADHARIA YA UMUUNDO-MPYA Tunatumia neno Umuundo-mpya kuonyesha mtizamo wa kimuundo katika fasihi ambao ulitokea baada ya Umuundo. Japo dhana hii haiwezi kupewa maana moja maalum, imehusishwa na maendeleo kutoka au katika kazi za Derrida (1973, 1976), Lacan (1977), Kristeva (1981, 1984, 1986), Althusser (1971) na Foucault (1978, 1979a na b, 1981, 1986). Kazi hizi nazo zilichangiwa na kazi za Ferdinand de Saussure na Emile Benveniste (kuhusu isimu-jamii ya umuundo), kazi ya umarx hasa kupitia nadharia ya itikadi iliyoendelezwa na Louis Althusser, na kazi ya tathimini-nafsi ya Sigmund Freud na Jacques Lacan. Kazi hizi zimetoa athari mbali mbali kwa nadharia tofauti lakini zote zinazingatia makisio sawa kuhusu lugha, maana, na ubinafsia (subjectivity). Lugha yachukuliwa kama nguzo maalum ya uainishi wa mpangilio wa jamii, maana za kijamii, nguvu na urazini wa kibinafsi. Hii ni kwa sababu ni katika lugha ambapo maana za mpangilio wa jamii na matokeo yake ya kisiasa na kijamii hujengwa na kupingwa. ni kupitia lugha ambapo hisia na maana yetu ya kibinafsi (ambayo inatufasili) hujengwa. Aidha, lugha haielezi ubinafsi wa kipekee wa mtu bali hujenga ubinafsia wa mtu kwa njia zilizojengeka katika miundo ya jamii yake. Katika Umuundo-mpya, ubinafsia sio hali yenye umoja au isiyobadilika, bali hubadilika kila mara ili kuchukuana na hali halisi ya kihistoria na kisiasa ili kudumisha nafasi ya mhusika katika jamii. Umuundo-mpya, kama nadharia nyinginezo ina makisio fulani kuhusu lugha, ubinafsia, ufahamu, na ukweli. Nguzo zake, ambazo zatokana, kama tulivyotaja hapo juu, na mwanaisimu wa kiimuundo Ferninard de Saussure, ni kwamba lugha, badala ya kudhihirisha uhalisi wa kijamii uliopo, huwa yatujengea uhalisi huo wa kijamii. Kwa hivyo sio uhalisi wa kijamii wala ulimwengu asilia huwa na maana zinazodhihirishwa ni lugha. Lugha mbali mbali pamoja na matumizi mbali mbali ya lugha moja huugawa ulimwengu na kuupa maana kwa njia tofauti ambazo haziwezi kupatana ili kuunda kigezo kimoja kinachodhihirisha uhalisi wa jamii. Kwa mfano, maana ya tajiri hutofautiana katika lugha mbali mbali na hata kati ya miundo tofauti ya lugha moja, na hutegemea

43

matumizi na muktadha wa matumizi hayo. Ndiposa hapana maana moja ya neno au fungu la maneno. Miundo yote ya umuundo-mpya huchukulia kwamba maana hujengwa katika lugha na huwa yule anayezungumza lugha hiyo hawezi kuhakikisha maana hiyo. Kwa hivyo tofauti na maoni ya Saussure, maana huzaliwa na kuundwa kwa njia mbali mbali. Hata hivyo nadharia hii hukubaliana na wazo lake kwamba lugha haimuliki maana; bali maana hukuzwa katika lugha na kwamba ishara hazina maana ya kivyake bali hupata maana katika mkururo wa lugha pamoja na tofauti yake na ishara nyingine. Dhana hii ni muhimu sana kwa sababu yadhihirisha lugha kama chombo cha kijamii ambacho chapingwa na kung'ang'aniwa. Kulingana na nadharia hii basi, neno 'mama' kwa mfano, huwa halina maana ya kindani inayotokana na lugha husika bali huwa na maana za kijamii zilizotokana na lugha hiyo na ambazo zinakinzana na kubadilika kulingana na mazingira na kipindi cha kihistoria. Kwa hivyo kinyume na maoni ya wanamuundo kama vile Levi-Strauss walioshikilia kwamba maana ya kisa, kwa mfano, ipo katika matini na maana hiyo hiyo hutokea katika matini nyengine yoyote, nadharia hii yaeleza kuwa maana ya kisa ni amali ya msomaji/msikizi (hadhira) na kwamba pana fasili mbali mbali za kisa hicho kulingana na muktadha. Hivyo basi kwa umuundo-mpya twaweza kueleza kuwepo kwa wingi wa maana pamoja na mabadiliko yake kwa kuona maana sio kama iliyojengwa katika ishara zisizobadilika bali kama iliyo katika viashiria (signifiers) ambapo kiashiriwa (signified) hubadilikabadilika. Hapo ndipo alipojikita Derrida ambaye aliingiza dhana ya muktadha katika kueleza maana katika lugha na matini. Umuundo-mpya ulimulika kazi ya Marx huku ukijaribu kuonyesha ufinya wa kuzingatia tu mahusiano yaliyopo kati ya wafanyakazi na walioshikilia nguvu za kuzalisha mali. Ni kwamba umarx haukudhihiri hali kwamba uhalisi wa kijamii huwa ni tofauti kwa wengi na katika miktadha mbali mbali. Isitoshe, uhalisi huo wapaswa kuzingatiwa kulingana na athari zake za kijamii ambazo hutoa maana tofauti kwa wanajamii tofauti. Umarx ulidunisha ubinafsi wa fikira, hisia, tajiriba, na mielekeo (ubinafsia) ya watu ambayo ni muhimu katika kueleza mahusiano ya kijamii. Ni katika kigezo hiki cha ubinafsia fikira na hisia za mtu binafsi, hali yake ya kipekee isiyofanana na mwengine, jinsi anavyojiona na kujielewa dhidi ya ulimwengu, huchukuliwa kama

44

nguzo kuu ya ummundo-mpya. Wahakiki wanaozingatia nadharia hii basi huongozwa na dhana ya kubadilika kwa maana katika miktadha mbali mbali na hivyo basi kuwashurutisha kuzingatia muktadha wa kazi hiyo kama nguzo ya kueleza kazi hiyo. 2.4.5 NADHARIA ZA UFEMINISTI Aghalabu, uhakiki unaozuka miaka ya karibuni husisitiza umuhimu wa kuchunguza kazi yenyewe ya fasihi. Hata hivyo, yaelekea kwamba kila msomaji huwa na fikra za kiawali ambazo huziingiza katika kazi anayoipitia. Fikra hizi, kwa kawaida, huwa ni nuru ya maadili na imani muhimu za jamii husika wakati huo. Hali hii ndiyo iliyozaa Ufeministi ambao hujaribu kukiuka mitizamo ya kiume ambayo yaelekea imetumiwa sana katika jamii. Tukiangalia mifano ya nadharia tulizozitaja hapo awali, twaona kwamba waitifaki wake wote ni wanaume; na kama nadharia yaweza kuhusishwa na maoni ya mtunzi yaliyotokana na tajiriba yake ya kijamii basi ni wazi kwamba maoni ya wanawake hayapo pale. Hii ni kwa sababu wanaume na wanawake aghalabu huathiriwa na maisha ya kijamii kwa njia tofauti kwani misingi na kaida za kijamii zimejengwa ili kudhihiri na kuendeleza tofauti hizo. Nadharia hii hudhamiria kuonyesha kwamba uana na uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke ni mambo ya kati kabisa katika fasihi. Uhakiki huu pia hupiga hatua mbele na kuonyesha uhafifu wa hali ilivyo hasa katika nadharia nyingi za uhakiki. Wahakiki wanaozingatia nadharia hii hudai kwamba tahakiki za kijadi zimekandamiza mjadala kuhusu uana jambo ambalo yaelekea ni kwa manufaa yao. Kwa hivyo azma kuu ya Ufeministi ni `kusoma upya' kazi za fasihi ili kusisitiza umuhimu wa vipengele vilivyopuuzwa na wahakiki wengi au ambavyo hawangeviona kwa sababu walikuwa wanafanya kazi katika nadharia za kijadi zinazomtukuza mwanaume. Ama kwa hakika Ufeministi ni siasa. Siasa kwa sababu mfumo huu wa uhakiki unaelekezwa katika kubadilisha uhusiano uliopo kati ya wanaume na wanawake uliopo sasa. Uhusiano huu, ambao umejaa mivutano, hughubika miundo yote ya maisha pakiwemo familia, elimu, kazi na siasa, utamaduni na hata mambo ya starehe na anasa. Hivyo basi, kwa kifupi ni kwamba uhusiano huu huongoza jinsi wanajamii wanavyoishi, wanachotenda, wanayemtendea, na jinsi watakavyokuwa siku za usoni.

45

Kama ilivyo na mitizamo mingine ya kijamii, Ufeministi una mizizi yake katika siasa ya ukombozi. Hasa, nadharia hii ilianguliwa katika muungano wa ukombozi wa wanawake uliopamba moto kunako miaka ya sitini (hasa Marekani). Baadhi ya mambo yaliyozingatiwa na muungano huu ni kuunda upya uhalisi wa mwanamke kwa kupangua na kudhihirisha miundo ya kijadi ambayo inamtukuza mwanamme na kumkandamiza mwanamke. Kutokana na muungano huu, palizuka nyanja tatu kuu za Ufeministi; Ufeministi huru (liberal feminism), Ufeministi wa kijamii (socialist-feminism), na Ufeministi mapinduzi (radical feminism). Japo nyanja zote tatu zimegusia muundo wa jamii na tofauti za kimaumbile kati ya mwanamme na mwanamke, kila moja inahimiza mkondo fulani wa maoni. Wafeministi huru huchukua kwamba maisha ya jamii na uamuzi wa kupata watoto unategemea wahusika wenyewe; na kusisitiza uhuru wa wanawake kama watu binafsi wanaopaswa kuwa na uchaguzi ambao haufungwi na tofauti za kiuana. Kwa hivyo nia ya mtizamo huu ni kuona kwamba mwanamke anapata nafasi ya kujichagulia mkondo wa maisha anaotaka kuuchukua. Aidha, mtizamo huu hupendekeza pawe na usawa katika ulezi wa watoto na iwe ni kazi yenye malipo kama kazi nyinginezo. Kama hili litatimizwa, basi atakayehusika katika kazi hiyo, awe amechagua mwenyewe sio kwa kushurutishwa ni sababu za kijamii au kimaumbile. Katika Ufeministi mapinduzi hamna nafasi ya jamii kama ilivyo hivi sasa kwa sababu mtizamo huu unasisitiza kwamba ukandamizaji wa wanawake umehusishwa na tofauti za kimaumbile. Hususa, jamii yachukuliwa kama chombo kikuu kinachoendeleza ukandamizaji wa wanawake na suluhisho ni kutenganisha wanawake na wanaume ili wanawake waweze kutawala miili na maisha yao bila kuongozwa na wanaume. Ufeministi wa kijamii ni mtizamo unaochukua baadhi ya maoni yaliyoendelezwa na Karl Marx hasa kuhusiana na suala kwamba hali ya maisha ya mwanadamu ni zao la mahusiano ya kijamii ambayo huendelezwa na kubadilishwa na jamii husika. Kwa hivyo mtizamo huu hauchukulii mfumo wa kuumeni/upatriaki kama dhana moja bali kama muundo wa ukandamizaji unaobadilika kihistoria. Kwa hivyo masuala ya ubaguzi, ukapitolisti, na upatriaki ni namna za ukandamizaji zinazohusiana. Kwa mtizamo huu, wanaume wanapaswa kuhusishwa katika nyanja ya kulea watoto na kuwaacha wanawake wafanye uchaguzi wa maisha yao.

46

Mitizamo hii mitatu inapoingia katika fasihi huwa ni kama yachungua kazi za fasihi zinazoendeleza taasubi za kiume na hivyo kuzipinga na kuzipuuza. Aidha, inadhihirisha jinsi fasihi inavyotumiwa kuendeleza taasubi za kiume pamoja na kumkandamiza mwanamke. Vile vile mojawapo wa nguzo za Ufeministi ni kwamba hakuna nadharia yoyote ya fasihi inayotambuliwa vilivyo ambayo iliendelezwa na mwanamke. Hivyo basi, nadharia hii yaendelea, kwa vile mwanaume ameishi kujinufaisha kwanza, kila nadharia anayoiendeleza ni chombo kimoja cha kupalilia nafasi yake katika jamii na pia kuhimiza ukandamizwaji wa mwanamke. Nadharia hii yaamini kwamba ujenzi wa maana anayodhamiriwa kupata msomaji ni zao la maana ambayo tayari ipo katika jamii. Na kwa vile waandishi wengi ni wanaume, mtizamo wa wanawake pamoja na tajiriba zao za maisha hazipo katika kazi nyingi za fasihi. Na hili ladhihirika katika usawiri na uwasilishi wa wanawake katika kazi za fasihi ambapo mtunzi, ambaye aghalabu ni mwanaume, humsawiri mwanamke kulingana na tajiriba ya kiume na kama anavyotarajia mwanamke kuwa. Ndiposa, Wafeministi walioanza kazi za uhakiki kunako miaka ya sabini, wanasisitiza zaidi kazi zilizoandikwa na wanawake na zinazoeleza tajiriba ya mwanamke kama aijuavyo na aionavyo. Na pia wanazingatia kazi zinazopinga taasubi za kiume. Kwa mifano ya kazi hizi za tahakiki angalia Showalter (1977), Gilbert na Gubar (1979) na Jacobus (1979). Msingi wa ufeministi upo katika imana kwamba uana na tofauti zake ni tokeo la kijamii sio la kimaumbile; hivi kwamba hapana kilicho katika mwili wa mwanamke kinachomshurutisha kuwa mwuguzi na mwanamme kuwa daktari, mwanamke kuwa karani na mwanamme kuwa mkuu wa kampuni. Hulka, sifa, na amali walizonazo wanaume na wanawake ni zao la kijamii ambalo huzingatia kuwatayarisha ili kuchukua nafasi za kijamii walizotengewa. Ndiposa twaona hata kama hapana uhusiano wa moja kwa moja kati ya maumbile yetu kama wanaumme na wanawake na kazi za kijamii tunazozifanya pana uwiano usiotatanika kati ya kazi hizo na majukumu ya kijamii tunayolelewa kuyachukua. Hivyo basi kama hali zetu na tofauti zetu ni tokeo la kimakusudi la kijamii hali hiyo yaweza kubadilishwa. Huo ndio msukumo wa ufeministi. Mhakiki anayezingatia nadharia hii huwa basi anaiangalia kazi ile ya fasihi kama iliyoumbwa kutokana na tajiriba za kiuana alizonazo mtunzi. jinsi alivyowasawiri wahusika wake na sifa anazowapa huweza kueleweka iwapo tunafahamu maana ya kuwa

47

mwanamke /mwanamme katika jamii hiyo na muktadha huo. Mara nyingi huenda maoni ya mtunzi kama yanavyojitokeza katika sifa na hulka za wahusika wake huwa ni maoni yake au msimamo wake kuhusu uana kama alivyofundishwa na jamii yake au kama anavyotarajia uwe. Mara nyingine huwa anasawiri wahusika waliokiuka misingi ya maana na matarajio ya sifa zao za kiuana kama njia ya kupendekeza mabadiliko katika hali halisi ya maisha. Mara nyingi wengi wamechukulia Ufeministi kama nadharia inayopiga vita wanaume na hivyo basi kutoielewa ipasavyo. mtizamo huu aghalabu umetokana na jinsi dhana ya ufeministi ilivyosambazwa hasa nchi za kimagharibi ambapo wanaume walisawiriwa kama adui anayestahili kupigwa vita na wanawake. ukweli ni kwamba ufeministi husaidia kudhihirisha kwamba wanadamu wamelelwa ili kuchukua nafasi maalumu za kijamii ambazo zadhihirisha mahusiano kati ya wanawake na wanaume. Ni uhusiano huu ambao Wafeministi wengi wanaagiza uangaliwe upya ili kuwapa wanawake na wanaume nafasi sawa katika kumudu maisha na mazingira yao. Hivyo basi wanawake na wanaume hawakinzani bali wanasaidiana; lililo muhimu ni kwamba usaidizi huo uwe hauna masharti ya kuwakataza uhuru wa kuchagua jinsi na maana sawa aitakayo mhusika (awe mwanaume au mwanamke) katika kuyaendeleza maisha na kumudu mazingira yake. 2.4.6 NADHARIA YA UHALISIA Nadharia hii katika upana wake, humaanisha uwakilishi wa uhalisi wa mambo katika fasihi. Nadharia hii ilizuka katika karne ya kumi na tisa hususa kwa sababu za kupinga mkondo wa ulimbwende. Mhalisia huamini katika matokeo ya mambo na ukweli anaouzingatia ni ule unaoweza kuonekana na kuthibitishwa kwa tajiriba. Vile vile, wahalisia huiamini demokrasia kama hali ya maisha, na malighafi anayochagua kueleza maisha ni yale ya kawaida, ya kadiri na ya kila siku. Hivyo basi uhalisia hujikita katika mambo yaliyopo, tukio mahsusi na matokeo yanayoweza kuthibitika. Imani ya mhalisia ni kwamba kazi ya fasihi yapaswa kuwaweka wanajamii husika katika ulimwengu wao wa kawaida, wa kweli, na halisi. Hivyo basi hata picha za ulimwengu atakazoumba msanii, zapaswa kudhihirisa hali hiyo. Kama tulivyotaja hapo juu, uhalisia ulizuka ili kupinga ulimbwende ambao ulizingatia mambo ya kihisia na

48

yasiyo halisi maishani. wahalisia wanaona kwamba kazi ya fasihi yapaswa kuwa sahihi, iliyo wazi na inayozingatia maswala halisi moja kwa moja bila kupiga chuku. Maswala ya kati maishani huhusu maadili na hivyo basi msanii hana budi kuyazingatia kwa kiwango fulani cha uteuzi. Wahalisia wanashikilia kwamba msanii anapaswa kuteua lakini akiwa na nia ya kuendeleza maswala yake kama yanavyowahusu watu katika hali halisi za maisha. Mwelekeo huu wa uhalisi katika utunzi unamfanya mhalisia kumwona mhusika kama kiungo muhimu sana katika kazi ya fasihi (hususa riwaya). Hivyo basi anazingatia saikolojia ya wahusika katika hadithi. Mhakiki anayezingatia nadharia hii ya uhalisia, hupembua namna mtunzi alivyodhihirisha uhalisi wa mambo kupitia maudhui aliyoyazingatia na wahusika aliowasawiri. Hivyo basi, mhakiki hutizama jinsi ukweli ulivyodhihirishwa katika juhudi za mtunzi za kuchora hali halisi ya mambo katika wakati maalum. Kwa muhtasari basi msanii anatarajiwa kusawiri wahusika, matukio na mandhari yanayokubalika na kuaminika katika jamii ya wakati wake. Ufahamu wa mazingira na maisha anayoyalenga mtunzi ni nguzo muhimu kwa mhakiki wa kihalisia. Shida inayoletwa na nadharia hii ni kuchukulia kwamba uhalisi na maana yake hauna utata wowote katika jamii yoyote, ni kwamba unachukulia kuwa watu wote katika jamii hiyo waona uhalisi mmoja na kuwa na fasili sawa kuhusu maisha yao. 2.4.7 NADHARIA YA UHALISIA-NAFSI (THATHMINI-SAIKOLOJIA) Kiini cha nadharia hii ni tabia ya ndani ya mtunzi ambapo nia, azma, motisho na fikra za mtunzi ndizo huchukuliwa kama nguzo ya utunzi. Mwitifaki mkuu wa mkondo huu ni mtaalamu wa elimu ya nafsi Sigmund Freud ambaye mbali na kueleza vitendo vinavyozuliwa na nguvu za ndani za mtunzi alieleza kwanini vitendo hivyo hutokea. Kimsingi, Freud alielemea maana ya kuwa utamaduni hutumiwa kufinya na kuondoa hisia na hamu zetu za kinyama tulizonazo ili kutustaarabisha na kutuwezesha kuisha na wengine. Lakini huwa hisia na hamu hizi hazitoweki bali hutokea katika sura mbali mbali za maisha yetu kama vile katika ndoto, matamanio, na michezo yetu. Wahakiki walioegemea mkondo huu waliingiza maoni ya Freud katika fasihi huku wakiiona kazi ya mtunzi kama kielelezo cha hamu na hisia hizo.

49

Katika kueleza nguzo ya nadharia hii, Freud anamlinganisha mtunzi na mtoto anayecheza. Anasema kuwa kwa mtoto, jambo au kazi anayoipenda sana inayomridhisha, ni kucheza. Twaweza kusema kwamba mtoto awapo mchezoni, hufanana na mtunzi kwa ambavyo yeye (mtoto) huumba ulimwengu wake, au kwa maneno mengine yeye huvipanga upya vitu katika ulimwengu wake ili vimpendeze. Ni kosa kuchukulia kwamba mtoto huyu hatilii maanani huu ulimwengu wake; kinyume na hivyo, ni kwamba yeye huutilia maanani sana kiasi cha kwamba huhusisha kiwango kikubwa cha hisia zake. Ama kwa hakika, kinyume cha mchezo ni uhalisi. Ni katika ulimwengu huu wa mtoto ambapo anapata uhuru wa kutenda atakacho bila kukanywa na watu wazima. Hata ingawa kiwango kikubwa cha hisia zake huhusishwa katika huu ulimwengu wa mchezo, ifahamike kwamba huyo mtoto huubainisha ulimwengu wake wa mchezo na maisha halisi na hupenda kuvioanisha vitu vyake bunia na vile avipatavyo katika ulimwengu halisi. Ndoa hii ndiyo inayotofautisha kule kucheza na kuota (Phantasyzing). Kulingana na nadharia hii, mtunzi hufanya kazi yake sawa na mtoto anayecheza. Yeye huumba ulimwengu wake bunia ambao anautilia maanani sana - yaani anahusisha kiasi kikubwa cha hisia zake pale - huku akiutengamisha na uhalisia. Jambo hili la kubuni hufaidi mtunzi kwa vile kazi yake huwa ya kuvutia kwa hadhira yake. Mara nyingi mtunzi hutumia visa halisi vya maisha na kuunda huu ulimwengu bunia wake ambapo mambo anayoyazingatia huwa ni yanayoweza kutokea. Pana jambo lingine linalozingatiwa na nadharia hii. Baada ya mtoto kukua na kuacha kucheza na baada ya kupambana kwa miaka mingi kuhimili maisha katika uhalisia wake, huenda siku moja akajipata fikirani mwake amefikwa na ile hali ya kutenga mchezo na uhalisia. Jinsi watu wanavyokua ndivyo wanavyoacha kucheza na huonekana kana kwamba wamesahau raha waliokuwa wanapata mchezoni. Lakini yeyote anayemwelewa mwanadamu, hufahamu kwamba hakuna kitu kigumu kwake kama kusahau raha aliyowahi kupata. Ama kwa hakika hatuachi lolote, bali hulibadilisha na lingine, tukapata kitu chengine cha kuchukua nafasi ya shibe au utoshelezi uliyoletwa na mchezo. Yaani nafasi ya jambo moja huchukuliwa na lingine ili kuonekana kana kwamba la kwanza limetoweka. Hivyo basi wakati mtoto akuapo na kuacha kucheza, anachotengana nacho ni vifaa halisi, na badala ya kucheza yeye hushiriki ndoto. Hizi

50

ndoto, kulingana na nadharia hii, ndizo nguzo katika utunzi. Hii ni kwa sababu ni vigumu kuona ndoto za watu wazima ikilinganishwa na michezo ya watoto. Mtu mzima huona aibu kuwa na ndoto hizi kama amali za nafsi yake na kwa kawaida ataona ikiwa rahisi kukiri makosa yake kuliko kutoa kiini cha ndoto zake kwa yeyote. Mchezo wa mtoto huongozwa na matamanio yake. Aghalabu yeye hucheza akiwa `mtu mzima' na katika michezo yake, yeye hushirikisha yale anayoyafahamu kuhusu watu wazima. Hana sababu yoyote ya kusetiri matamanio haya. Kwa upande ule mwingine, mtu mzima anafahamu kuwa hatarajiwi kuendelea kucheza au kuota, bali hupaswa kutenda mambo kihalisia, kiutu uzima; hivyo basi anongozwa na kufungwa na matarajio ya kijamii kwake. Isitoshe, baadhi ya matamanio yanayozua ndoto zake huwa ni yale yanayohitaji kusetiriwa yasijulikane kwa wengine kwani huwa ni kinyume na matarajio ya jamii. Hivyo basi hawezi kuyatoa hadharani lau yatachukuliwa kuwa ya kitoto na yasiyokubalika. Lakini ni lazima yatoke ili atue. Hapo ndipo anapata utulivu katika utunzi: anayatoa katika utunzi. Kwa kawaida, chanzo na msukumo wa ndoto ni matamanio yasiyotimizwa, na kila ndoto hutokea kutimiza kila tamanio ili kuchukua nafasi ya uhalisia usioridhisha. Hivyo basi kazi ya fasihi, kulingana na mtizamo huo, huwa ni jaribio la kutimiza matamanio ya mtunzi ambayo hayakutimizwa katika ulimwengu halisi. Uhusiano kati ya ndoto na wakati, kwa kawaida huwa muhimu sana na huchukuana na vipindi vitatu - - navyo ni vipindi vinavyohusika katika ujenzi wa dhana katika binadamu. Kazi ya fikra huanzishwa na jambo linalotokea wakati uliopo na linalosismua matamanio ya mhusika. Kutoka hapo linarejelea tajiriba ya awali ambapo tamaa hiyo ilitimizwa; kisha inajenga hali inayohusisha wakati ujao inayowakilisha kutimizwa kwa tamaa hiyo. Kile kinachotokea ni ndoto inayobeba chembe chembe za asili yake kutokana na hali iliyoizaa hiyo ndoto pamoja na ukumbufu (memory). Hivyo basi wakati uliopita, uliopo, na utakaokuja huunganishwa pamoja na uzi wa matamanio na kudhihirika katika utunzi. Tunachokipata tangu michezo ya utotoni hadi ndoto na hadi kazi za sanaa ni kwamba Freud anataka kuonyesha jambo moja kuu; kwamba binadamu kwa kawaida huwa na hamu ya kubadili kilichopo na hasa kile kisichoridhisha au kisichotosha katika ulimwengu halisi. Kwa hivyo fikra zinaendelezwa katika kubuni hali ambapo matamanio

51

ambayo hayajaridhishwa hutimizwa. Hapo ndipo twaona kazi ya fasihi ikielezwa kama zao la ndoto na matamanio ya mtunzi anayehusika. Mhakiki anayezingatia nadharia hii ataichukulia kazi ya fasihi kama kielezo cha matamanio ya mtunzi na juhudi zake za kuyatimiza katika ulimwengu wa sanaa. Hapo inahitajika wahakiki kwa kiwango fulani wazingatie maisha halisi ya mtunzi husika ili kuielewa kazi yake ipasavyo. Nadharia hii yaweza kutumiwa kueleza sanaa kama vile ya sinema, muziki, na drama ambazo maudhui yake huenda yakadhihiri mambo ambayo hayatendeki kwa ulimwengu halisi lakini ambayo yanasisimua na kuvutia hadhira kwa ambavyo yanatoa picha ya mambo ambayo yapaswa kutokea. 2.4.8 HITIMISHO Ni kweli kwamba hizi ni baadhi tu ya nadharia za uhakiki zilizopo, hata hivyo tumejaribu kuonyesha kwamba kila nadharia ina kaida na kanuni zake ambazo huzitoa ili kuzingatiwa. Hamna nadharia yoyote ambayo yaweza kusemekana imejitosheleza katika uhakiki. Tutakariri tena kwamba nadharia anayoichagua mhakiki wa fasihi yapaswa kuongozwa na anachotaka kuthibitisha kwa kazi yake n.k. Wakati mwingine mtunzi wa kazi ya fasihi huwa hazingatii nadharia yoyote katika utunzi wake na hivyo basi huenda nadharia yoyote ya uhakiki itumiwe kuihakiki kazi yake mradi tu pawe na ithibati za kutosha katika kazi hiyo kuchukuana na maoni ya nadharia hiyo. Kwa upande mwingine huwa inadhihirika kwamba mtunzi alizingatia nadharia maalum katika kutunga kazi yake na hivyo basi nadharia hiyo hiyo itakuwa mwafaka zaidi katika kuihahiki kazi hiyo. Kwa mfano kitabu cha S.A Mohammed, Dunia Mti Mkavu hudhihirisha uzingatifu wa nadharia ya Umarx na tahakiki yoyote inayofanyiwa kitabu hicho huenda ikajikita katika misingi ya nadharia za ki-marx. Hali kadhalika kitabu cha E. Kezilahabi, Rosa Mistika kimezingatia nadharia ya utamaushi (Extistentialism) na tahakiki zake mara nyingi huzingatia nadharia hiyo. Pana nyakati ambapo kitabu kimoja au kazi moja ya fasihi huenda ikazingatiwa kwa nadharia zaidi ya moja kulingana na azma ya mhakiki. Hivyo basi hatuwezi kubana kazi yoyote ya fasihi kwa nadharia moja maalum. Kama tulivyotangulia kutaja, hakuna kazi ya uhakiki ilyo kamili na kila kuchapo, panazuka nadharia mpya ya uhakiki. Lililo dhahiri katika kazi nyingi za uhakiki ni kwamba zinachukuana na maelezo kuhusu

52

maisha ya wanadamu na mikondo na mikinzano inayoyakumba. Jinsi wanadamu wanavyojaribu kuuelewa ulimwengu wao ndivyo wanavyozua nadharia mbali mbali za kueleza maisha na tabia za wanajamii. Kwa jumla tumeona kwamba uhakiki ni kitendo kinachoongozwa na kaida maalum zilizopo. Hivyo basi mhakiki huwa na nafasi ya kuzizingatia huku zikimwongoza katika kazi yake.

53

SURA YA TATU

3.0

MAENDELEO YA FASIHI-ANDISHI Kwa vile tunazingatia kwa kijumla kazi za fasihi-andishi katika kazi hii yetu, ni

muhimu tuchukue nafasi ndogo tueleze jinsi kazi hizi zilivyoanza na kuendelea. Tutazingatia katika sehemu hii maendeleo ya tanzu tatu kuu za fasihi andishi - Tamthilia, Riwaya na Ushairi - ambazo aghalabu huchukua vigezo sawa katika kuhakikiwa. Kwa jumla, maendeleo ya tanzu hizi tatu za fasihi yamepitia vipindi mbalimbali katika historia na kila kipindi kimekuwa na athari kwa tanzu hizo, yaani mabadiliko ya kijamii kihistoria, yamedhihirika katika tanzu hizi za fasihi hususa katika fani na maudhui. Jambo hili litadhihirika zaidi wakati tutakapokuwa twazingatia utanzu mmoja mmoja. 3.1 TAMTHILIA UTANGULIZI: Tamthilia ni utanzu wa fasihi- andishi ambao twaweza kusema ni zao la mabadiliko ya fasihi kama kipengee cha utamaduni wa jamii. Jina tamthilia limetokana na kitendo `mithilisha' ambacho maana yake ni kufananisha au kumithilisha hali ya maisha fulani kwa vitendo. Tamthilia basi ni maigizo ya matukio au visa fulani kwa uhalisi wake kwa ajili ya kuyasawiri maudhui au maelezo fulani. Dhana ya tamthilia imekuwepo tangu asili na jadi hata katika jamii zetu za kiafrika kabla ya athari za kinagharibi kupitia ukoloni, kwa vile pamekuwepo sanaa mbali mbali za maonyesho ambazo humithilishwa na tamthilia. Ama kwa hakika ugeni au tofauti ya tamthilia ya fasihi - andishi na sanaa za maonyesho za hapo awali, ni katika kugawanya mchezo katika vijisehemu - matendo na maonyesho na kumpa kila mhusika sehemu maalum ya kushiriki. Mtindo huu bila shaka ni zao la mabadiliko ya kijamii. Kabla ya tamthilia tuipatayo siku hizi, maigizo kwa jumla yalihimiza ushirikishaji wa hisia kama

54

zinavyovutia bila shuruti. Hata wahusika walizingatia mambo papo hapo bila kupanga vile au kakariri yaliyohifadhiwa pahali fulani; yaani hapakuwa na nafasi ya kupanga na kuandika maigizo hapo awali kama ilivyo katika tamthilia ya siku hizi. Ama kwa hakika, mtindo tunaoupata katika tamthilia ya siku hizi umekopwa kutoka kwa ule wa fasihi ya kimagharibi ambao ulitufikia kupitia kwa elimu ya kikoloni. Mfano mzuri wa kazi zilizotoa athari hii ni zile za Shakespeare anayefahamika sana kwa utunzi wa tamthilia za kiingereza. Tamthilia ya aina hii hugawika katika matendo, na kila tendo huwa na maonyesho kadha. Kila onyesho huwa na waigizaji, kila mmoja wao akiwa na sehemu yake maalum ya kuigiza ambayo ametayarishiwa na mtunzi. Tamthilia hutofautiana na tanzu nyengine za fasihi kwa kuwashirikisha wahusika wake katika mazungumzo au vitendo ambavyo hubainisha hali ilivyo mbele ya hadhira. Tamthilia huihusisha sio tu lugha ya mdomo bali pia lugha bubu inayotokana na ishara za mwili wa mhusika. Kila mtunzi wa tamthilia huwaza jinsi kazi yake ingebainishwa jukwaani na ndiposa baadhi yao husisitiza mpangilio maalum wa mapambo jukwaani, kwani yote hayo husaidia katika kuyasawiri maudhui vyema zaidi. Jambo moja la kimsingi kuhusu tamthilia zote ni kwamba wahusika wote hukutikiana katika mikinzano na matatizo fulani. Lugha wanayotumia huwa ni ya kukunzana kwa vile kila mmoja kapewa jukum lake la kutekeleza. MAENDELEO Maendeleo ya tamthilia ya kiswahili yanachukuana na vipindi viwili vikuu - kuja kwa wageni na baada ya uhuru. Kabla ya mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki kuingiliwa na athari za kigeni zilizotoka ng'ambo, fasihi ya kiswahili, kama fasihi nyinginezo za Kiafrika, ilikuwa ni ya kusimuliwa tu (pasi na kuandikwa) na ilikuwa na tanzu kama vile ngano, sanaa za maonyesho, vitendawili, methali n.k. Tamthilia hivyo basi haikuwepo kama ilivyo sasa bali palikuwa na maigizo ambayo yalitolewa mbele ya hadhira kwa minajili ya kuongoa na kufundisha maadili au hata kutoa sifa kwa vitendo mwafaka vya wanajamii husika. Baada ya majilio ya wageni (Waarabu na Wakoloni) maonyesho haya yalianza kubadilika kwa kuingizwa katika maandishi na kuiga mitindo ya kimagharibi ili kuchukua mkondo wa tamthilia kwa jumla.

55

Kihistoria, tamthilila ilianza kwa kutongoa maudhui ya kidini ambayo aghalabu yalikuwa ni uteuzi wa visa fulani kutoka katika Bibilia ili kutoa funzo fulani. Pindi mabadiliko yalipoendelea kutokea katika maisha ya mwanadamu, hali hii ilibadilika hadi kuingia katika tamthilia zilizozingatia maudhui mengine kama vile vichekesho na hata ya huzuni. Peck na Coyle (1984:75) wanaunga mkono maoni haya hivi; "katika drama ya Kigiriki, wahusika walikabiliana na matatizo yaliyohusu uhusiano kati ya binadamu na miungu au Mungu. Katika karne ya kumi na sita hata hivyo msisitizo ulitoka katika dini na kuingilia maswala ya kijamii na tamthilia zikaanza kuzingatia maadili ya kijamii na kisiasa." Katika Kiswahili, tamthilia ya kwanza kabisa kutungwa na kuchapishwa ni ile ya Henry Kuria (1975) kwa kichwa cha `Nakupenda Lakini ......' ambayo ilitungwa katika enzi ya ukoloni. Maudhui yake sawa na tungo nyengine nyingi za wakati huo, yaliegemea zaidi upande wa kufurahisha. Huu ni mchezo wa kuigiza unaotongoa maisha ya kijamii, lakini maudhui yake si mazito na hayazingatii hali ya jamii kujisaka na kujitafiti. Twaweza kusema kwamba kwa muda mrefu sana kabla ya miaka ya sabini, tamthilia zilikuwa chache sana na nyingi zilikuwa ni tafsiri. Ndiposa katika fasihi ya kiswahili pana tamthilia za tafsiri kama vile Mfalme Edipode (19 ), Mabepari wa Venisi (19 ), Julias Kaizari (19 ) na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (19 ) . Yaelekea kwamba kazi za tamthilia katika kiswahili mbali na kuziba pengo lililokuwepo la kazi za tamthilia katika kiswahili, tamthilia hizi pia zilitoa athari katika mtindo wa utunzi ambapo tulipata zile zilizotungwa kishairi, na nyengive zilizotungwa katika hali ya mazungumzo. Baada ya uhuru, watunzi wa Kiafrika walijitoma katika ugwa wa maandishi ya tamthilia na hasa zenye maudhui ya kuonyesha ubovu na udhalimu wa wakoloni. Waandishi hawa walijitosa katika lindi la kuonyesha mwamko wa waafrika katika kuutetea na kuupata ukombozi wao, huku wakionyesha kila aina ya uonevu waliofanyiwa na wakoloni. Mathalani, waandishi Ebrahim Hussein katika Kinjeketile na Mugyabuso Mulokozi katika Mukwava wa Uhehe wanaonyesha hali hiyo katika utunzi wao. Halafu pakatokea mwamko mpya miogoni mwa waandishi asilia wa kiafrika waliotanabahi kwamba kuondoka kwa mkoloni kamwe hakikuwa kitambulisho cha mwisho wa dhuluma ya ukoloni, kwani ukoloni uliacha nyuma mwenzake kwa jina

56

ukoloni-mamboleo. Ndiposa twapata kazi kama vile Mashetani (E. Hussein) na Kilio cha Haki (A. Mazrui) zikitongoa maudhui ya ukoloni - mamboleo, unyanayasaji wake, mifumo ya kisiasa na sera za jamii katika nchi zilizojipatia uhuru wa kisiasa. Kwa jumla, pana mambo muhimu yanayodhihirika tunapotizama historia ya tamthilia. Maendeleo ya tamthilia kihistoria yamechukuana na mabadiliko ya kijamii. Jinsi miaka inavyopita ndivyo shughuli na mitizamo ya wanajamii inavyobadilika na mabadiliko yameratibiwa katika tamthilia. Hata ingawa tumetaja kuhusu kazi zilizozingatia historia ya ukoloni na baadaye ukoloni-mamboleo, watunzi wengine wamezingatia maswala halisi ya kijamii. Penina Mhando katika nyingi za tamthilia zake amezingatia maisha ya mwanamke katika jamii inayomtukuza mwanaume. Waandishi wengine wamepuuza maudhui yenye uzito na kuzingatia sanaa kwa ajili ya sanaa tu; yaani wakatunga kwa ajili ya kutunga tu. Tunaporejelea tuamthilia kwa jumla, twapata kwamba inayo mambo au vipengee muhimu vinavyoikamilisha. Tamthilia kwa kawaida huwa yahusus wahusika waliopewa majukumu ambapo wanawasiliana kwa mpangilio maalum ulio na sura na katika kutungwa kwake huwa inadhamiriwa kuonyeshwa na kutendwa (kuigizwa) jukwaani na kila kipengee chake lazima kulenga jambo hilo. Tuyazingatie mambo muhimu yanayoikamilisha tamthilia yoyote ile. Kwanza kabisa pana hadhira. Maonyesho hutokea tu kama pana hadhira, kwani madhumuni yake ni kugusa hisia za hadhira kwa njia moja au nyengine. Kwa hivyo kitendo cha kuigiza hutokea tu pale ambapo hadhiria inashuhudia maigizo. Katika tamthilia hadhira huwa ni wale wanaoitizama jukwaani wanaoisikiliza ikiigizwa redioni au hata wasomaji wake. Pili, pana mahali pa kuonyeshewa au mandhari. Kwa kawaida, kile kitendo cha kuwasilisha mchezo wa kuigiza (tamthilia) mbele ya hadhira huhitaji mahali pa kuonyeshea pawe kando na mahali pa hadhira. Hii ndiyo ile dhana ya jukwaa na huwa ni kwa sababu mbili kuu- - kwanza, ili kuwapa hadhira fursa ya kuona maigizo, na pili ili kutoa nafasi ya kuunda jukwaa kisanaa ili kuvutia na kuwa halisi kwa kitendo kitakachoigizwa. Tatu, pana watendaji/waigizaji. Hawa ndio uti wa mgongo katika kitendo kizima kwani ndio wanaotoa kitendo chenyewe na pia kuwafikishia hadhira kitendo hicho.

57

Wanaitumia miili yao, sauti zao na hisia zao ili kuwasilisha ujumbe wao. Muhimu hapa ni jinsi wanavyojitokeza na jinsi walivyosawiriwa na mtunzi kwa vile ni lazima usawiri wao (maneno, matendo na umbo) uwe wa kuchukuana na hali halisi wanayowakilisha. Kwa mfano, kama mhusika anaigiza nafasi ya mahabusi katika jela, lazima achorwe hivyo na sio vingine, lau sivyo hatakuwa mhusika wa kuaminika. Hatimaye, ni mambo yanayoigizwa. Kwanza kabisa lazima pawe na ujumbe fulani katika maigizo hayo na lazima pawe na uwiano wa kila kitendo na chengine ili kufanikisha dhamira ya mtunzi. Huenda kitendo chenyewe kikawa ni kichekesho, tanzia, hali ya kukejeli au kuwapa watu motisho na kuwahimiza kujisaka na kujirekebisha. Hapa ndipo twapata maudhui. Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayoifanikisha tamthilia kama utanzu wa fasihi lakini ni ya kimsingi na hayakosi katika tamthilia yoyote ile. HITIMISHO Katika sehemu hii tumeona jinsi ambavyo tamthilia kama tuijuavyo leo imepitia mikondo mbali mbali. Hili ni jambo la kawaida katika fasihi yoyote kwani kila fasihi na tanzu zake, hubadilika, kwa hivyo twapata mabadiliko ya tamthilia kutoka hali ya awali hadi ilivyo kwa hivi sasa. Kwa muhtasari, twaona kwamba tamthilia ilianza kama maonyesho ya kidini kunako miaka ya 1500 kule Ugiriki ambapo watu walidondoa sehemu fupi kutoka maandiko matakatifu na kuziigiza sehemu hizo ili kutoa ujumbe wa kidini. Baadaye, mkondo huu ulififia na pakaingia maudhui ya kuburudisha. Ikawa jukumu kubwa la maonyesho ya jukwaani ni kutumbuiza au pia kuhuzunisha. Katika fasihi ya Kiswahili vichekesho na kutumbuiza viligeuka na kuwa maigizo ya kuwacheka waafrika walioazimia kuwa wazungu. Hatimaye maudhui mazito ya kihalisia yakachukua nafasi ya vichekesho na watunzi wakaanza kutunga tungo zenye maudhui mazito zaidi. Hata hivyo kila kipindi cha kihistoria kina mifano mbali mbali ya kazi za tamthilia na hivyo basi hatuwezi kusema kuwa ni aina moja tu ya tamthilia inayopatikana katika kipindi maalum cha historia.

58

3.2

RIWAYA UTANGULIZI: Riwaya ni utanzu wa fasihi-andishi unaowiana sana na hadithi katika fasihi-

simulizi. Wakati mwingine tunaweza kusema kwamba riwaya ni hadithi iliyohifadhiwa katika maandishi. Tofauti inatokea pale ambapo mwandishi wa riwaya, kinyume na mtamba hadithi, anakuwa na wakati na nafasi ya kusawiri visa na wahusika wake vile anavyotaka. Mtamba hadithi naye huwa hana nafasi kama hii kwa vile yeye hutoa masimulisi moja kwa moja. Lakini naye ana nafasi ya kubadili usimulizi wake kwa jinsi anavyoipima hadhira na matarajio yake. Pametokea utata katika kujaribu kueleza riwaya ni nini. Wataalam wengi, kama walivyonukuliwa na Senkoro, F.E.M.K (1982:72) wametoa maana mbali mbali za riwaya. Mathalani, `Riwaya ni hadithi ndefu ambazo zimeandikwa - Matteru (1976); `Riwaya inaundwa kwa njia ambayo tukio lingine lolote likiongezwa au kupunguzwa litaharibu ukamilifu wake' - Nazareth (1972); `Riwaya ni mfuatano mahsusi wa visa vilivyapangwa kufuatia wakati na kwa njia ambayo chakula cha mchana huja baada ya chamsha kinywa, Jumanne baada ya Jumatatu, kuoza baada ya kifo na kadhalika' Forster (1949). Kilicho dhahiri katika maelezo haya ni kwamba hapana yale yanayoweza kudai utoshelezi, kila maelezo yana dosari zake. Hata hivyo, ili kuepuka tatizo hili twaweza kusema kwamba kilicho muhimu katika kueleza chombo chochote ni sura muhimu zinazokitambulisha. Bila shaka riwaya inazo sura zake. Kwa mfano ni wazi kwamba riwaya ni utungo ulioendelezwa kinadhari na huwa na urefu wa kiasi cha kuwezesha usawiri wa whusika pamoja na matendo yao. Vile vile huwa ni kazi ya kubuni lakini ambayo imejengeka katika ploti maalum na hujaribu kuyachora maisha ya jamii inayozingatiwa. Kwa hivyo twaweza kusema kwamba riwaya ni utungo wa kinadhari uliobuniwa na ulio na urefu wa kiasi kinachowezesha usawiri wa wahusika na matendo yao ili kuwakilisha uhalisi wa maisha ya jamii husika katika ploti maalum. Kutaja kwamba riwaya ni utungo wa kubuni na hali ni utungo unaowasilisha maswala halisi ya maisha ni jambo la kukanganya. Nia yetu katika kauli hiyo ni kuonyesha kwamba matukio na visa anavyovisawiri mtunzi huwa amevibuni lakini lazima visa vyenyewe viwe karibu na ukweli wa mambo; yaani yawe matukio halisi

59

ambayo huenda yakatokea katika jamii. Isiwe amebuni visa ambavyo ni dhahania ambavyo haviwezakani katika ulimwengu halisi. Hata hivyo hali ya ubunifu ndiyo inayoitambulisha kazi yoyote ya fasihi na kuitofautisha na kazi nyingine za kijamii; kama haingekuwa hivyo, basi hiyo ingekuwa kazi ya historia au ripoti ya matukio badala ya fasihi. Hata wahusika katika riwaya huwa ni watu au viumbe wa kubuniwa na mtunzi lakini hawakiuki sana mipaka ya watu katika maisha ya kila siku, na matendo yao huwa ni ya kawaida na yaliyojikita katika mantiki ya maisha ya kila siku. Kwa hivyo neno `Riwaya' aghalabu limetuniwa kumaanisha kazi za kinadhari zilizotungwa ili kujaribu kumithilisha uhalisi wa maisha ya jamii. Huwa inajaribu kubashiri yanayoweza kuwa ya kweli kwa kutumia ploti na matendo katika usawiri wa wahusika. Riwaya basi hutambuliwa iwapo itajaribu kuchora uhalisi wa maisha hata ingawa haifungwi na kaida za maisha halisi katika kuendeleza lengo lake. Mtunzi katika riwaya kinyume na shairi au tamthilia, hutumia lugha elezi na fafanuzi zaidi kwani yeye aghalabu hufanya kutoa matukio kinadhari na kwa mfululizo unaojenga kisa au visa. Hadithi ya riwaya huwa kamili kivyake bila kuegemea matukio, maoni, au maelezo mengine yaliyo nje ya kazi hiyo. Mambo ya nje yaweza kutumiwa kueleza zaidi matukio yaliyosawiriwa katika riwaya lakini ukamilifu wake kama kazi ya fasihi huwa hivi kwamba inatoa maudhui au hadithi inayojisimamia. MAENDELEO Historia ya riwaya ya Kiswahili hususa huchukuana na majilio ya wageni katika upwa wa Afrika Mashariki. Hata hivyo, riwaya hii ilianza kama hadithi zilizoandikwa kinadhari. Halmashauri ya kusanifisha lugha ya Kiswahili ilipoanzishawa mwaka 1930, ilileta mashindano ya uandishi wa hadithi fupi fupi na vitabu. Hapo ndipo palitokea vitabu vidogo vidogo kama vile Safari za Sungura, Hadithi za Mjomba Remus na Safari za Juma. Hata hivyo, hapo awali palikuwa na aina ya riwaya ya Kiswahili ambayo ilikuwa ni insha ndefu kuhusu tajiriba za Waafrika kuhusu ukoloni au tawasifu zao (Autobiography). Abdalla Bin Hamed Bin Ali alichangia sana hali hii alipoandika Habari za Wakilindi, kazi ambayo ilichapishwa na UMCA magila Press katika miaka ya 1895 - 1907. Vile vile palikuwa Tawasifu ya Tippu Tip ya mwaka 1902. Waandishi

60

wengine walifuata kama vile H.M.T Kayamba aliyeandika Tulivyoona na Tulivyofanya Uingereza (1932) ambapo alisimulia safari ya Kundi la Waafrika walioalikwa na afisi ya ukoloni mwaka 1931. Naye James Mbotela (1934) aliandika Uhuru wa Watumwa ambapo alisimulia kuhusu watumwa walioachwa huru; ingawa alichukua mkondo wa kuwatukuza Wazungu na Kuwaonyesha Waafrika kama watu duni na wenye dini za Kishenzi. Kazi hii ambayo ilifanywa kitabu muhimu cha kufundishwa shuleni ilikuwa na lengo moja kuu - - kudhihirisha, kwa mtizamo wa kiafrika (japo ulikuwa wa kikoloni uliotumia jina la Mbotela tu kuupa uzito wa Kiafrika), Waswahili, Waarabu na Waislamu kama wanyama walioendeleza biashara ya watumwa na ilhali kuasawiri waingereza kama waokozi waliotumwa na mungu (Mazrui na Shariff 1994:35). Hali hiyo ya uduni wa Mwafrika katika fasihi iliendelezwa na kwa wakoloni. Hii ni kwa sababu palikuwa (kama ambavyo tumetaja) na maandishi ya kazi za Kiswahili (riwaya) kabla ya kuja kwa Wageni (Wakoloni). Hata hivyo, baada ya kuja kwa Wakoloni, Waafrika walianza kutunga kazi zao wakifuata mkondo fulani uliofanana na ule uliopatikana katika vitabu vya tafsiri. Hii ni kwa sababu Wakoloni walipoingia Afrika Mashariki, waliwaonyesha wenyeji kwamba walikuwa na hatua ndefu ya kupiga kabla ya kufikia kiwango cha ustaarabu na uhalisi (katika utunzi). Jambo hili lilifanya vitabu vya tafsiri kuenea sana na kutumiwa kama vigezo vya kupimia ubora au ubovu wa kazi zilizotungwa na wenyeji. Ndiposa twapata ploti na usimulizi wa kazi za kwanza za mtunzi kama Shaaban Robert zilifanana na baadhi ya kazi za tafsiri zilizokuwepo. Fauka ya hilo ni kuwa hata wahusika wake walidhihiri hali hiyo. mathalani, wengi wa wahusika walionyesha hali ya unyenyekevu huku wafalme wakisawiriwa kama wenye nguvu sana na wahusika wakuu wakiwa waadilifu. Hizi zote ni athari za falsafa za Wakoloni kwa wenyeji. Isichukuliwe kwamba twapinga kuwepo kazi za tafsiri katika fasihi ya Kiswahili. Ukweli ni kwamba sababu mojawapo ya kuenea kwa vitabu vya tafsiri kwenya fasihi ya Kiswahili ni upungufu wa vitabu vya tungo asilia ambazo zingetosheleza wadhifa wa fasihi kikamilifu. Ni dhahiri basi kwamba kuweko kwa vitabu vilivyotafsiriwa kama ziada ya vitabu vya fasihi ni jambo la maslahi na maendeleo ya fasihi kwa jumla. ndiposa twapata maudhui katika vitabu hivi vilivyotafsiriwa ni ya kuwafurahisha wasomaji walioandikiwa - kuwapatia watu fursa ya kusoma fasihi isiyohitaji uzito wa

61

fikra kwa kuyaelewa yanayoendelezwa vitabuni humo. Hata hivyo, baadhi ya vitabu hivi vilivyotafsiriwa siku hizo vilitongoa maudhui yanayowatukuza Wazungu, kuonyesha ustaarabu na uwezo wao, huku wakiwatweza wenyeji. Mifano ya kazi kama hizo ni Mashimo ya Mfalme Suleimani. Mkondo huu uliathiri waandishi chipukizi kama vile Shaaban Robert (Kusadikika), M.S. Farsay, (Kurwa na Doto) Ali Jamadaar (Nahodha Fikirini) Mohamed S. Abudulla (Kisima cha Giningi) hasa katika muundo na usawiri wa wahusika. Kwa upande mwingine, hatuwezi kufikiria riwaya ya Kiswahili bila kuzingatia swala la kuja kwa Waarabu ambao waliwafunza Waafrika hati za maandishi na mbinu za kuchapisha. Kwa hivyo twaone majilio ya wageni katika upwa wa Afrika Mashariki yalileta mbinu ya maandishi na uchapishaji, hali ambayo iliathiri sana fasihi ya Kiswahili. Matokeo ya athari hizi ni kwamba hadithi na hekaya nyingi za Waarabu na Waajemi kama zile za Abunwazi, Alfu-Lela-Ulela n.k. zilitafsiriwa na kuingia katika fasihi ya Kiswahili. Vile vile pana hadithi kadha wa kadha za kizungu kama vile Hadithi za Esopo, Kisiwa chenye Hazina Mashimo ya Mfalme Suleimani n.k zilizotafsiriwa na kuingia katika uwanja wa fasihi ya Kiswahili. Licha ya kuwepo kazi hizi zilizowakilisha riwaya ya Kiswahili, utanzu huu haukupanuka sana wakati huo wa ukoloni. Hili halikuwa jambo la sadfa bali liliandamana na sababu kadhaa kwa mfano, palikuwepo ile hali ya kudunisha utamaduni wa Mwafrika na Kumfanya aabudu chochote cha wageni. Pia waingereza walihimiza mabadiliko kupitia elimu iliyosisitiza kiingereza ambapo kazi za asili ya kiingereza ziliingizwa katika sera ya elimu. Wakati huo huo Kiswahili kilipingwa sana na wakristo kwa kuhusishwa na dini ya Kiislamu. Sababu nyengine ni kuwa watafiti wengi wa kigeni (ambao ndio wangechangia katika kurutubisha riwaya ya Kiswahili) walihimiza zaidi ushairi na fasihisimulizi. Hivyo basi utanzu wa riwaya ukapuuzwa. Katika miaka ya sitini, palitokea waandishi wengine kama vile Mohamed Saleh Abdulla Farsay aliyetunga Kurwa na Doto (1962), J.A. sipendi aliyetunga Kisa cha Germana, Monka na Shetani (1962) na Shaaban Robert katka Kufikirika (1969). Linalodhihiri katika kazi hizi ni aina ya mambo yaliyozingatiwa mle. Waandishi hawa walitunga kazi hizo kwa kutumbuiza wasomaji wake kwa vile maswala yaliyotokea mle hayakuwa maswala ya kati katika jamii zao. Ndiposa katika kazi hizo twapata yale

62

mawazo ya ki-utopia ambayo yanahimiza ujenzi wa jamii mpya lakini kwa njia ambazo hazina mashiko ya kimantiki. Yaani matatizo ya binadamu yanatatuliwa kwa njia za kiholela kabisa ambazo hasipatikani katika hali halisi maishani. Hata hivyo, mwelekeo huu wa ki-utopia umeungwa mkono na wahakiki wengine wanaodai kwamba ni makosa kumnyima mtunzi au mwanadamu nafasi ya kuota kwani ni kigezo muhimu katika ubunifu wake ambacho humsaidia kwenda zaidi ya uwezo wake na kuunda picha za mambo anayoweza kujaribu kufikia katika maisha halisi. Katika miaka ya sabini, panazuka mkondo wa waaandishi kuzingatia zaidi riwaya pevu au (riwaya nyeti) zenye mwelekeo zaidi wa kisiasa. Hizi ni riwaya ambazo twaweza kuziita riwaya za kisiasa. Ni katika kipindi hichi ambapo riwaya ya `kimapinduzi' ilijitokeza, riwaya ambayo ilitanguliwa - na hata kuchochewa kwa kiasi fulani - ushari wa kimapinduzi. Riwaya hii ni zao la hali halisi ya kihistoria ya wakati huo. Yaani katika miaka ya sabini, nchi za Afrika Mashariki zilishuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi ambayo yaliziweka jamii katika hali ya matatizo. Katika kipindi hiki, maisha ya jamii yalikumbana na mabadiliko mapana ya kiuchumi na hata kisiasa. Maadili ya kijumla ya kijamii pia yalibadilika huku faida na fedha zikitiliwa maanani zaidi ya utu. Kutokana na hili, twapata waandishi wakitizama swala la ujenzi wa jamii mpya inayojali maslahi ya jumuiya badala ya maslahi ya kibinafsi. Wakatongoa maswali ya kati ya kijamii kujisaka na kutafakari zaidi. Mifano ya kazi kama hizi ni Kiu, Kichwamaji, Gamba la Njoka, Nyota ya Rehema, Kasri ya Mwinyi Fuad n.k. Vile vile palizuka riwaya ambayo twaweza kuita ya ukasuku ambayo watunzi wake huwa na tabia ya kurudia au kukariri bila ya kupima vizuri maneno na mahubiri ya viongozi wa kisiasa na wengineo. Inakuwa kazi zenyewe ni kama zimetolewa ili kutoa aina fulani ya propaganda ambapo wanaosoma kazi hizo hawahitajiki kuyapima yanayotolewa na viongozi na badala yake wanatarajiwa kuyameza moja kwa moja. Kazi kama vile Siku ya Watenzi Wote (Shaaban robert) Mtu ni Utu (Mhina G.A) na Ndoto ya Ndaria ( ) ni mifano ya kazi hizo. Mkondo wa riwaya nyeti uliendelea na kuingia katika miaka ya themanini kupitia kwa kazi kama vile Mafuta (Katama Mkangi) Kiza Katika Nuru (S.A. Mohamed) Utengano (M.S. Mohamed), Dunia Mti Mkavu (S.A. Mohamed) n.k. Lakini twapata aina nyengine ya riwaya ambayo haina sura za riwaya nyeti. Ni dhahiri shabiri kwamba jinsi

63

miaka inavyoendelea ndiyo idadi ya watu inavyoongezeka na eneo la ardhi kupungua. Hivyo basi bidhaa zinazozalishwa ili kukidhi mahitaji ya wanajamii hazichukuani na matakwa yao na hivyo basi panatokea tofauti za kuzigawa. Hapo ndipo watu wachache wenye uwezo wa kudhibiti mali hizo chache zizalishwazo huitumia silaha ya uhaba kuchuma na kujinufaisha wenyewe. Matokeo ya hali hii ni rushwa, biashara za magendo, ulanguzi, upikaji wa pombe haramu, wizi wa nguvu, ukahaba, kushuka kwa thamani ya fedha n.k. Hii ni hali ambayo imeendelea tangu miaka ya sabini na bila shaka imeathiri sana maandishi. Kwa upande wa riwaya, pametokea waandishi ambao wameandika kama njia ya kujitatulia matatizo ya kiuchumi. Waandishi hawa wameingia katika uwanja wa riwaya-pendwa ambapo zaidi hujishughulisha na mada za mapenzi na uhalifu. Kazi hizi zimejitokeza kwa wingi katika kipindi hiki si kwa lile lengo la hapo awali la kuziba pengo la upungufu wa maandishi ya fashihi bali kwa lengo la mwandishi kupigania na hali ngumu ya kiuchumi ya kipindi hiki. Aidha kazi hizi zimefaulu kujitosheleza kwa wingi kwa sababu mbili za kimsingi. Kwanza, ni kutokana na soko lake kubwa ambalo hasa uchapishaji. Baadhi ya kazi zinazoainishwa katika kigezo hiki ni kama vile Mpango (K.M. Kassam), Je, Kisasi? (H.A. Kimwanga), Nitakuja kwa Siri (Mbunda Msokile) n.k. Hivyo basi katika miaka ya themanini, riwaya nyeti si nyingi tukilinganisha na miaka ya sabini. Hata hivyo, pameendelea ile hali ya kutafsiri vitabu vilivyoandikwa na Waafrika katika lugha nyngine na kuviingiza katika fashi ya Kiswahili. Mifano ya vitabu hivi ni kama vile Boi, Mshale wa Mungu, Wema Hawajazaliwa, Mwakilishi wa Watu, Shetani Msalabani n.k. Kwa jumla, tunapotazama riwaya kama kazi ya fasihi-andishi, twapata kwamba ni utanzu wenye uwezo wa kuzingatia mambo kwa upana sana. Hivyo basi huenda mambo mengi yakazingatiwa katika riwaya moja au hata jambo moja tu likazingatiwa lakini kwa undani zaidi. Kwa kufuatia hali hii, panatokea aina mbali mbali za riwaya hasa kimuundo na kimaudhui. Ndiposa twaweza kupata aina zifuatazo za riwaya. Kwanza, pana riwaya ambayo itaratibiwa kwa kuhusishwa na wakati au kipindi halisi cha historia kinachojenga kazi hiyo. Hapa ndipo twapata riway zinazozingatia historia halisi ya jamii husika.

64

Pili, pana aina ya riwaya iliyo na misingi ya mkondo wa ulimbwende. Utapata katika riwaya kama hiyo, nguli hutokea na kusifika sana huku akihusishwa na visa vya kusisimua na vinavyomwathiri kwa njia moja au nyengine. riwaya nyingi zenye nia ya kufurahisha na kusisimua wasomaji wake hupatikana hapa. Watu wengine wameziita riwaya - pendwa. Tatu, pana riwaya ambazo huzingatia kwa undani sana fikra azma na hisia za mhusika au wahusika. Hivyo basi riwaya kama hii zaidi hujikita katika kuingilia kwa kindani maisha ya ndani ya mhusika mmoja au ya wahusika wachache ndipo twapata ile inayoitwa riwaya ya kisaikolojia. Vile vile utapata riwaya iliyojengeka katika nguzo halisi za kijamii ambapo mtunzi wake hujaribu kusawiri jamii nzima au hata kijisehemu kikubwa cha jamii hiyo kinavyotenda mambo. Aghalabu riwaya kama hii itajaribu kusawiri hali halisi ya maisha ya jamii husika huku ikidhihirisha shida zake, matamanio yake, na hata kutoa pendekezo la suluhisho kwa shida hizo. Hivyo basi utapata katika utanzu wa riwaya peke yake pana aina mbali mbali za utunzi ambazo zaweza kuainika. Hata hivyo sio lazima riwaya iweze kuratibiwa katika vigezo hivyo au vingineyo kwa vile wakati mwingine huenda riwaya moja ikazingatia vigezo viwili au zaidi. 3.3 MASHAIRI UTANGULIZI Ushairi ndio utanzu mkongwe kabisa katika fasihi na yamkinika ulianza tangu binadanu alipoanza kutumia lugha wakati wa kazi na mapumziko. Ushairi umechipuka kutoka katika nyimbo zilizoundwa na binadamu kutoa hisi zake alipoanza kushirikiana na kuwasiliana na wenzake. Ndiposa Senkoro, F.E.M.K. (1988:17) anasema; Baada ya kuzuka kwa lugha, fasihi ya Mwanzo ilifuatia. Fasihi hii ilitokana na kazi alizofanya mtu katika kupambana na mazingira Polepole alianza kutunga maneno na sauti Zilizofuatia mapigo ya zana za kazi. Baada ya muda alizitumia

65

sauti hizi hizi za mapigo ya zana zake za kazi kujiimbia nyimbo wakati alipokuwa akifanya kazi. Wimbo wa kazi, basi ukawa ndiyo fasihi ya mwanzo. Hivyo basi nyimbo zilitumiwa katika harakati za binadamu za kuzalisha mali ambapo mwimbaji aliathirika kihisia na hivyo kumsukuma kufanya kazi kwa dhati zaidi na kumsahaulisha ugumu wa kazi ile. Kufuatia hili, twaweza kusema kwamba ushairi asilia ulifungamana na nyimbo na ulitungwa kwa njia ambayo iliweza kuufanya ufuatie mapigo ya zana za kazi na kuweza kukumbukwa kwa urahisi. Kwa uzi huo huo twaweza kusema kuwa ushairi kama utanzu katika fasihi-andishi ulianza pindi taaluma ya kuandika na kupiga chapa ilipoanza Afrika Mashariki. Tungependa kutaja hapa kwamba neno shairi si sawa na ushairi kwa vile shairi ni mojawapo ya tanzu katika ushairi. Kwa hivyo katika ushairi twazingatia dhana ya namna ya kutunga shairi/mashairi na twapata tungo kama vile tenzi, nyimbo, wajiwaji, hamziya, tumbuizo, shairi n.k. Katika sehemu hii tutazingatia shairi kama utungo wa kisanaa ulioandikwa kwa matumizi ya lugha ya mkato na yenye mpangilio maalum unaoonyesha uzingatifu wa utaratibu wa urari na muwala maalum unaoheshimu kanuni za utunzi wa ushairi unaohusika. Kwa ujumla wake ushairi huwasilisha fikra na taswira mbali mbali ili kugusa hisia za hadhira. MAENDELEO Historia ya ushairi wa kiswahili haiwezi kuelezwa bila kurejelea swala la kuja kwa wageni katika Afrika Mashariki. Hii ni kwa sababu kuja kwa wageni hao kulisababisha mabadiliko katika umbo la shairi la kiswahili. Kama ambavyo tayari tumetaja, ushairi wa Kiswahili asili yake ni nyimbo; na kabla ya kuja kwa wageni, nyimbo hizi hazikufuata sheria za vina na mizani kama ilivyo leo. Aidha nyimbo hizo zilisimuliwa tu na watunzi hawakuwa na muda wa kukaa na kupanga nashairi yao kama ilivyo na waandishi wa siku hizi. Wageni (hasa waarabu na wazungu) walipoingia Afrika Mashariki waliwaletea wenyeji mbinu ya maandishi (waarabu) na uchapishaji (wazungu) na kuwafanya wawe na

66

uwezo wa kuandika na kuhifadhi mashairi yao. Wakati huo huo waarabu walikuwa na nyimbo zao za dini (kasida) ambazo zilitungwa kwa mpango maalum wa silabi zilizoishia kwa mapigo sawa ya sauti. Mpangilio huu uliendelezwa kwa`nyimbo' za kiswahili. Wenyeji nao walivutiwa na ufundi huo wa kuwa na mistari iliyoishilia kwa silabi sawa. Kwa vile kasida za waarabu zilikuwa katika mstari mmoja, ilikuwa vigumu kuandika mstari mmoja uliojitosheleza katika kiswahili. Ndiposa palizuka tungo zenye zaidi ya mstari mmoja. Tungo kama vile tarbia, tathlitha na takhimisa zilitokea zikionyesha tofauti katika idadi ya mishororo katika kila ubeti. Hata hivyo twaweza kusema kuwa mashairi aina ya takhimisa na hamziya yana asili ya kiarabu na tathlitha au utatu umetokana na nyimbo za kiswahili. Athari ya wageni haikuishia hapa, kwani Waajemi nao walichangia ushairi wa Kiswahili kimuundo kwa kusisitiza vina vya mwisho viwiane. Kimaudhui twapata athari za waarabu (hasa dini ya Kiislamu) na Wazungu (unyenyekevu kwa watawala) zikijitokeza sana katika mashairi yaliyotungwa na wanyeji katika kipindi cha kuwepo wageni hao. Ndiposa twapata mahairi ya zamani kama vile Utendi wa Mwanakupona, Hamziyya na utenzi wa Al-Inkishafi yanakita zaidi katika maudhui ya dini ya unyenyekevu. Mbali na athari hii, tutaongeza kwamba kwa vile wageni hawa ndio waliotamalaki nyenzo za uandishi na uchapishi, bila shaka hawangekubali kutoa kazi ambazo zilikiuka kaida na matarajio yao. Baadaye yalitungwa na kuchapishwa mashairi yaliyokuwa na maudhui mbali mbali yaliyolenga nyanja zote za maisha ya mwanadamu. Mfano wa mashairi kama hayo yaliyotungwa enzi hizo ni kama vile ya Muyaka bin Haji. Katika kipindi kilichofuatia, hasa baada ya nchi za Afrika Mashariki kupata uhuru wa kisiasa, mashairi yalitungwa yaliyoegemea maudhui mbali mbali. Pana yale yaliyozingatia vita vya uhuru, Mengine yakazingatia wakati wa na baada ya uhuru. Mashairi kama vile Sikate Tamaa (S.A. Mohamed) na Sauti ya Dhiki (A. Abdalla) yanatoa mifano mizuri ya maudhui ya mambo tofauti yakumbayo jamii kila mara. Mbali na kutokea mkondo wa kukiuka utunzi uliozingatia maudhui ya kidini, palizuka waandishi chipukizi (katika miaka ya sabini) ambao walipinga matumizi ya vina na mizani kama kigezo cha kutunga mashairi ya Kiswahili. Walitaja kwamba kila kitu duniani hukumbwa na mabadiliko. Walishikilia kwamba maudhui ndicho kitivo cha ushairi wa Kiswahili. Baadhi ya waitifaki wa

67

mkondo huu ni kama vile S.A. Mohamed na E.Kezilahabi ambao wamedhihirisha msimamo wao katika tungo zao. Hata hivyo mpaka wa leo haijakubaliwa ni mkondo upi wafaa kufuatwa. Pengine yategemea mtunzi husika, nia yake, na itikadi yake kuhusu utunzi. Lakini hata wanamapokeo wanaoshikilia kwamba uketo wa ushairi wa Kiswahili ni ufuasi wa sheria za utunzi hawapingi kabisa umuhimu wa maudhui (yanayosisitiwa na wanamapinduzi). Ama kwa hakika Kaluta Amri Abedi katika kitabu chake Sheria za kutunga mashairi na Diwani ya Amri, na ambaye ni mfuasi mkuu wa mkondo wa wanamapokeo, anakanganya hali hii asemapo katika utangulizi kwamba; Neno moja tukumbuke katika utungaji, maudhui Yazue vina, siovinakuzua mawazo. Ndiyo kusema, baadhi ya watungaji, hasa wale wanaojifunza, hukusudia kitu kingine lakinitaratibu ya vina kawalazimisha waingiekatika jambo jingine wasilokusudia, ili tu wapatanishe vina. Jambo linalodihirika kutokana na mawazo haya ya amri Abedi ni kwamba bado pana utata katika kuamua ni lipi la muhimu katika utunzi wa shairi la Kiswahili - ni maudhui au fani. Mzozo bado upo lakini hauwezi kusuia utunzi wala uhakiki wa kazi za kishairi. Hata hivyo bila kuunga mkono upande wowote ule, ni dhahiri kwamba pana mambo kadhaa yanayofanya shairi kuwa bora. Kwanza, shairi liwe na mpangilio mzuri wa mistari katika ubeti, na habari zinazozungumziwa ziungane tangu mwanzo hadi mwisho ili kuzua mitiririko maalum. Kila ubeti ujitosheleze kiujumbe ili kueleweka kivyake. Hivyo basi shairi liwe na maana. Mbali na hayo, utamu wa shairi upo katika jinsi ya kuficha maana katika mafumbo ili lisiwe rahisi sana kueleweka. Twaweza kuona shairi kama mchezo kati ya mtunzi na hadhira ambapo pana masharti na kaida wanazozielewa wote ili kuweza kuzhiriki katika mchezo huo. Kufahamu lugha iliyotumiwa, muktadha wa maudhui, na maana fiche ya maneno ni baadhi ya masharti anayopaswa kufahamu mpokezi wa shairi.

68

Kwa kuhitimisha twaweza kusema kwa jumla kuwa pana miundo mingi ya mashairi katika Kiswahili na aghalabu huratibiwa kutegemea idadi ya mizani, idadi ya mishororo, mkarara wa maneno, majibizano, maudhuni na urari wake.

3.4

HITIMISHO Maendeleo ya kazi za fasihi-andishi ya Kiswahili ni swala ambalo haliwezi

kujadiliwa kivyake bila kuhusishwa na maendeleo na historia ya jamii husika. Hii ni kwa sababu mabadiliko ya mtindo na maudhui ya kazi hizo yalikuwa ni zao la mabadiliko ya ujuzi, maadili, mielekeo, na urazini wa wanajamii husika. Ndiposa twapata vipindi vitatu maalum vya maendeleo hayo. Vipindi hivi tutavizingatia kama ifuatayo; kipindi cha kwanza ambacho chasimamia hatua ya mwanzo katika fasihi-andishi, kipindi cha pili kinachosimamia miaka kadhaa baada ya mwanzo lakini kabla ya uhuru na kipindi cha tatu kinachosimamia enzi baada ya uhuru hadi leo. Tutazingatia kila hatua moja moja. HATUA YA MWANZO Hiki ni kipindi ambacho twaweza kukiona kama kilichokuwa na utasa wa namna fulani kwa ukosefu wa nyenzo za maandishi na uchapishi. Hata hivyo kazi za mwanzo kabisa zilikuwa katika utanzu wa ushairi kwa namna ya nyimbo zilizoimbwa na wanajamii husika. Hapana ithibati zozote zinazoonyesha palikuwepo na maandishi (fasihi-andishi) kabla ya kuja kwa wageni toka magharibi na mashariki. Kwa wakati huo jamii ilikuwa inashirikiana sana, fasihi (ambayo ilikuwa simulizi wakati huo). ilikuwa chombo cha kuunganisha wanajamii pamoja na kuyajumulisha matukio yote ya utamaduni wao. Pia fasihi ilikuwa ni chombo cha kuhusisha kila mwanajamii hata hadhira yake. Twaweza kupendekeza kwamba imani za dini na falsafa ya unyenyekevu kwa dini za kigeni na himaya zake haikuwa imeingilia maudhui ya fasihi hiyo. Hatuwezi kukanusha kuwepo kwa utunzi ulioonyesha ubinafsi wa mtunzi na ubunifu wake. Tungo zenye sifa kwa shujaa, viongozi, mazingira, na maisha kama yalivyoeleweka enzi hizo lazima pia zilikuwepo. Ni baada ya kuja kwa taaluma ya kuandika na kupiga chapa ndipo tungo zilipoingizwa katika fasihi-andishi.

69

HATUA YA PILI Katika kipindi hiki twapata mataifa ya kimagharibi yalikuwa yakigawa Afrika kwa minajili ya kuendeleza utawala. Hiki ni kipindi ambapo pia twapata aina mbalimbali za vita - vita vya dunia na vita kutaka uhuru miongoni mwa nchi za Afrika. Kuja kwa wageni kulitoa athari zenye mashiko kwa fasihi ya kiswahili. Kuja kwa wageni wa mashariki (waarabu) kulileta mbinu ya maandishi na pia dini ya kiislamu. Hivyo basi wenyeji wakapata mbinu ya kuwasaidia kutunga kazi zao - vile vile umbo la mashairi ya kiswahili liliathiriwa na utunzi wa kiislamu (kasida) uliozingatia maudhui ya kusifu mtume Mohammed. Pia palitokea athari kwa maudhui ya fasihi ya kiswahili (hasa mashairi) kwa kuzingatia maudhui yaliyotoa fikira za Mungu mmoja na kuzingatia unyenyekevu kwa kuogopa kuangamia baadaye. Kwa upande mwingine, kuja kwa wageni wa Magharibi ambao walizua ukoloni wa kizungu, pia ulitoa athari kwa fasihi ya kiswahili. Wageni hawa waliwaletea wenyeji mbinu ya uchapishaji wa vitabu na kuvisambaza. Hivyo, basi wakapata njia ya kuhifadhi maandishi yao. Lakini wageni hawa walikuja kwa nia yao ya kutawala na kujiendeleza kiuchumi, hivyo basi kukawa iwapo wangeendeleza fasihi, basi lazima iwe na sura zitakazochukuana na nia yao. Ndiposa palitokea hali ya kulazimisha tafsiri za kazi za kigeni na pia kazi zinazotoa maudhui ya kidini na unyenyekevu. Hapa twapata watunzi kama vile Mwana Kupona (japo pana maoni kwamba kazi yake yapaswa kusomwa kama iliyokuwa ikidhihaki misingi ya kijamii iliyozingatiwa), Aidarus, na Shaaban Robert wakithibiti hali hiyo. Hata hivyo mkondo huo haukudumu sana kwa vile palitokea watunzi wengine walioanza kujiuliza maswali na kuanza kutunga kazi zilizoegemea maudhui ya matukio mahsusi katika jamii. Kazi kama vile Utenzi wa vita vya Maji Maji, Utenzi wa vita vya uhuru, Kusadikika n.k. zilizingatia maudhui ya mambo halisi katika jamii husika. Palitokea pia kazi za kuwahimiza waafrika katika vita vya uhuru huku pakidhihirishwa hadaa na hila za wageni hao. Hata hivyo bado palikuwa na shehena la vitabu vya tafsiri katika fasihi ya kiswahili kwani wenyeji bado hawakuwa wamehimili nguvu za kupiga chapa na kuandika.

70

HATUA YA TATU Baada ya utunzi kushika mizizi miongoni mwa waafrika, palitokea kazi nyingi ambazo ziliwafahamisha wasomaji kuhusu maswala ya kitawala na kijamii ya wakati huo. Fasihi ikatumiwa kama chombo cha kuibua na kuhamasisha urazini mpya miongoni mwa Waafrika. Hapa ndipo palikuwa kilele cha vita vya uhuru katika nchi za Afrika Mashariki (hasa miaka ya mwanzo ya sitini) na palitungwa kazi za kuonyesha dhuluma ya ukoloni. Baada ya uhuru palitokea mabadiliko ya mtizamo katika utunzi ambapo badala ya kukashifu dhuluma ya ukoloni - mamboleo, baadhi ya watunzi waliwapongeza viongozi na wapigania uhuru. Lakini ilidhihirika kwamba matamanio na matarajio ya uhuru yaligeuka na kuwa kinyume ndiposa Abdalla, A (1983:ix) alisema; Tangu nchi zetu zipate uhuru, yajapo mambo yahusianayo na siasa, fasihi ya kiswahili imebaki kuzungumzia na kujishughulisha zaidi na uchambuzi wa yaliyokuwa yakitendwa na wakoloni walipokuwa wametutawala na imekuwa ikiyafumbia macho yale maovu na makosa tuyatendayo sisi wenyewe. Kwa hivyo tukawa na kazi za fasihi za kikasuku ambazo silijaa sifa na propaganda kemkemu za wanasiasa na viongozi wengine huku maswala muhimu ya wananchi yakipuuzwa. Mara nyingi kazi hizi zilitungwa huku watunzi wakitaka kupata kutambuliwa na viongozi na hivyo basi kutunukiwa au ilikuwa viongozi wetu hawawezi kukubali kazi zichapishwe amabzo zilikashifu uongozi wao. Wengi wa watunzi waliotiwa kizuizini walikiuka matarajio hayo ya viongozi. Hata hivyo palikuwa na kazi zilizopinga hali hii baada ya watunzi kuona hatari ya mkondo huo wa kikasuku. Hapa ndipo twapata kazi nyingi za kimapinduzi. Kwa jumla twaweza kusema kwamba jinsi miaka ilivyopita, ndivyo wanajamii walivyobadilika katika mitizamo yao kuhusu maisha huku ubinafsi ukishika nafasi ya kwanza maishani. Mabadiliko haya yalijitokeza katika fasihi hasa ambapo watunzi walisawiri undani wa wahusika. Hapo ndipo twapata riwaya na tamthilia za kisaikolojia ambazo uketo wake upo katika matarajio na hisia za ndani za mhusika/wahusika na

71

zinazohitaji upembuzi na kujisaka kwingi. Mashetani (E. Hussein) na Shetani Msalabani (Ngugi wa Thiong'o) ni mifano ya kazi sampuli hiyo.

72

SURA YA NNE

4.0 4.1

UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI UTANGULIZI Pana watu wengi ambao husoma kazi fulani ya fasihi (shairi, tamthilia au riwaya)

mara nyingi na kuifurahia; pana wengine wanaoiona kazi fulani ya fasihi kama utanzu mgumu usioweza kueleweka. Pana uwezekano wa kusoma ama shairi au tamthilia mara nyingi na kuishia kutoielewa kazi ile. Kazi kama vile Arusi (E. Hussein) imepata kuwatatiza wengi waisomao. Ili kuepukana na tatizo hili, huenda likawa jambo mwafaka kushughulikia swala la `kazi za fasihi huhusu nini kwa jumla.' Iwapo tutapata picha sahili na halisi kuhusu jinsi kazi za fasihi hufanya kazi pamoja na mada zinazozingatia, basi huenda tutakuwa katika hali mwafaka ya kuelewa kazi yoyote ile kwa yakini. Hili huenda likawa jambo gumu kutekeleza hasa tukitanabahi kwamba pana kitu kiitwacho `uhuru wa mtunzi' ambacho humwezesha kuchagua sio tu utanzu wowote ule bali humwezesha pia kuchagua jambo lolote lile na akalishughulikia. Kwa hivyo hapana mipaka wala idadi maalum ya mambo yanayozingatiwa na kazi za fasihi. Hata hivyo pana njia mbili kuu za kuzingatia kazi za fasihi ambazo twaamini husaidia katika kuzielewa. Mtizamo mmoja ni ule ambao huzingatia zaidi mtunzi wa kazi ile. Uketo wa mtizamo huu ni dhana kwamba fasihi ni kielelezo cha hisia za mtunzi na juhudi zake za kuzidhihirisha hisia hizo kwa wenzake. Kwa hivyo mhakiki anayezingatia mtizamo huu, huzingatia kile kazi hiyo inachodhihirisha kuhusu hisia za ndani za mtunzi; yaani huwa anasoma kazi ile ili kuelewa mtunzi wake. Ingawa mtizamo huu umepata kuhimizwa na watu fulani, mara nyingi hauwezi kumsaidia msomaji ambaye haoni `hisia' zinazoendelezwa na hivyo basi hawezi kuielewa na kuifurahia kazi ile (kama hilo ndilo lengo lake). Kasoro nyengine ya mtizamo huu ni kwamba huzingatia

73

zaidi zile fikra na hulka za mtunzi kuliko matini yenyewe. Hivyo basi ni mtizamo wenye upungufu kwani unakosa kuzingatia swala la kati tunalopaswa kufikiria: kule kusoma kazi ya fasihi na kujaribu kuielewa. Mtizamo wa pili hushughulika na kuijadili kazi yenyewe. Kiini cha mtazamo huu ni maneno yaliyotumiwa katika kazi husika; na hapa mtunzi huwa ni kiumbe kilicho kando na huchukuliwa kama mjenzi- - mjenzi wa maana kwa maneno. Pindi tuzingatiapo mkondo huu, huwa tupo tayari kuzingatia maudhui na fani ya kazi ya fasihi kwa pamoja katika msingi maalum. Na huu ndio mkondo tutakaouzingatia katika sehemu hii huku tukijaribu kupendekeza baadhi ya mambo anayopaswa kutalii mhakiki afanyapo kazi yake. Kwa maoni kuhusu mkondo wa kwanza tafadhali rejelea sehemu ya nadharia katika sura ya pili. Maudhui ni kile kinachosemwa katika kazi ya fasihi. Fani ni jinsi kinavyosemwa, jinsi kilivyoandikwa, lugha iliyotumiwa, mbinu inazotumia. Iwapo tutataka kuielewa fasihi vilivyo, basi hatuna budi kuzingatia kipengee kimoja muhimu katika fasihi - matumizi maalum ya lugha. Lugha ndicho kipengee kinachoidhirisha fasihi na ndicho chombo kinachosafirisha anachokisema mtunzi. Kinadharia, kazi ya fasihi yaweza kuwa juu ya kitu chochote kile; hata hivyo pana mada fulani ambazo hutuhusu sote kama wanadamu na aghalabu hutokea katika maudhui mengi ya fasihi. Ama kwa hakika maudhui muhimu ya fasihi ni mada za kawaida kutokana na tajiriba za kila siku. Kile anachokifanya mtunzi ni kuchukua moja ya mada hizo na kuizungumzia kwa njia inayovutia kisanaa. Aghalabu huwa anatueleza mambo ambayo twayafahamu lakini haja yetu kama wahakiki ni kuona jinsi ambavyo mtunzi huyachukua mambo hayo na kuyafanya mapya kwa jinsi anavyopanga lugha yake. kama ambavyo seremala hujenga kipande cha fanicha kizuri kwa kutumia mbao za kawaida, ndivyo mtunzi huunda kitu kizuri kutokana na malighafi ya kawaida ya maisha na maneno. Hali hii huenda mara nyingine ikafanikishwa na kipawa alicho nacho mtunzi lakini hata hivyo pana kaida na kanuni zilizowekwa za kumfaa na kumwongoza mtunzi katika kazi yake. Hizi ndizo kaida na kanuni tunazonuia kudhihirisha hapa na kumwongoza mhakiki katika kuzipata na kuzichambua. Mojawapo ya kazi za mhakiki ni kuipambanua kazi ya fasihi ili ieleweke na impendeze msomaji wake.

74

Uchambuzi ama uhakiki wa kazi yoyote ya fasihi ni jambo ambalo wengi wetu hujishughulisha nalo ama kwa maksudi au kwa kutojua. Tunasema kwa kutojua sababu msomaji wa kazi ya fasihi huenda katika kule kusoma kwake "akaanza kuifananisha kazi hiyo na mambo ambayo pengine anayafahamu maishani mwake au kuifananisha na kazi nyengine ya fasihi aikumbukayo. Pindi afanyapo hivyo na aghalabu bila kupanga hivyo, basi huwa ameanza uhakiki" - Hough, G. (1973:5). Uhakiki unahusu kule kusoma maandishi kwa makini na kuyagawanya katika sehemu mbali mbali ili kuonyesha mambo muhimu yaliyomo huku pakitolewa misingi na sababu ya mtunzi kuzingatia mambo hayo. Kwa hivyo anayechambua na kuhakiki huwa anajishughulisha na kazi za watu wengine huku akizisoma kwa undani na kwa kuyatafakari yaliyomo kisha kutoa uzuri au udhaifu wa kazi hiyo. Jukumu la kuhakiki kazi yoyote ya fasihi hutokea wakati ambapo msomaji wa kazi hiyo anapoanza kujiuliza maswali kama vile:* * * * Ni kwa nini mwandishi katunga kazi hiyo? Ni mambo gani aliyoyazingatia? anayaendelezaje mambo hayo? Anataka kazi yake iwafikie nani? n.k.

Tukumbuke kwamba mtu yeyote anaposoma kazi ya fasihi, yeye huielewa kwa njia ya kipekee, kwani huwa anaongozwa na itikadi yake kuhusu fasihi na maisha kwa jumla. Kwa hivyo, atayaona mambo aliyoyakusudia mwandishi katika misingi ya itikadi yake. Kazi ya mwandishi huwa ni kutunga na huenda mambo atakayoyadhihirisha mhakiki yasiwe ndiyo alidhamiria kutoa mtunzi. 4.2 JUKUMU LA MHAKIKI Ama kwa hakika si rahisi kuitenga kazi ya uhakiki na kuiwekea mipaka ambayo inamwezesha mtu kusema kuwa huwa inaanza hapa na kuishia pale. Hii ni kwa sababu pana viwango na misingi mbali mbali ya kuzingatiwa katika uhakiki kama tulivyotaja hapo awali. Tumeona kwamba yeyote anayelinganisha kazi yeyote ya fasihi na tajiriba yake, basi huenda akaitwa mhakiki. Vile vile pana wahakiki mashuhuri ambao kazi yao

75

ni kuichambua na kuipambanua kazi ya fasihi huku wakitoa hoja za kueleza alichokusudia mtunzi asilia, alichomaanisha kwa kutaja hiki na kile, na hata kufaulu au kutofaulu kwake kisanaa. Hata hivyo, pana mambo muhimu ambayo mhakiki yeyote hupaswa kutimiza na kuzingatia katika kuhakiki kazi yoyote ya fasihi. Hii ni kwa sababu uhakiki ni kazi inayoweza kujisimamia na inazo kaida zake ambazo huzingatiwa. Kila mara mhakiki anapaswa kukumbuka kuwa kalamu yake inayotoa mawazo yake huwa ni kifaa kinachoweza ama kunufaisha au kuidhuru jamii husika. Uhakiki kwa jumla huchukuana au huwa umejikita katika misingi ya ile kazi yoyote ambayo inahusu kulinganisha, kuuliza, kutathimini na kuweka katika mpangilio fulani kazi ya fasihi. Mhakiki hivyo basi huenda akazingatia maswali kama vile:* * * * * * Mwandishi anatufahamisha nini? Kazi ya mwandishi inamlenga nani? anazungumzia nini na ni suluhisho gani analotutolea kwa shida alizozitaja? Mwandishi ametunga katika kipindi gani cha historia na katika mazingira gani? Ametumia lugha gani, mbinu na mtindo gani na kwa nini? Mwandishi alitaka au alidhamiria kutaja nini, na je, amefaulu kufanya vile? n.k. Mhakiki atayapata majibu kwa maswali haya kwa kusoma kazi ile kwa makini huku akifahamu anachotafuta kitabuni mle. Lakini la muhimu ni kukumbuka kwamba maswali haya anayojiuliza mhakiki huweza kueleweka tu kwa kutizamwa katika misingi ya lugha. Ni kwamba lugha ndicho kiungo kinachowaunganisha mhakiki na mtunzi na ni kupitia lugha aitumiayo mtunzi ambapo mhakiki hufahamu anamlenga nani, na anachokizingatia kwa vile bila lugha hamna maudhui. Baada ya kujiuliza maswali kama hayo, mhakiki hakomei hapo. Yeye hupiga hatua mbele na kuachana na swala la azma au lengo la mwandishi na kuanza

76

kushughulikia usanifu wa mtunzi katika kazi yake. katika kiwango hiki cha usanifu basi , mhakiki atatizama:* * Ni vipi mwandishi amewachora wahusika wake, je ni wahusika bapa au duara? Amewapatia majina ya aina gani hao wahusika wake? Yana umuhimu wowote katika kuendeleza maudhui yake; ni majina ya majazi au ni ya kubandika tu? * Ametumia wahusika kiasi gani? Wengi sana mpaka inakuwa vigumu kwa msomaji kukumbuka yaliyotokea kwanza au ni wachache sana hivi kwamba mhusika mmoja apewa jukumu kubwa sana na kumchosha msomaji? * * Amewachora wahusika wake vipi, wanaingizwa na kuondolewa kilazima au ni kwa utaratibu mwafaka? je, ametumia lugha ya aina gani; ni ngumu isiyoeleweka na hivyo kukanganya maudhui ama ni rahisi kiasi kwamba haimpatii msomaji kitu cha kutafakari? n.k. Kwa vile mhakiki huja kati ya mtunzi na msomaji basi hana budi kuridhisha pande zote mbili. Hivyo basi mhakiki anapaswa kujihadhari yeye kama binadamu kwani anazo hisia za kupenda na kuchukia hiki ama kile. Huenda akaongozwa na hisia kama hizo kutathimini sivyo kazi ya fasihi. Wakati mwingine huwa tunasoma vitabu fulani kwa sababu vimesifiwa na kupendekezwa na watu wengine. Hata shuleni na vyuoni huenda wanafunzi wakasoma vitabu vilivyochaguliwa na walimu wao kwa sababu ni vya marafiki zao. Ndiposa Gibbe. A.G.N.M. (1978:4) anasema; `.... kuna baadhi ya watu ambao hupenda kuhakiki vitabu vya watu wanaowahishimu au marafiki zao ili kufanya urafiki baina yao ukomae zaidi, na mara nyingi hujikuta wanaandika muhtasari tu wa maandishi hayo na kujaza sifa kemkem.

77

Jambo hili huenda likamkumba mhakiki yeyote yule. Hii, ama kwa hakika, ni hatari kwa kazi ya fasihi kwa jumla kwani badala ya kuiimarisha twaibomoa. Mhakiki anapaswa kufanya kazi yake kipofu bila kusukumwa na yaliyosemwa na wengine kuhusu kazi husika au hisia zake na uhusiano wake na mtunzi. 4.3 MISINGI YA KUZINGATIWA KATIKA UHAKIKI Kama wasemavyo Jefferson, A. na Robey, D. (1982) katika utangulizi wa kazi yao, ..........`Uhakiki umeendelea katika karne hii hadi kuwa somo la kifasihi linalofundishwa shuleni na hata katika vyuo vingine vya elimu'. Hili lisichukuliwe kumaanisha kwamba uhakiki ni mada mpya katika shuguli za binadamu. Ukweli ni kwamba uhakiki umekuwepo tangu asili na jadi laikin kinachoendelea na kubadilika na jinsi watu mbali mbali huhakiki kazi za fasihi. Siku hizi imetokea kwamba uhakiki ni kitendo kinachojisi-mamia na kinachozingatia kaida na kanuni maalum. Hata hivyo utapa kwamba kaida na kanuni hizo huenda zikawa tofauti tangu mhakiki hadi mwingine. Hii ni kwa sababu kaida anazozizingatia mhakiki kwa kiasi kikubwa hutegemea lengo analodhamiria kutimiza pamoja na imani yake kuhusu fasihi, na jukumu la fasihi hiyo kwa jamii husika. Kazi ya fasihi, hata ya aina gani, hutungwa ili kusomwa, kusikizwa, au kutazamwa na hadhira fulani. Lakini tukumbuke kwamba sio kila kazi iliyotungwa huweza kuainishwa kama fasihi. Pana kaida maalum za kifasihi ambazo hutawala utunzi wa kazi ya fasihi. Tumezipitia baadhi ya kaida hizo katika sehemu ya kwanza ya kazi hii tulipokuwa tunajadili swala la fasihi ni nini. Basi ni kaida hizo ambazo mhakiki hutathimini na kuona kama zimetimizwa na kwa kiwango gani. Kazi ya fasihi hutungwa kwa sababu mbali mbali ikiwemo haja ya kushawishi, kutumbuiza, kumotisha au hata kuunda upya mapisi kisanaa. Lakini kwa vyovyote vile, sababu kuu ya kutungwa kwa kazi ya fasihi ni kwamba tukio fulani (fikra, hoja au kisa) humfika mtunzi na akaona haja ya kuwahusisha wanajamii wenzake katika tajiriba ya tukio hilo ama kwa kuwafanya walione kama alionavyo yeye au kuwatolea tu hisia zake. Tunapotaja dhana ya tukio kama kisababu cha kuzuka kazi ya fasihi tunadhamiria kutaja kuwa kazi ya fasihi kamwe haitokei katika ombwe. Ni kwamba mtunzi pamoja na

78

kazi yake huathiriwa na mazingira yake, itikadi yake na ya wanajamii wenzake, historia, kazi nyingine zilizotungwa n.k. na hivyo basi mhakiki hupata kuzingatia mambo kama hayo afanyapo kazi yake. Tunachokisema hapa ni kuwa kazi ya uhakiki huongozwa na mambo mengi ambayo tayari yafahamika kwa mhakiki. Hizo ndizo tunazoita kaida na kanuni za uhakiki na ndizo tunadhamiria kutalii katika sehemu hii. Kwa kawaida mhakiki anapaswa kutilia maanani mambo yafuatayo, anapofanya kazi yake. JUMUIYA AU TABAKA LINALOTUNGIWA Kifasihi jumuiya ni lile kundi au tabaka la watu ambalo hulengwa na kazi ya mtunzi kwa vile kama ambavyo tumeshataja, ni dhahiri kuwa kazi yake yatungwa kumfikia mwingine. Iwapo mtunzi amezingatia swala maalum la kijamii katika kazi yake na angependa swala hilo liwafikie watu fulani basi hiyo ndiyo jumuiya yake; yaani kundi analolitaka lifikiwe na ujumbe wake. Pengine mtunzi anawatetea watu fulani katika kazi yake na mambo anayoyazingatia yanakaribiana na hali ya maisha ya wanajamii katika jamii yake; hivyo anakuwa anawalenga hao watu wa jamii yake. Isitoshe, huenda akawa anakashifu vitendo fulani vinavyofanywa na watawala kama vile Nikolai Gogol katika Mkaguzi Mkuu wa Serikali anavyoonyesha hila za wale walio na nguvu za kitawala. Kazi kama hii mbali na kulenga wananchi kwa kuwadhihirishia hila na matendo ya watawala wao, pia anawalenga watawala wenyewe huku akiwaonyesha ni vibaya kushiriki matendo kama hayo na hivyo basi kuwaomba wajirekebishe. Ni muhimu kwa mhakiki kufahamu jumuiya inayolengwa na mtunzi ili kiwe chombo cha kupimia ubora au ubovu, ukweli au uwongo wa matukio, uhalisi wa mambo na fikira za mwandishi katika misingi ya ukweli wa hali ya maisha ya jumuiya hiyo. Hivyo basi mhakiki atakuwa anajiuliza maswali kama vile; mtunzi analenga jumuiya yoyote? ni jumuiya gani? je, mambo anayoyazingatia yanachukuana na kuwafaa watu wa jumuiya hiyo? n.k. Jambo hili litamwezesha mhakiki kuona kama kazi ile ilikusudiwa kuwafikia watu fulani. Ni muhimu kwa mhakiki kuzingatia au kujali jumuiya inayolengwa kwa sababu ataweza kuelewa kwa nini mtunzi akachagua aina ya lugha na maudhui aliyochagua. Kila jumuiya huchukuliwa kivyake na lugha atakayochagua mtunzi yapaswa kuchukuana

79

na kiwango cha jumuiya yake; pia maudhui yake yapaswa kuwafaa watu wa jumuiya yake. Tuchukue mfano wa mhadhiri anayetarajiwa kuhutubia kundi la wanakijiji ambao aghalabu maisha yao ni ya kilimo na hawajawahi kufika shuleni. Mambo atakayoyazingatia, mtindo atakaouzingatia pamoja na lugha atakayochagua mhadhiri huyo yatategemea kwa kiwango kikubwa kundi hilo analolilenga. Itakuwa ni hasara kwake kwenda pale na kuwaeleza kuhusu chombo cha kisayansi kama kile kompyuta huku akitumia lugha nzito iliyojaa msamiati wa kisayansi. Hapo atakuwa hatimizi lengo lake la kuwasiliana na kundi hilo na hawatanufaishwa na maelezo yake. Hivyo ndivyo ilivyo na mtunzi. Lazima afahamu watu atakaowatungia kazi yake. Hicho ndicho kitakuwa kigezo cha kutathimini na kuhakiki kazi yake. Mhakiki ataweza kufahamu hadhira inayolengwa kwa kuzingatia maudhui na fani katika kazi anayoihakiki. Mathalan kazi zilizodhamiriwa kusomwa na watoto agahalabu huwa na lugha rahisi na visa vya kuvutia na kusisimua. Ndiposa twapata pana vitabu viliyotengwa kusomwa na watoto, vijana, wasomi n.k. Hivyo basi mhakiki ana jukumu la kuona kufaulu kwa mtunzi katika kuifikishia hadhira/jumuiya yake ujumbe wake. Kitabu cha Ebrahim Hussein (Arusi) kilichojaa jazanda na mafumbo hakiwezi kulenga jumuiya au hadhira ya watoto kwa ule ugumu wa maudhui na fani yake; iwapo lengo muhimu la kusoma kazi ya fasihi ni kuielewa. DHAMIRI YA MTUNZI Dhamiri hapa ni neno linalochukuana na ile azma, lile lengo au kusudi la mtunzi katika kuitunga kazi yake. Hii ni kwa sababu, aghalabu kila mtunzi huwa amesukumwa na jambo fulani (liwe zito au liepesi) katika utunzi wake. Kama tulivyotangulia kutaja, hakuna mtunzi anayeweza kutunga katika au kutokana na ombwe. Mwandishi, hata anapoandika tungo za kubuni, huwa amesukumwa na jambo au mambo fulani aliyowahi kushuhudia katika fikra zake au katika hali halisi maishani; hata hizi fikra hujengwa na mambo fulani ya tajiriba halisi katika maisha halisi. Kwa hivyo hakuna mwandishi (anayestahili tahakiki) ambaye hutunga bila lengo fulani. Dhamiri ya mtunzi hujitokeza katika wahusika aliowasawiri, jinsi anavyofinyanga visa vyakae na matumizi yake ya lugha. Mtunzi anaweza kuwa anadhamiria kuendeleza,

80

kusifu au kukashifu jambo fulani katika jamii, au wakati mwingine kushawishi nafsi za wanajamii wenzake. Haya yote ni kwa sababu fasihi ni zao la kazi ya binandamu. Vipi? Hivi kwamba mtu mmoja (mtunzi) anatumia ishara dhahiri za mazingira yake ili kuwawasilishia watu wengine hisia zake alizozipata kutokana na tajiriba yake, huku akiwa na nia ya kuonyesha kwamba wote ni washiriki katika hisia hizo. Hapo tunachukulia kwamba zao la kazi ya mwandishi kama vile fasihi, huwa na sura mbili kuu - - ya kwanza huonyesha uhalisi wa maisha, na ya pili ni kule kujaribu kushawishi msomaji kuchukua msimamo fulani kuhusu uhalisi huo. Ni juu ya mhakiki kutambua dhamiri kuu ya/za mwandishi na kujaribu kuona na kuthibitisha kama kweli imeendelezwa ikajitokeza bayana. Hapa mhakiki atajiuliza, je, mwandishi ameendeleza dhamiri yake mpaka akafanikiwa? Kwa mfano, mhakiki baada ya kusoma kazi ya mwandishi huwa yuko radhi kujiuliza kwamba mwandishi alikuwa na nia gani? Na je, ameiendeleza nia hiyo vilivyo? Huenda dhamiri au lengo la mtunzi likawa ni kuonyesha nafasi ya mwanamke katika jamii. Pengine amedhamiria kuonyesha kuwa mwananamke ni sawa na mwanamme. Ni juu ya mhakiki kuona kama kweli mwanamke amechorwa kama mwenye nafasi sawa na mwanamme katika kazi hiyo. Mathalani, tuchukue jinsi Said A. Mohamed (Utengano) alivyoonyesha nafasi ya mwanamke katika jamii ya wanaume wakatili kama vile Maksuudi. Mtunzi huyu amemuonyesha Maksuudi kama mwanaume mkatili anayejipenda sana, lakini hatimaye anaangushwa na mwanamke (Kazija). Vile vile twapata kwamba pale nyumbani kwa Maksuudi pametolewa amri fulani za kufuatwana, kama vile kutawishwa kwa bintiye na bibi kutohudumiwa na mkunga. Lakini amri hii yapuuzwa na kuvunjwa kwa juhudi za mwanamke. Hivyo basi twaweza kutaja kwamba mtunzi alidhamiria kuonyesha kuwa hata mwanamke ana nafasi katika jamii ya wanaume wenye kiburi na taasubi nyingi. Lakini dhamiri hii haishikilii hadi mwisho wa hadithi kwani Kazija anatoweka hadithini naye Maimuna (ambaye ni mhusika muhimu) anaokolewa na mwanamme (Kabi). Twaishia kujiuliza kama kweli ni lazima mwanamke aokolewe na mwanamme iwapo mwanamke an nafasi katika jamii husika. Je, mwandishi amehimili dhamiri yake? Au ameacha maoni na hulka yake kuteka usawiri wake hivi kwamba anakanganya dhamira yake.

81

ITIKADI Wakati mwingine itikadi ya mtunzi huisaliti dhamiri yake katika fasihi. Katika mfano wa dhamiri tulioutoa hapo juu, tumeona kwamba Said A. Mohammed alishindwa kuendeleza dhamiri yake. Pengine itikadi yake ilimsaliti akamfanya mwanamke aokolewe na mwanamme yuyo huyo aliyekuwa akikinzana naye. Mwandishi katika kuchagua ni nini atakachozingatia katika kazi yake, huwa anaongozwa na itikadi yake, na hii itikadi ni zao la mtazamo na msimamo madhubuti alionao mtunzi juu ya mambo mbali mbali ya maisha. Itikadi humaanisha yale anayoyaamini mtu, ambayo humwezesha kutizama na kuelewa maisha yaliyomzunguka katika ujumla wake; ni mambo anayoyakubali mtu kuwa ni ya kweli na anayopaswa kuzingatia na kuheshimu. Itikadi ni imani aliyonayo mtu kuhusu mambo ya maisha. Ni jambo la msingi katika fasihi kwani ni kigezo cha kupima na kutathimini kazi ya fasihi fulani kwa upande wa msomaji au mhakiki. Mawazo au rai yoyote atoayo msomaji hutegemea itikadi yake. Hii ni kwa sababu watu hutizama maisha na kuyaelewa kwa njia tofauti; na njia hizo mara hujitokeza katika namna wanavyoyaelewa na kuyasawiri maisha. Itikadi ni dira ya kupima ni mambo gani mwandishi anapaswa kuchagua kuandika na ni kwa madhumuni gani. Kwa upande wa mwandshi itikadi ndiyo humwezesha kusawiri wahusika wake vilivyo ili wakubalike katika utunzi fulani. Itikadi ni muhimu sana katika kuitazama kazi ya mwandishi, kwani ni vigumu kutoa uchambuzi na uhakiki wa halali kuhusu fani na maudhui ya kazi fulani bila itikadi. Fikra hazitoki mbinguni au katika ombwe. Fikra na mbinu au maumbo ya kisanaa yanaibuka kutokana na maisha halisi ya jamii zetu katika mitizamo mbali mbali ya maisha. Kwa hivyo itikadi ni kitu cha lazima katika uandishi na uhakiki wa kazi za fasihi. Hii ni kwa sababu mtu asomapo kazi yoyote ya fasihi huwa anaielewa kivyake. Yaani yeye huwa anayaona yale anayoyakusudia mandishi katika misingi ya itikadi zake. Kwa hivyo mhakiki kuwa na itikadi humwezesha kupima kufaulu au kutofaulu kwa mwandishi kulingana na itikadi za jamii husika. Hivyo basi atajiuliza, je, maadili anayoyazungumzia mwandishi yanapatana na itikadi au imani za jamii hiyo? Ni muhimu kwa mhakiki kutambua waandishi wale ambao kwa kuogopa kusaliti itikadi zake au za jamii nzima, hushindwa kutoa uhalisi wa mambo, hasa katika maandisii ya kimapinduzi.

82

Yaani anaweka usalama wake mbele na hivyo basi kuishia kutoa mawazo yanayopendeza watawala tu. Hatari iliyo katika maoni haya ni kwamba hatuwezi kabisa kujua itikadi ya mtunzi nje ya anavyoishi, anavyodhihiri katika kazi yake na kulingana na jamii alimokulia (iwe anaiunga mkono au aipinga). Mwandishi aweza kujitetea (kama atapata nafasi) na kusema kwamba itikadi yake ni hiyo ya kusifu viongozi. Hiyo ni tahadhari ambayo twaweza kumtolea mhakiki yeyote. MAUDHUI Wakati mwingi wahakiki hushughulikia mambo mawili makuu katika fasihi - -yale yanayozingatiwa na kuendelezwa (maudhui) na jinsi yanavyoendelezwa (fani). Aghalabu, wahakiki wa kazi za fasihi wamekanganya dhana ya maudhui na dhamira; huku wakisichukuwa kama zilizo sawa. Kwa kawaida, maudhui ni ujumbe muhimu unaojitokeza katika kisa kizima katika kazi ya fasihi; yaani, `kile kitu, mtu, sifa ya kibinadamu au hali ya maisha inayozungumziwa hadithini - Mazrui (1983:13). Kazi moja ya fasihi yaweza kuchukua maudhui mbali mbali pia. Ni nadra kupata kazi ya fasihi ambayo haizungumzii jambo fulani, na kama ipo, basi itakuwa vigumu kukubalika kama kazi halisi ya fasihi. Hivyo basi, kile kinachozungumziwa katika kazi ya fasihi ndicho tunachokiita maudhui. Huenda ikawa ni ukoloni -mamboleo, ulevi, dhuluma, ukoloni, tamaa, umalaya n.k. Ni kwamba maudhui huchukua hali mbali mbali za maisha lakini aghalabu utapata hayo maudhui yanachukuana na hali ya kisiasa, kiuchumi au kijamii, katika jamii husika na katika wakati maalum wa kihistoria. Kama asemavyo Mohammed, S.A (1984:41) "riwaya ina marefu na mapana ya maisha yanayosomba kila kitu cha uhai wa mwanadamu." Kwa hivyo twaweza kusema kwamba kazi ya fasihi huzingatia maisha. Lakini swala hili lazua maswali mengi. Kwa kiwango gani maisha huzingatiwa? Maisha ni nini au ni yepi? Panatokea shida kwamba maisha ni kitu kipana sana hivi kwamba hakuna kazi hata moja ya fasihi inayoweza kudai kuzingatia kila kipembe cha maisha. Ndiposa Mohammed, S.A (1984) anaendelea kwa kumithilisha mtiririko wa maudhui katika riwaya na mtiririko wa mto anaposema;

83

`.........mtiririko wa maudhui na dhamira ya riwaya waweza kumithilishwa na mtiririko wa mto mkubwa wenye ba-mchirizi unaotiririka kwa kasi ukisomba yale yaliyo karibu na mtiririko......................' Kutokana na mawazo hayo ya Mohammed, twaona kwamba kazi yoyote ya fasihi (sio tu riwaya) huzingatia kipembe fulani au maalum cha maisha, kwani kazi hiyo sawa na mto haiwezi kutambaa kila eneo la maisha. Ni muhimu kutaja kwamba mambo anayoyazungumzia mtunzi, yanapaswa kuafikiana na hali ya maisha ya wanaolengwa na kazi hiyo. Aghalabu, husemekana kwamba mtunzi mzuri ni yule anayepuuza maudhui yaliyotuathiri jana na juzi (isipokuwa kama anayatoa kama nguzo tu ya yaliyopo) na kuzingatia ya leo na ya kesho. Hii ni kwa sababu shida zenye tisho kubwa kwa jamii ni zile zijazo na zilizopo, wala sio zile zilizopita. Lakini hatutaki kuchukiliwa kama tunapuuza historia. Msisitizo wetu hapa ni kuwa tusishikilie sana ya kale huku tukiyafumbia macho yaliyomo na yajayo. Sio lazima kazi ya fasihi iwe inahusu mambo halisi ya maisha kwani huo ni mtizamo finyu. Mtunzi ana uhuru wa kuchagua jambo lolote lile bora tu liwe litachukuana na matarajio na tajiriba za hadhira yake. Mtunzi vile vile anapaswa kutunga kuhusu mambo yanayohusu jamii (sio maudhui finyu). Lakini kama ambavyo tumeshataja tayari, mtunzi hawezi kushughulikia kila kitu maishani, yeye huchagua ni mkondo gani wa maisha atakaozingatia; na hufanya hivyo kwa mpango fulani. Kuhusiana na hili Mohammed, S.A (1984:43) anasema; Katika upembuzi na uchaguzi, mwandishi lazima awe na kigezo yaani `criterion' au hataweza au hatakuwa na njia ya kutenga yaliyo mazima, yafaayo kuandikwa, na yalivyovunda, yapasayo kupuuzwa au kuandikwa kwa madhumuni ya kuyapiga vita. Kigezo hiki ni itikadi yake mwandishi. Ni wapi mwandishi hutoa maudhui au mambo anayoyazingatia hadithini? Tumeona ni katika maisha. Lakini kwa njia gani. Ni nini katika maisha kinachomfanya

84

atake kutunga na kuandika kazi yake? Mohammed, S.A (1984:44) ambaye ni mtunzi, anakiri kwamba; `siku zote huiachia kariha inifume na ichukue umbo la riwaya yangu. Jambo lolote linaweza kuzusha chanzo cha umbo hilo............ kwa mfano, methali ya Kiswahili, maneno ya hekima, tukio nililoliona au nililosikia, mandhari, hali ya hewa n.k.' Kinachodhihirika hapa ni kuwa hakuna mtunzi anayeweza kutunga ndoto, ni kwamba pana uhusiano kati ya kazi ya fasihi aliyoitunga na maisha halisi ya jamii anayotungia (na kiini cha ndoto hiyo kitakuwa katika hali halisi ya maisha iwe ni kuijenga upya, kuipuuza, au kuifafanua). Kazi ya mhakiki hivyo basi ni kutambua ujumbe ambao unajitokeza katika kazi nzima anayoizingatia huku akitoa mifano ya kuhimili hoja zake. Mathalan, katika kitabu cha Ebrahim Hussein cha Mashetani pana maudhui ya ukoloni mamboleo. Ni juu ya mhakiki wa kazi hiyo kuthibitisha, kwa mifano, linalomwelekeza kwenye maudhui hayo. Huenda lugha au matamshi ya Juma na Kitaru (kama shetani na binadamu katika mchezo wao mbuyuni) yakamfaa. ANWANI AU KICHWA CHA KAZI INAYOZINGATIWA Kichwa cha kazi yoyote ya fasihi chaweza kutumiwa kama msingi wa kuielewa kazi hiyo. Kichwa ni sawa na ishara ya kwanza inayoonekana katika kitu chochote, hivi kwamba ishara hiyo hutoa fununu kuhusu ni nini cha kutarajia katika kitu hicho. Kichwa huwa ni kama utangulizi au muhtasari wa kazi husika na hutoa mwelekeo wa kwanza kuhusu kazi hiyo. Wakati mwingine, huenda kichwa kikafananishwa na mlango wa kuingia katika nyumba hivi kwamba huo mlango unatoa nafasi (hata kama ndogo) ya mhusika kuwa na picha ya kile anachotarajia mle nyumbani. Hatuwezi kufikiria kazi yoyote ya fasihi bila ya kichwa hata kama ni shairi. Huwa ni pungufu kwa njia fulani. Kichwa hicho huenda kikatumiwa kama kinyume cha mambo yaliyozingatiwa kati kazi ile lakini kwa vyovyote vile, huwa kina uhusiano na yaliyomo katika utunzi ule.

85

Ni muhimu kwa mhakiki kutumia kichwa cha kazi ya fasihi anayoihakiki kama nuru ya kuiangazia kazi husika. Huenda akahitajika kujiuliza, ni uwiaono upi uliopo kati ya kichwa na maudhui, dhamira na wahusika? au je, pana uhusiano wowote kati ya kichwa na mambo mengine yoyote muhimu katika kazi hiyo? Kwa muhtasari huenda tukawa na maelezo kama haya: kichwa Fani Wahusika Muktadha Maudhui Dhamira

Tahakiki

Yaani kichwa kitamwelekeza mhakiki katika nguzo muhimu za kazi husika ili hatimaye atokee na tahakiki yake. Mara nyingi kichwa cha kazi ya fasihi huchukuana na mambo yanayopatikana katika kazi hiyo hata kama si kwa njia ya moja kwa moja. Kwa mfano, vichwa kama vile Utengano (Mohamed S.A) Nyota ya Rehema (Mohamed S.N) Sauti ya Dhiki (Abdalla, A), Kilio cha Haki (Mazrui, A) Wingu Jeusi (Chacha N.C) n.k vina uhusiano na kile kinachozingatiwa katika hadithi nzima. Hakuna kichwa kisicho na uhusiano na mambo yaliyozingatiwa katika kazi husika na hivyo basi huwa muhimu sana katika uhakiki. Yaani mhakiki hapaswi kupuuza kichwa hicho. MANDHARI Ili kazi yoyote ya fasihi ieleweke na iwe ya kuvutia, haina budi kuwa na nguzo au msingi inamokulia. Kwa vile yamkinika kazi ya fasihi huwa inamulika uhalisia wa aina fulani, basi bila shaka lazima iwe na ulimwengu wake. Tutaipima kazi ya fasihi kulingana na vile ilivyoumbwa. Aghalabu, mandhari huwa kigezo muhimu cha kuielewa kazi ya fasihi. Jinsi mtunzi anavyojenga mandhari yake ni jambo linalosaidia katika kuelekeza msomaji katika kuelewa zaidi kazi hiyo. Kwa kawaida, mandhari huwa ni sura ya mahali hususa jinsi panavyoonekana katika hali halisi ya maisha. Mtunzi anaweza

86

kutumia mandhari kueleza mazingara halisi ya kisa anachosimulia katika kazi yake. Mathalani, mtunzi anaweza kutuchorea mandhari ya pwani kwa kushughulikia vitu kama vile upwa na ziwa, minazi, nyumba za makuti n.k. Jambo hili huleta hali ya ufasaha katika utunzi. Mandhari hutokea kuwa muhimu sana katika tamthilia, hii ni kwa sababu lengo la kutunga tamthilia ni kuiigiza jukwaani. Maigizo hayo hayawezi kueleweka iwapo mandhari yatakinzana na maudhui au wahusika wenyewe. Iwapo kwa mfano mtunzi atasawiri mhusika masikini hohe haha, twataraji, mahali anapoishi, maisha yake, na taswira yake kwa jumla iwe yadhihirisha hali hiyo lau sivyo hatakuwa wa kuaminika. Katika tamthilia ya Kilio cha Haki, A. Mazrui ametumia mandhari kwa ufasaha, na hivyo basi kufanya kazi yake iwe ya hali ya juu zaidi kisanaa. Katika utangulizi wa tamthilia hiyo kwa mfano, mandhari ya chini ya mti ambapo Musa anavuta sigara ilhali Dewe anajisomea gazeti, ni picha ya watu ambao hawana la kufanya hasa, na hivyo basi wanazembea tu. Katika onyesho la nne la kitabu hicho hicho, Mazrui anatuchorea mandhari yanayodhihirisha hali ya umasikini waishio Lanina na Mwengo. Hivi ndivyo anatueleza mtunzi; Ndani ya chumba kidogo kuna kochi moja bovu bovu, meza moja ndogo na viti viwili viko katikati ya chumba. Kando ya chumba kuna sufuria chache, masigiri mawili na visahani. Kama mandhari hayo yanadhamiria kutueleza kuhusu wanavyoishi wahusika hao basi twaona ile hali ya umasikini. Wakati mwingine mtunzi huenda akamweka mhusika masikini katika mandhari ya utajiri ili kutoa maana au picha fulani maalum. Hilo huenda likawa maksuudi na dhahiri katika mambo mengine katika kazi hiyo na mhakiki hana budi kudhihirisha hivyo. Maelezo kama hayo ya Mazrui hapo juu yanatutolea picha ya umasikini ambayo kamwe haionyeshi ukwasi. Kwa hivyo, twaona kwamba mandhari ni kigezo muhimu kwa mhakiki katika kupima kueleweka kwa utungo anaoshughulikia. Kwa kuangalia mandhari ya kazi anayoihakiki, mhakiki anafaidika katika kujibu maswali kama vile, je, mtunzi

87

ametuchorea mandhari yanayochukuana na wahusika pamoja na maudhui yake? Je, mandhari yanatekeleza jukumu gani katika kuilewa kazi nzima? n.k. MAZINGIRA ALIMOTUNGIA MTUNZI Wakati mwingine ni muhimu kutambua mazingara alimotungia mtunzi kama njia ya kumsaidia mhakiki kuelewa zaidi sababu ya uchaguzi wa lugha na maudhui katika kazi husika. Hii ni kwa sababu mazingara anamotungia kazi huathiri sana uchaguzi wake wa lugha na jinsi anavyoendeleza maudhui yake. Kuelewa mazingira alimotungia huenda kukamsaidia mhakiki katambua kinagaubaga maana ya mtunzi kutumia fani mbali mbali katika lugha, kuweza kutambua kama palikuwa na mshawasha wa namna fulani uliomfanya kuandika hivi na sio vile na pengine kutambua ni kwa nini kaandika. Mwandishi anapotunga kazi yake akiwa gerezani (Abdilatif Abdalla - Sauti ya Dhiki, Ngugi wa Thiongo - Detained) ni tofauti na anapoandika akiwa huru. Huenda akawa na maudhui yanayoonyesha chuki na ghadhabu kwa sababu ya yale maisha ya kifungoni au akatumia lugha ya mafumbo isiyoeleweka moja kwa moja. Anapotunga akiwa katika hekalu la viongozi (Muyaka) ni tofauti na anapotunga kazi yake akiwa kijijini pamoja na wanakijiji wenzake kwa vile sifa kwa viongonzi huenda zikadhihiri anapotungia hekaluni. Jambo hili litaathiri sio tu maudhui yake bali hata lugha yake. Katika uzi huo huo twapata kwamba hata yale mazingara ya kiwakati ambayo yahusu hali halisi ya wakati anapotunga kazi yake. Mathalani, wakati wa jioni huenda ukatoa sura muhimu za kuteua lugha kwa yale mazingira ya kutua kwa jua. Mtunzi pia huenda akaathiriwa na mazingira ya jua kali linalotoa mazigazi barabarani huku akiyatumia kuunda taswira na picha katika kazi yake. Isitoshe, mazingira ya kimsimu pia ni muhimu kwa vile hali hizo (kipindi cha mvua, baridi, kiangazai n.k) hutoa athari katika uteuzi wa lugha na hata maudhui. Kwa jumla hivyo basi, twaona ni jambo la ziada kwa mhakiki kuelewa mazingara alimotungia mtunzi (kama ataweza) ili kuelewa zaidi kazi ile.

88

HALI YA KIHISTORIA Kuelewa hali ya kihisitoria au kipindi cha historia alimotungia mwandishi ni jambo la kumfaa mhakiki wa kazi ya fasihi. Jambo hili litamwezesha mhakiki kutambua uhalisi wa maudhui na vile vile kuyaelewa zaidi maudhui hayo. Mabadiliko ya utamaduni na ya binadamu kupitia miaka mingi na mwendo wa jamii kiwakati na kinafsi, ni mambo muhimu sana kwa mwandishi yeyote kwa sababu mengi ya yale yaliyotendeka wakati uliopita katika historia huwa yanafungamana na mtizamo au picha yetu ya yajayo. Ama kwa hakika, mtizamo wa yale ambayo huenda yakamkumba binadamu katika maisha ya baadaye, huwa yanajikita kwenye misingi ya tajiriba zake za yaliyopita. Tunachokisema hapa ni kuwa kazi nyingi mashuhuri za fasihi zimeathiriwa sana na historia pamoja na matukio yake. Kwa mfano Kilio cha Haki (A. Mazrui) huenda ni kazi iliyoathiriwa na mgomo wa wafanyakazi Katika kampuni ya Del Monte ya Thika nchini Kenya, kazi ya Wingu Jeusi (Chacha N. Chacha) huenda iliathiriwa na mabadiliko ya maisha ya kijamii nchini Kenya huku wananchi wakizingatia zaidi ubinafsi katika mfumo wa kibepari, kazi ya Dunia Mti Mkavu (S.A. Mohamed) iliathiriwa na mgomo wa makuli katika bandari ya Zanzibar, kazi ya Gamba la Nyoka (E. Kelilahabi) iliathiriwa na utekelezaji wa siasa ya ujamaa nchini Tanzania n.k. Mifano hii yaonyesha kwamba hakuna mtunzi anayeweza kuepuka athari za yaliyotendeka au yanayotendeka katika mazingira yake. Kwa hivyo kila kazi ya fasihi huwa na muktadha wa kiwakati. Yaani kila kazi ya fasihi ni muktadha wa kihistoria; kwamba huainishwa katika kipindi fulani cha historia. Hata kueleweka kwake huchukuana na kuelewa kwa anayeisoma kuhusu kipindi cha kihistoria ilipotungwa. Waandishi katika kipindi fulani huwa wakati mwingine wanazingatia maswala sawa kwa kuwa na maadili sawa. Kufahamu kipindi cha kihistoria alimotungia mtunzi huenda kikawa kigezo cha kumwezesha hata msomaji kutambua ni nini cha kutarajia katika, tuseme, shairi la baada ya uhuru likilinganishwa na shairi la kabla ya uhuru. Wakati mwingine imesemekana kwamba riwaya (ambayo husomba mambo mengi ya maisha) zote huwa ni riwaya za kihistoria hivi kwamba kila riwaya kwa njia moja au nyengine huwa ni picha au dhihirisho la hali ilivyo au ilivyokuwa katika jamii husika. Hata ingawa huwa ni kazi ya kisanaa, yale mambo inayoyazingatia huwa

89

yanatokana na mambo halisi ya maisha katika jamii husika. Yaani kiungo maalum cha riwaya ni kile kinachohusu ripoti ya uhalisi wa jamii, hata kama haudhihiri uhusiano wa moja kwa moja na uhalisi huo. Mbali na riwaya, au kazi yoyote ya fasihi, kuwa imefungwa katika sheria za matokeo ya kila siku, huwa inajifunga kwa wakati maalum katika mahali maalum. Hivyo basi kazi hiyo hujengeka au kuumbwa katika kipindi fulani cha historia, na mandhari inamojengewa si tukio tu au sadfa bali ni kiungo muhimu cha maudhui ya kazi hiyo. Fasihi huweza kuwakilisha jamii fulani katika wakati fulani na ina jukumu la kuwasilisha mambo mengi kama yalivyokuwa/yatakavyokuwa, na mengi inayoyapitia ni ya kudhibitisha hali hiyo huku ikitoa ushahidi kamili. Fasihi huenda ikawa yatungwa kuburudisha na kupuuza maswala halisi ya maisha. Iwapo fasihi inamulika hali halisi ya maisha ya jamii, basi bila shaka huwa inahifadhi historia ya jamii hiyo na hakuna kazi ya fasihi yenye lengo hilo inayoweza kukiuka hali hiyo. Hivyo basi, tahakiki ya kazi hiyo ya fasihi itakayopuuza uhusiano wake na uyakinifu wa kihistoria huwa imekiuka mipaka ya uhalisi wa maadili ya kazi za fasihi hiyo na ni tahakiki isiyo kamili. PLOTI Ploti katika fasihi ni muundo wa matukio ya kazi ya fasihi (hasa riwaya na tamthilia) kwa jinsi ambavyo yamejengwa ili kufikia mguso fulani wa kihisia na kisanaa. Ni muhimu kutofautisha kati ya ploti na hadithi kwa vile wakati mwingine dhana hizo huchanganywa. Hadithi ni mfululizo wa matukio katika kazi ya fasihi. Ploti nayo hukiuka mpaka hiyo na kuingilia hali ya usababishano. Twaweza kutoa muhtasari wa kazi ya fasihi kwa kusema kwamba hiki kilitokea kwanza kikafuatiwa na hiki na hiki..... Lakini pindi tuanzapo kuona ni vipi kimoja kinahusiana na chengine na ni kwa njia gani kimepangwa ili kutoa mguso fulani, basi huwa tumeingilia ploti, na kama asemavyo Mohamed S.A. (1984:49) Riwaya hukua kimawazo, kifikra na falsafa, na pia katika mtiririko wa mambo na matukio, neno na neno, sentensi, aya, upeo, kurasa, sura n.k. Haya ndiyo matakwa ya riwaya kwa jumla katika kipengee hiki cha ploti.

90

Kwa hivyo hadithi au kiini cha hadithi hakijengi kazi ya fasihi, bali hujengwa kwa kupanua kiini au hadithi hiyo. Na upanuzi huo huchukuana na matukio yanayoambatana na wakati, kurasa za kitabu na mazingira yanayozingatiwa ili kutoa usababishano unaozaa ploti. Katika kukamilisha ploti, tamthilia na riwaya hustahili kupangwa, na pana mbinu nyingi za kufanya hivyo kutegemea mtunzi na aina ya kazi anayoitunga. Katika ploti ni muhimu pawe na vitushi vilivyo na uwiano; na kila hali iliyopita ni muhimu ifungamanishwe na kitushi kijacho ili pawe na mitiririko wa vitushi. Kwa hivyo ploti ni uchaguzi wa vijisehemu vinavyojenga hadithi kwa njia ambayo yatoa mfuatano na usababishano ili hatimaye kujenga kitu kamilifu. Sio lazima hadithi ifululize kwanza tangu mtoto kuzaliwa hadi kukomaa na hatimaye kufa kwake. Huenda mtunzi akatuonyesha kwanza maisha yake ya uzeeni na kisha akaturejesha katika ujana wake. hapa ndipo ploti inakuwa muhimu, na ni juu ya mhakiki kuutizama ufanisi wa mtunzi kiploti. Iwapo tunaweza kutoa mfano wa jinsi ploti inavyodhihirika tunaweza kufikiria kitabu kilicho na visa vinane tofauti lakini vinavyojenga hadithi nzima - - 1,2,3,4,5,6,7, na 8. Mtunzi anaweza kuvipanmga visa hivyo hivi kulingana na ploti yake:-

2

6

8

4

7

1

3

5

Yaani sio lazima kisa cha 1 kifuatiwe ni kisa cha 2 na cha 3. Hivyo basi twaweza kupata mtunzi ameanza kazi yake kwa kisa cha mwisho cha hadithi kama alivyofanya mazrui katika Kilo cha Haki. Katika kazi hiyo twapata mwanzo wa hadithi ukiwa ni Dewe na

91

Musa kutoroka kwao wakiishi uhamishoni. Ni baada ya kisa cha mwisho tunapotambua kuwa walitoroka baada ya vifo viliyotokea mwisho wa kitabu hicho. Twaweza kuibana dhana hii ya ploti na kutizama katika kiwango cha maneno na sentensi. Kwamba mtunzi hufanya ploti hata katika kuyapanga maneno na sentensi zake ili kuathiriana na kutoa mguso unaohitajika. WAHUSIKA Mhusika katika fasihi ni kiumbe cha hadithini kilichobuniwa na msanii ili kuendeleza hoja na maudhui yake katika kazi yake. Mhusika husaidia katika kuendeleza mada nzima anayoizingatia msanii hususa kwa kufululiza vitushi na visa mbali mbali katika kazi ya msanii ili kuwafikia wasomaji au wasikizi wake. Aghalabu, kila kazi ya fasihi huwa na mhusika au wahusika na huwa wamebuniwa na msanii ili kuchukuana na anachotaka kukifafanua. Ufanisi wa uwasilishaji wa ujumbe wa msanii mbali na kutekelezwa ni lugha, hutekelezwa pia ni uchaguzi pamoja na usawiri wa wahusika wake. Mhusika hupewa maneno dhana, na hulka ambazo ni muhimu katika kujenga hadithi, dhamira, na maudhui ya kazi ile. Kuwepo kwa mhusika katika kazi ya fasihi hususa hutegemea uwezo wa mtunzi wa kumuumba na kumsawiri. Mhusika huyo huenda akawa anawakilisha watu anaowafahamu mtunzi ambao pengine walimvutia kwa maumbile na tabia zao. Huenda akawa kiumbe ambaye mtunzi amewasikia wenzake wakizungumzia au amesoma katika maandishi mengine. vile vile huenda mhusika wake akawa mtu asiye na sura maalum, asiyeishi katika maisha halisi kwa sura na hata kwa umbo, lakini akawa ni kiumbe bunia alichokiumba mtunzi kutokana na tajiriba yake maishani. Kwa hivyo mhusika ni kielezo/kiwakilishi cha aina fulani ya watu waishio katika hali halisi ya maisha. Ndiposa Mohamed S.A. (1984:45) anasema; Mhusika kama Dude na Zuberi a Asali chungu, ni mhusika ambaye amehusihwakwamaishaalisiya jamii yangu. Kama ni mnyonge anayeonewa, basi anawakilisha wanyonge wanaonewa; kama ni bwana mkubwa mwonevu anayeonea, basi anawakilisha waonevu wanaoonea.

92

Dude huyu si dude maalum kwa maana ya Dude yeyote aishie Zanzibar, bali ni Dude wa hadithi anayejaribu kukopa tabia ya mtu au watu wanaopatikana katika jamii ya mwandishi. Hivyo basi pana ile dhana ya kwamba vitendo wanavyowakilisha wahusika hawa ni vya kuaminika. Kuaminika kwa ambavyo ama vimetokea au vyaweza kutokea. Pana aina mbali mbali za wahusika tunaoweza kuona katika fasihi kulingana na tabia zao na jukumu lao hadithini. Katika fasihi ya kiswahili twaweza kutaja kwamba pana aina mbili kuu za wahusika - wahusika bapa na wahusika duara. WAHUSIKA BAPA Hawa ni wahusika ambao zaidi hutambuliwa kama wahusika wasiobadilika na tabia zao zaweza kubashirika. Wahusika hawa huwa ni kielezo cha sifa fulani, na toka mwanzo hadi mwisho wa hadithi, wahusika hawa huwa wameumbwa kuchukuana na sifa hizo bila kubadilishwa na wakati, uhusiano wao na wengine au mazingira wanamotokea. Mhusika wa aina hii kama amesawiriwa kama kielezo cha sifa ya wema huwa anaiendeleza hali hiyo bila utata kutoka mwanzo hadi mwisho wa kazi ya fasihi anamotokea. Wahusika hawa huwa wanatumiwa na msanii kama chombo kilichotayarishwa kutimiza lengo fulani bila kujali hali za kawaida zinazotokea maishani. Wahusika wa aina hii huwa wanaweza kutambuliwa mapema kwani aghalabu hupewa majina ambayo huwa vielelezo vya tabia zao. Mifano ya wahusika hawa ni kama wale wanaopatikana katika riwaya za hapo awali kama vile za Shaaban Robert. Vile vile mhusika sulubu katika Nyota ya Rehema (Mohamed S.M.) ni mfano wa mhusika bapa. WAHUSIKA DUARA Hawa huwa ni wahusika ambao hutambuliwa kwa kubadilika kwao kitabia. Wahusika hawa ni kielelezo cha hali halisi ya maisha hivi kwamba tabia zao huenda tukaziita za kibinadamu kwani wanaonyesha hali yao ya kuwa na saikolojia pamoja na hisia. Wahusika hawa wanapewa wasifu wa binadamu halisi na kuwaleta karibu kabisa na ukweli wa maisha katika mazingira halisi. Hivyo basi vitendo vyao na tabia zao zinachukuana na tabia za binadamu yeyote yule katika jamii. Ni kwamba hawana uwezo

93

wa kuwapita watu wa kawaida. Hawa ni wahusika ambao wana desturi ya kubadilika kitabia, kimawazo au kisaikolojia kulingana na uhusiano wao na wengine pamoja na mazingira wanamotokea. Maisha yao yanatawaliwa na hali halisi za maisha. Mifano ya wahusika hawa ni kama vile Juma na Kitaru (Mashetani) Rehema (Nyota ya Rehema), Maimuna (Utengano) n.k. Kwa kawaida wahusika wakuu wa riwaya au tamthilia dhati (nyeti) huwa ni duara ilhali wahusika wadogo mara nyingi huwa bapa. Ni kwamba si rahisi kupata kazi ya fasihi yenye wahusika duara peke yao. Twaweza kujiuliza ni kwa njia gani tunatambua tabia za wahusika katika kazi ya fasihi? Kwa kawaida twaweza kuwatambua kwa: * * * * * Majina yao Majukumu yao katika kazi nzima Mahusiano yao na wengine Masengenyo ya wengine kuwahusu wao Maelezo ya mtunzi kuwahusu n.k.

Mhakiki hana budi kuchambua ni wahusika wa aina gani wamesawiriwa, ni majukumu gani waliopewa, kama wameendeleza majukumu hayo bila utata, na kama ni vinyago vya mtunzi vya kutoa maoni yake LUGHA Tunapozungumza kuhusu fasihi huwa kwa kawaida twazingatia au twazungmza kuhusu lugha na jinsi lugha hiyo imetumiwa. Huenda likawa jambo rahisi kushughulikia maudhui ya kazi ya fasihi peke yake lakini kamwe hatuwezi kupuuza kwamba kazi za fasihi hujengwa kwa maneno na hayo maneno huungana kujenga sentensi ambazo hujenga aya - - yaani lugha. Richards I.A (1924) katika Principles of Literary Criticism na hata wengine waliotoa misingi ya nadharia za uhakiki, wametoa mipaka kati ya lugha ya fasihi na lugha ya kawaida. Lugha ya kawaida ni lugha inayopatikana katika ripoti za magazeti kwa mfano, ambapo msisitizo unatiliwa mwasilishi wa habari au habari

94

yenyewe. Katika fasihi, lugha hutumiwa kwa njia ya `kihisia' - yaani kwa mbinu inayozua na kusisimua hisia za msomaji. Kwa hivyo lugha ni kipengee muhimu sana katika kazi ya fasihi kwani mbali na kuwa mtambo anaoutumia mtunzi kusafirisha maudhui yake kwa hadhira yake, humsaidia katika usawiri wa wahusika wake, kudhihirisha dhamira yake, kutoa mguso mwafaka n.k. Kwa hivyo kazi ya fasihi ni kama ujumbe unaotolewa na mtunzi kwa hadhira yake kupitia kwa lugha. Lugha itamsaidia mtunzi kuficha habari zake zisieleweke moja kwa moja iwapo huenda zikitolewa kiwazi zitamtia matatani. Vile vile kwa lugha anayoitumia mtuzi ni rahisi kutambua anaokusudia wanufaishwe na kazi yake. Kwa hivyo ni juu ya mhakiki kutizama na kuchunguza lugha ya mwandishi kwa makini. Kazi ya fasihi yahitaji kuwa na mnato wa kushika msomaji na kuibua hisi zake na kuogelea katika anachozungumzia mtunzi; jambo hili hutekelezwa na lugha anayoitumia mtunzi ambayo anaiteua kwa ujuzi ili uhai wa matukio upate kudhihirika. Wakati mwingine lugha imekuwa kigezo muhimu sana katika kutofautisha tanzu za fasihi. Mathalani, lugha ya shairi ni ya mkato yenye mafumbo ya tamthilia huwa ya majibizano na pia kinzani ilhali ile ya riwaya huwa ni elezi na pia fafanuzi. Kwa hivyo twaweza kusema kwamba fasihi ina lugha yake ambayo hutambulisha na yaweza kuhakikiwa. Na mtunzi anaweza kufahamu kwa hakika ni mambo gani atakayozingatia katika kipengee hiki cha lugha. Pana isitlahi kadhaa zinazotumiwa kuonyesha matumizi mbali mbali ya lugha ya fasihi na aghalabu hutumiwa na wahakiki wakati wanapofanya kazi yao. Lakini pia pana tanzu nyingine za lugha ambazo mhakiki hupaswa kuzingatia. Mambo kama vile uteuzi wa maneno, grafolojia, fonolojia, mofolojia, sintaksia, muundo, usimulizi n.k ni baadhi ya yale anayoyazingatia mhakiki katika kipengee cha lugha. Mohamed S.A (1984:) anatoa muhtasari wa hali hiyo anaposema: Lugha ya riwaya ni lugha ya kisanaa. Lugha ya sanaa ni ile inayojengwa, ama kwa makusudi au kwa sadfa tu, kuwa na uzuri (aesthetism), mvuto na mguso wa hisi katika maonjo ya wasomaji. Lugha yenye kufunua

95

milango ya hisi ni lugha ya hisi kwa nafsi yake, ambayo ina mbinu ya kitamathali (figurative) pamoja na mbinu nyingine za kisauti (phonological) za kiumbo la neno (morphological) pamoja na kumpangilia (syntactical). Kwa hivyo pana mambo mengi yanayojumulishwa ili kutimiza tahakiki ya matumizi ya lugha katika kazi ya fasihi. Pengine njia mwafaka ya kushugulikia swala la lugha ya fasihi ni kujifunga na mtindo yani jinsi maudhui yalikuvyowasilishwa. Mtindo waweza kuendelezwa katika viwango mbali mbali vya lugha na matumizi yake; lakini viwango vya kimsingi huwa fonolojia, sintaksia, maana, uteuzi wa maneno na uwiano wa maneno. Tungependa kutalii viwango hivi kimoja kimoja. FONOLOJIA Kipengee hiki kinahusu mfumo wa sauti zilizopo katika lugha yoyote ile. Sauti hizi huunganishwa ili kujenga maneno. Wakati mwingine mtunzi hutumia kipengee hiki ili kuboresha kazi yake kisanaa. Kwa mfano, kazi zilizotungwa kwa minajili ya kutendeka kama vile kuigizwa jukwaani au kukaririwa, huenda zikatumia kipengee cha kifonolojia kama vile kiimbo, shada au takiriri. Katika Nyota ya Rehema uk. 139 twasoma "Juu ya hivyo, alitaka afike kwake upesi,akitoe, akione, akishike, madhubuti mkononi." Hapa twapata takiriri ya sauti [k] ambayo yaongeza ufasaha wa sentensi hiyo. Watunzi wengine hutumia kipengee hiki cha fonolojia katika kazi zao ili kuzua ladha na mdundo hasa katika vina vya mashairi. Ubeti ufuatao kutoka katika Sauti ya Dhiki (Abdalla A.) uk 23 ni mfano mwafaka wa mdundo unaoendelezwa na takriri ya sauti [n] na [k]. Kana na kuku kunena, kunenwa kakutakiwi kuna wanakokuona, kunena kwamba si kuwi kunena wakikuona, kukuita hawakawi kunena kana kwanuka, nikukome kukunena?

96

SINTAKSIA Kipengee hiki huashira ule mpangilio wa maneno au vifungo katika utunzi. Na hili hutokea katika viwango viwili vya kimsingi - - urefu wa sentensi na muundo wake. Aghalabu urefu wa sentensi huenda ukategemea haja ya mtunzi ya kutoa fafanuzi, maudhui yanayoshughulikiwa (Maswala tata huhitaji sentensi ndefu elezi), ufasaha wa mtunzi katika msamiati n.k. Wakati mwingine sintaksia hutumiwa kusimamia sarufi. Hata hivyo sintaksia hujishughulisha na kuweka vipengele muhimu vya lugha katika sentensi, pamoja na uhusiano wa vipengele hivi katika sentensi. Kwa maneno mengine sintaksia humaanisha jinsi ambavyo mpangilio wa maneno huathiri maana. Sentensi nyingi za Kiswahili hufuata mpangilio wa mtendi, kitenzi na mtendewa. Ama kwa hakika jambo la kwanza tunaloliona katika ushairi ni ile hali ya ukiukaji wa mpangilio huo, na hili hutokea kwa maksudi ili kutimiza masharti maalum ya kisanaa. UTEUZI WA MANENO Kila kazi iliyoandikwa, hujengwa kwa maneno. Na maana yake huwa ni tokeo la maingiliano ya kila neno lililotumiwa katika utunzi huo. Tuchukue mfano huu wa sentensi kutoka katika Utengano uk. 48 pamoja na mfano wetu;

Mfano asilia: Maksudi alitupa bakora yake na sasa aliupapatua ukanda wake kiunoni. Aliuondoa na kuanza Kumcharaza nao mkewe. Mfano wetu: Maksudi alirusha chini bakora yake na akaufungua Ukanda wake kiunoni. Aliuondoa na kuanza kumchapa nao mkewe.

97

Mifano yote miwili, kwa kimsingi, yaelezea kitu kimoja. Sasa twaweza kujiuliza, kwa nini Said A. Mohammed alichagua mkururo wa kwanza wa maneno na sio huu wetu? Hata ingawa pengine hangefikiria maneno hayo yetu tuliyoyatoa, twaweza kukisia sababu zilizomfanya Said aandike maneno yake hivyo. Tuzingatie maneno yaliyopigiwa mstari kutoka kila mfano. Katika lugha ya Kiswahili dhana inayosimamiwa na `alitupa' na `alirusha chini' ni moja; kwamba palikuwa na kitu kilichokuwa kimeshikwa na kuachiliwa kwa nguvu fulani kikaanguka. Hii ni kwa sababu kitu kikitupwa au kikirushwa, hakina budi kuanguka chini kufuatia mvuto wa ardhi (gravity). Kwa hivyo twaona pana sababu ya uteuzi wa neno `alitupa'. Kwamba kuonyesha hali ya kihisia aliyokuwa nayo Maksuudi. Tunapoendelea kusoma sentensi hiyo twaona kuwa Maksuudi alikuwa amefunga ukanda ambao aliutumia kama kiboko kwa mkewe. Kueleza kitendo kile Said anatumia neno `aliupapatua' lenye dhana sawa na `akafungua'. Twaweza kuona kwamba kufungua ni tendo la kawaida ilhali 'kupapatua' ni ishara ya utumizi wa nguvu na pupa. Hivyo basi, ili kuendeleza ile picha halisi ya hisia za Maksuudi, Said aliteua neno `aliupaptua'. Neno `kumcharaza' latofuatinaje na neno `kumchapa'? Uteuzi wa neno `kumcharaza' alioufanya Said ni wa Masuudi ili kuonyesha ile hali ya kupiga kwa mfululizo kinyume na kule kupiga mara moja au mara kwa mara kunakoashiriwa na neno `kumchapa.' Kwa hivyo, twaona kuwa kila neno katika sentensi ni kiungo cha mtindo wa mtunzi. Kila neno lapaswa kuteuliwa kwa makini ili sentensi itoe ile maana na mguzo anaoutarajia mtunzi. Ni juu ya mhakiki kuona ndoa hiyo kati ya kusudi la mtunzi na jinsi alivyodhirisha kusudi hilo katika maneno na sentensi zake. Tunapozungumzia uteuzi wa maneno katika utunzi, dhana nyingine yatufika kwamba mtunzi mzuri husema kile unachopaswa kusema kwa maneno machache iwezekanavyo. Yaani twafahamu kwamba mtunzi ana mambo maalum anayotaka kusema. Hana budi kuyaeleza, yakealeweka kwa kutumia maneno machache iwezekanavyo. Hali hii hutokea sana katika tamthilia na shairi. Matumizi ya maneno mengi yanavyojaribu kueleza wazo moja huchosha na huenda msomaji asivutiwe na kazi hiyo. Kila neno linalotumiwa lapaswa kuchangia maana katika sentensi linamotokea. Vile vile, neno lisirudie dhana ambayo tayari imetajwa au kudokezwa na neno lingine katika sentensi au aya ile.

98

Lakini tungependa kutaja hapa kwamba hatupingi ile mbinu ya takriri ambapo neno hurudiwa katika sentensi moja au mshororo mmoja kama itokeavyo katika shairi. Nia yetu hapa ni kuonyesha kwamba kama neno moja tayari limeeleza dhana, hapana haja ya kutumia neno lingine lenye maana hiyo hiyo katika fungu hilo hilo hasa sio kwa minajili ya kutilia mkazo. Wakati mwingine pana ile hali ya watunzi `kufuja' maneno, yaani kutumia maneno mengi ambayo hayachangii katika kueleweka kwa kazi zao. Kwa mfano mtunzi anaposema `kufuatia hali kwamba Juma alikuwa mwanafunzi mwema zaidi ya wote shuleni, mwalimu mkuu hakuwa na budi kumpongeza.' badala ya `Mwalimu mkuu alimpongeza Juma kwa kuwa mwanafunzi bora zaidi shuleni.' huwa ni dhahiri kwamba mtunzi ametumia maneno mengi yasiyo ya muhimu sana. Hali nyengine inayofanana na huu `ufujaji' wa maneno ni, kule kutumia maneno ili kujigamba. Pengine hili ni tokeo la kutaka kujinata badala ya kuwasilisha ujumbe. Huenda mtunzi kwa kufanya hivyo akawa analenga kuonekana mweledi aliyemakinika katika lugha. Hata hivyo matokea yake ni kinyume na matarajio hayo. Wasomaji huweza kutambua wakati ambapo hoja sahili imefichwa katika mzunguko uliosabibishwa na matumizi ya msamiati mwingi usiostahili. Hoja hii yaturejesha katika ile tuliyotaja hapo juu, kwamba mtunzi hana budi kusema anachokusudia kusema kwa wekevu wa maneno na lieleweke. Huenda mhakiki akahitaji kutambua kwamba mtunzi bora huchagua maneno yake kwa sababu ya kile yanachomaanisha, kile yanachokipendeza na kwa kule kufaa kwake katika muktadha husika; huu ni utanzu mmoja wa mtindo. Twafahamu pia pana haja ya kuyapanga maneno kuwa mafungu, na utungo sahihi (sintaksia). Tanzu hizi mbili ndizo

99

nguzo ya mtindo katika utunzi. kwamba maneno huteuliwa ili kufaa na kuchukuana na mengine kwa kuunda tungo au sentensi. Hili halitokei kwa sadfa bali kwa maksudi. Mtindo mzuri ni ule ambapo maneno halisi yameteuliwa na kuwekwa pamoja kwa muundo mwema zaidi ili kusema (bila kutatanisha) kile anachokusudia mtunzi. Haya yote ni mambo ambayo mhakiki aliye makini hana budi kuyashughulikia. MAANA Tunapozungumzia maana ya sentensi au tungo, huwa kwa hakika tunagusia mambo matatu tofauti; kwanza pana habari inayotolewa na hiyo sentensi; yaani hoja, dhana na hisia zinazotolewa na hiyo sentensi. Pili pana pendekezo linalotewa na mahusiano ya maneno katika sentensi hiyo. Tatu ni mkazo unaotiliwa kila kipembe cha habari katika sentensi hiyo. Tuchukue sentensi hii ambayo tayari tumeipitia; Maksuudi alitupa bakora yake na sasa aliupapatua ukanda wake kiunoni. Aliuvuta na kuanza kumcharaza nao mkewe. Twaweza kuiandika upya sentensi hiyo ili isomwe hivi: Maksuudi alikuwa ambeba bakora. Alipotaka kumpiga mkewe, alirusha hiyo bakora. Maksuudi pia alikuwa amefunga ukanda kiunoni. Alifungua ukanda wake na kuuvuta ili autumie kwa mkewe. Alimcharaza mkewe kwa kutumia ule ukanda. Mbali na maelezo haya ya ziada pana maswali ambayo hatuwezi kupata majibu ya moja kwa moja. Kwa mfano, je, alitupa bakora wapi? alitumia mkono gani kufungua ukanda? Bibi alikuwa vipi? alipigwa wapi? n.k. Tunachotaka kusema ni kwamba pana mambo mengi yanayochukuana na tungo moja. Hata hivyo mtunzi huchagua kiasi cha habari atakachotolea msomaji wake na ni dhana gani atakoyoitilia mkazo kwa minajili ya anachokusudia kuwasilisha. Kwa hivyo twaweza kusema kwamba Said A. Mohamed

100

alidhamiria kutilia mkazo kile kitendo cha kucharazwa kwa mke wa Maksuudi na hivyo basi habari anayoitoa katika sentensi hizo yalenga kudhihirisha hali hiyo tu. Yaani hiyo ndiyo maana tunayopaswa kupata hapo. UWIANO WA MANENO Hili ni jambo la kimsingi kabisa analopaswa kulizingatia mhakiki yeyote kila afanyapo kazi yake ya kuhakiki. Litamwezesha kupima upeo wa kazi ile kifasaha. Katika uaandishi, pana ile hali ya uelewaji wa matini ambayo inajitegemea kiujumbe. Iwapo mtu mwenye ujuzi katika lugha fulani atasikia au asome taarifa fulani katika lugha hiyo, huwa ni rahisi kwake kutambua bila tashwishi kama taarifa hiyo ni kamili au ni kundi la maneno au sentensi ambazo hazipatani. Tunachotaka kudhihirisha hapa ni kuwa kazi yoyote ya fasihi ni kazi kamilifu ambayo inaeleweka kivyake. Lakini kazi hiyo ni tokeo la vipande mbali mbali vya taarifa ambayo huweza kuwa ni neno, maneno, sentensi, aya, au hata sura nzima. Kila kipande lazima kiwe na uwiano unaochangia katika kueleweka kwake. Vipande hivi ndivyo tutaita matini. Matini yaweza kuwa maandishi au mazungumzo, riwaya au shairi, malumbano au mazungumzo nafsi. Matini ni kiungo cha lugha katika matumizi. Lugha hutumiwa ili kusababisha mawasiliano kati ya mzungumzi na msikizi. Mawasiliano hutokea iwapo mzikizi ataelewa alichowasilisha mzungumzi kama inavyotarajiwa; yaani kupata maana inayokusudiwa. Ni maana hii ambayo hujenga matini. Kwa hivyo matini si sentensi kwa uhusiano wa moja kwa moja; matini ni maana iliyopo katika sentensi hiyo. Kwa hivyo matini ni zaidi ya maneno yanayojenga sentensi; ina umbo lake, ni umbo hili linaloifanya matini kuwa kamili na umbo hili lake hutokana na hali kwamba matini huwa ni kiungo chenye umoja kutegemeana na mazingira yake. Hivyo basi iwapo msomaji atapata taarifa fulani (iwe ni sentensi mbili au hata aya) anapaswa afahamu kwamba ili taarifa hiyo ichukuliwe kuwa matini, haina budi kuwa na vipembe fulani ambavyo vinachangia katika umoja wake ile kuipa umbo lake. Kwa mfano, tuchukue sentensi hizi mbili kutoka katika Nyota ya Rehema uk. 139; Ingawaje, Rehema hakujipa tamaa kubwa. Alijua, kwa mujibu wa kielezo cha Idrisa, kwamba angeweza

101

kuwa mrithi halisi wa mali adhimu aliyoacha marehemu baba yake, kama walivyo nduguze wawili. Ni wazi kwamba `alijua' katika sentensi ya pili inarejelea Rehema katika sentensi ya kwanza. Vile vile maneno `angeweza' na `kama walivyo nduguze wawili' yanarejelea Rehema hata ingawa pametajwa watu watatu katika sentensi hizo mbili. Twaona pana namna ya utegemeano unaojenga uwiano katika sentensi zote mbili. Hivyo basi zinastahili kuitwa matini au zipo katika matini moja iwapo pana mengine yanayofuatia. Katika sentensi hizi pana umbo ambalo limetokana na uwiano wa uhusiano uliopo katika ya maneno hayo tuliyotaja hapo juu. Ni kwamba uwiano huu nasababishwa sio na kipande kimoja tu (kama vile Rehema) bali ni kwa kuwepo vipande vyote viwili katika sentensi zote mbili. Yaani, haitoshi tu kuwa na kinachorejelewa bali pana haja ya kuwepo kiashiria iwapo matini itakuwa na umoja. Ndiposa ni vigumu kuelewa sentensi kama hii ifuatayo itokeapo peke yake "halafu akatupatia kile chengine." Katika sentensi hii twapata vipande vinavyoashiria lakini hatufahamu ni nini kinachorejelewa kwa vile imetokea peke yake. Kiambishi a katika neno `akatupatia' kinarejelea kiumbe fulani lakini hatujui ni nini. Vile vile `kile chengine' kinaashiria ile hali kwamba pana zaidi ya kitu kimoja lakini hata hatufahamu kitu hicho ni nini. Kwa hivyo hatuwezi kuielewa sentensi kama hiyo kivyake. Twaweza kusema kuwa haina umoja na muundo kama ule uliojenga matini ya kwanza tuliyoipitia; yaani haina uwiano. Kama tulivyodhirisha katika mifano ya hapo juu, uwiano hutokea iwapo fasili ya kipande kimoja katika taarifa hutegema kuwepo kwa chengine. Yaani kimoja chaashiria chengine ambacho hakiwezi kueleweka bila kurejelea cha kwanza. Kwa hivyo, uwiano ni kiungo katika mfumo wa lugha. Kama tujuavyo, matumizi ya lugha huwa ni kwa madhumuni ya kutoa maana; na kama maana haijitokezi, basi twaweza kusema kuwa lugha hiyo haijatumiwa kwa ukamilifu. Yaani hakuna uwiano. Lakini tunaposema kuwa uwiano huchangia maana ya matini huenda tusieleweke kinaganaga. Kwa mfano, sentensi kama vile `Alisema hivyo' huenda ikawa na maana kwa kiwango fulani. Kwamba twafahamu inachomaanisha kwa ambavyo twaweza

102

kuivunja na kuona inacholenga. Lakini hatuwezi kuifasili kwa sababu hatujui kiambishi `a' - kinarejelea nani au ni nini `kilichosemwa'. Inatuhitaji turejelee kipande chengine; pengine muktadha inamotokea sentensi hiyo. Hapo ndipo tutwaweza kufahamu `nani alisema hivyo' na `alisema nini?' Hivyo basi twaona kuwa sentensi au fungu fulani laweza kuwa na maana lakini lisiweze kufasiliwa; inakuwa pana maana halisi na maana ya kijumla. Ili sentensi ieleweke, haina budi kuwa na maana halisi inayotoletwa na kuwepo kwa kirejeleo na muktadha halisi inamojengewa. Kwa jumla twaweza kutaja kwamba katika utunzi jinsi kitu fulani huandikwa, hutegemea uteuzi wa maneno na miundo ya sentensi anaofanya mtunzi. Haya ni mambo yaliyo muhimu sana kwa mhakiki yeyote hasa kila anaposama kazi anayoihakiki. Baadhi ya mambo hayo tuliyoyataja hapo juu, yanalenga kipengee cha lugha kinachozingatiwa zaidi na isimu. Sasa tungependa kuangalia tamathali za semi ambazo bila shaka hutokea katika kazi nyingi za fasihi na mhakiki hawezi kuziepuka kamwe. Kwanza pana haja ya kutoa vidokezi kuhusu matumizi ya tamathali za lugha. Kwanza, lugha ya tamathali haina budi kuvutia na kuwa yenye mantiki hivi kwamba itavutia msomaji, na vile vile wazo linaloelezwa liwe linachangia katika kushika hamu yake. Mathalani, hamna haja kufananisha vitu viwili vinavyokinzana katika mfano. Pili, lugha ya tamthali isisukumizwe kwa ajili ya kuitumia tu. Sio lazima mtunzi atumie lugha ya tamthali kama haihitajiki au kama haiimudu. Tatu, lugha ya tamathali isitumiwe kujigamba au kuonyesha umahiri wa mtunzi iwapo hapana haja. Lugha hiyo yapaswa kuingizwa kwa ukawaida na uasilia kabisa ili kuonekana kama `iliyozaliwa' pale. Katika kuzingatia jambo hili, pametokea isitilahi mbali mbali zinazoeleza matumzi ya lugha ambazo mhakiki huenda akahitaji `kuzitafuta' katika kazi anayoizingatia. TASHBIHI/TASHBIHA Hii ni isilahi ambayo hutumiwa kumaanisha ile hali ambapo maneno kama yafuatayo hutumiwa - vile, sawa sawa, na, kana kwamba, kama, mithili ya n.k mradi pawe na vitu viwili vinavyolinganishwa, kimoja kikitumiwa ili kueleza kingine. Aghalabu kimoja cha vitu hivyo huwa chaeleweka na hutumiwa ili kuangazia hicho kingine. Kwa mfano, tunaposema `amekonda kama sindano' huwa tunajaribu kuonyesha ile hali aliyo nayo mhusika. Kwamba tayari twafahamu unene wa sindano; hiyo basi

103

twajaribu kuulinganisha na hiyo mhusika. Twaweza kusema `mrefu kama mgomba', `mfupi kama nyundo' `mwenye maringo kama tausi' n.k. Hiyo yote ni mifano ya matumizi ya mbinu ya tashbiha. TASHIHISI/UHUISHAJI Hii ni ile hali ya mtunzi kupatia vitu visivyo na uhao hali ya kuwa na uhai na sifa za kibinadamu. Vitu hivyo, ambavyo kwa kawaida havina uhai, hupewa uhai ili kupata hisia za kibinadamu. Kwa mfano twaweza kupata mtunzi amesema; "Njaa ilimkodolea macho huku uzingizi umemkumbatia kana kwamba hautaki aondoke" au "Mifuko yake ilikuwa inaombeleza kwa kuondokewa na mpenzi wao wa kufa kuzikana -pesa". Twaona hapa kwamba maneno kama vile `kukodoa macho', `kukumbatia' na `kuombeleza' yanawakilisha sifa tunazozihusisha na wanadamu au wanyama ambao wana uhai. Lakini katika muktadha huu, sifa hizo zinachukuliwa na vitu visivyo na uhai kama vile njaa, usingizi na mifuko. Hivyo ni mbinu katika utunzi wa kifasihi tunyoiita uhuishaji au tashihishi. JAZANDA Haya ni mafumbo ambamo maana ya kitu imefichika. Wakati mwingine mwandishi huwa anawapatia wasomaji wake kazi ya kutafuta na kung'amua maana ya kitendo au hali fulani au kisa kwa kutumia fumbo au kwa kutumia jambo ambalo laelekea kuwa la kawaida lakini kumbe pana ujumbe uliofichika. Yaani anaweza kuwa ametumia maneno na visa ambavyo kwa msingi ni vya kawaida kumbe visa vile vyatoa ujumbe mwingine, ambao umefumbwa kama jazanda. Mathalani, katika Nyota ya Rehema (M.S Mohamed) twapata kisa hiki: Nadhari ya Fuad ilichukuliwa na picha iliyomo katika

104

kalenda iliyokuwa ikining'inia ukutani. Chui alikuwa katega juu ya ukingo wa jabali akitazama chini kwa shauku; kipaa kidogoo, kizuri, kilikuwa kimeinama mchirizini kikinywa maji, hakina habari. (uk 10) Hapa mtunzi anatutolea picha ya chui na paa ambao wamechorwa katika kalenda iliyokuwa mle afisini kwa Bwana Patel. Kwa kawaida twafahamu kwamba chui humla paa. Na sasa twaona chui anamtizama paa (ambaye hana habari anatizamwa) kwa shauku, pengine tayari kumrukia na kumfanya chakula chake. Tukio hili ni la kawaida kabisa kwa wanyama kama hao wa porini. Lakini hapa sasa mtunzi anatumia kisa hiki kutuchorea fumbo la kueleza hali ya Fuad na Adila ambapo mmoja wao (bila kutambua) yuawindwa na mwenzie. Ndiposa baadaye katika hadithi twapata matokea ya `uwindaji' huo baada ya Adila kuolewa na Fuad kwa mpango wake Adila. Hivyo basi twaona Fuad ndiye paa na Adila (ambaye anamtamani Fuad) ndiye chui. Fumbo kama hili ndilo tunaloita jazanda. TASWIRA Dhana hii mara nyingi imechukuliwa kumaanisha jazanda. Lakini ukweli ni kwmba taswira ni picha zinazoundwa akilini mwa msomaji kutokana na maelezo ya mtunzi. Ni ile hali ya mtunzi kueleza jambo au kitu fulani wasomaji wake wakakiona kwa uhalisi kabisa lakini katika akili zao. Kama anazungumzia mahali, wale wasomaji wake wanajenga picha ya mahali pale kiasi cha kwamba ni sawa na kushuhudia mahali pale katika hali halisi maishani. Yaani mtunzi anachora picha ambayo yadhirika kama tukio ua kisa halisi. Kwa mfano katika Utenzi wa Al-Inkishafi mtunzi anatuchorea taswira ya maisha ya anasa walivyoyaishi mamwinyi kabla ya kuanguka kwa Pate. Anasema; 37 Nyumba zao mbake zikinawiri kwa taa za kowa na za sufuri Masiku yakele kama nahari Haiba na jaha iwazingiye

105

38

Wapambiye sini ya kuteuwa Na kula kikombe kinakishiwa Kati watiziye kuzi za kowa Katika mapambo yanawiriye

Katika beti hzi mbili twaona jinsi mtunzi alivyoyachora maisha ya ukwasi na starehe waliyoyaishi hao Mamwinyi. Picha anayochora humfika msomaji na kumfanya aone anachozungumzia mtunzi kwa njia ya wazi kabisa. Twaelezwa kuhusu nyumba walizoishi zilizokuwa zinan'gara kwa taa na vito. Picha hii yadhirisha hali ilivyokuwa na ni hali hiyo inayodhihirika akilini mwa msomaji. Hiyo ndiyo mbinu ya taswira katika fasihi. KINAYA Hii ni mbinu katika fasihi ambapo mtunzi hutumia maneno dhidi ya mtu au hali fulani ili kucheka na kutoa kejeli. Aghalabu, huwa ni kusema au kutenda jambo ambalo linatoa maana iliyo kinyume na vile ilivyosemwa au kutendwa. Mtunzi aweza kuwa amemchora mhusika wake kuwa katika tabaka fulani au katika hali fulani ya maisha, lakini maneno anayompa yanakuwa kinyume kabisa na maisha yake. Wakati Zakaria anapomwambia Charles "chukua pesa zako, unafikiri sisi ni masikini" katika Rosa Mistika (E. Kezilahabi), ni matumizi ya kinaya, kwani tayari mtunzi ametuonyesha umasikini wa jamii ya Zakaria. Mhusika ambaye amechorwa kama aliyeshirikiana na wakoloni kuwanyanyasa waafrika wenzake kisha akapewa maneno haya - "huu ndiyo uhuru tulioutaka" (katika Kilio cha Haki) basi itakuwa mtunzi ametumia kinaya. Atakuwa anamkinai mhusika huyo kwa kumpa maneno kinyume na matendo yake na pia kinyume na matarajio ya hadhira. MAJAZI Hii ni isitlahi ya fasihi inayotumiwa kuonyesha matumizi ya majina kwa wahusika ambayo yanalingana na sifa na matendo yao. Huenda majina haya yakawa muhtasari wa tabia au sifa ya mhusika fulani. Wakati mwingine mhusika hupewa jina

106

lenye sifa ambayo ni kinyume kabisa na tabia yake katika kazi husika. Katika kazi nyingi za fasihi, ambazo zilitungwa zamani na zilozoelemea upande wa kutoa maadili, palikuwa na mkondo wa kusawiri wahusika wenye majina ya majazi kwani lengo kuu la wahusika hao lilikuwa kutoa mifano mwafaka ya wema na uadilifu. Ndiposa twapata wahusika wengi wa kazi za Sheikh Shaaban Robert walipewa majina ya majazi. Mathalani, Adili wa Adili na Nduguze au Karama na Majivuno katika Kusadikika. Aziza, Fuad, Sulubu (Nyota ya Rehema) kitaru (Mashetani) ni mifano mingine ya wahusika waliopewa majina kulingana na tabia zao. TAKRIRI Hii ni istilahi inayoonyesha kile kitendo cha mtunzi kurudia rudia (kariri) maneno au sauti au vifungu fulani katika kazi yake. Aghalabu, mbinu ya takriri hutumiwa ili kutilia uzito maneno au mafungu yaliyorudiwa katika riwaya au tamthilia ilhali mbinu hiyo hiyo hutumiwa kama mbinu mojawapo ya kudhirihirisha ustadi katika ushairi. Katika kitabu cha Rosa Mistika (E. Kezilahabi), neno "walirithi" limekaririwa mwishoni mwa hadithi ambapo wanakijiji waligawana mali ya mzee zakaria baada yake na bibie kuaga dunia. Katika vita vya Maji Maji vilivyoendelezwa katika Kinjeketile (E. Hussein), maneno `maji' na `umoja' yamekaririwa pia. Hapa ni kwa minajili ya kuyapa maneno yale msisitizo. Takriri katika ushairi ni mbinu inayotumiwa kwa upana sana, kwa vile twaweza kuwa na ukariri wa neno moja au zaidi, sauti, mshororo n.k. Kwa mfano katika shairi la `kuno kunena' katika Sauti ya Dhiki (A. Abdallah) sauti [k] na [c] zimekaririwa sana. Katika shairi `oa' katika mashairi ya Muyaka (Abdulaziz) neno oa limikaririwa katika kila ubeti. Hapo twaona basi takriri ni mbinu inayoweza kutumiwa kwa sababu mbali mbali katika utunzi. SADFA Hii ni istilahi, ambayo hutumiwa kuonyesha utukiaji wa matukio, visa au mambo mawili kwa wakati mmoja lakini bila kupangiwa kufanyika vile. Kwa mfano, iwapo msichana atakuwa anataka kutoroka nyumbani na iwe basi wakati ule anapotorokaa wazazi wake hawapo nyumbani kumkataza (kama ilivyokuwa kwa Hawa katika Anasa

107

cha Yusuf Kingala) basi vitendo vyote viwili huwa vimesadifu. Yaani kutoroka nyumbani kwa Hawa pamoja na kutokuwepo nyumbani kwa wazazi wake ni sadfa. MAJAALIWA Hii ni isitlahi ambayo hutumiwa katika fasihi kueleza yale mambo yaliyompita binadamu hivi kwamba huwa ni kama yamepangwa na Mungu au kiumbe aliye na uwezo mkubwa zaidi ya binadamu. Yaani bindamu hata afanyeje hawezi kuyabadili mambo hayo. Mfano mzuri ni Rehema katika Nyota ya Rehema ambapo yeye kuzaliwa akiwa kitoto `kibaya' ambacho hakikumvutia babake yalikuwa majaaliwa, kwani hangeweza kuyabadili. Kwa jumla basi hizo ni baadhi ya isitilahi katika fasihi ambazo hutumiwa kuonyesha matumizi mbali mbali ya lugha. Vile vile, pana isitilahi nyengine kama vile tashititi, tabaini, mbinu rejeshi n.k. ambazo mhakiki anapaswa kufahamu ili azitambue pindi akutanapo nazo katika kazi anayo hakiki. Ni muhimu mhakiki atambue kwamba kazi nzuri ya fasihi huratibiwa kulingana na vile maudhui yake yameendelezwa, na hili hutegemea lugha kwani bila lugha hapana maudhui. Kipengee cha lugha hivyo basi ni muhimu sana katika kuihakiki kazi yoyote ya fasihi. 4.4 HITIMISHO Uhakiki wa kazi ya fasihi ni shughuli ambayo ina historia ndefu. Tangu enzi za babu zetu, uhakiki ulikuwa ukitumika katika kulinganisha, kukosoa na kurekebisha masimulizi mbali mbali ambako hadithi ilishiriki kikamilifu. Shughuli hii imeendelea kukua na kufikia kiwango ambacho hivi leo chahitaji ujuzi wa hali ya juu. Kulingana na ukuaji wa jamii katika ujumla wa maisha, kumekuwa na haja ya kuitizama jamii kutoka pande zake zote. Kutokana na haya, uhakiki wa kazi za fasihi umethibiti mikondo maalum ya kutazama kazi za fasihi. Ingawa wahakiki wana uhuru wa kuichambua kazi ya fasihi wapendavyo, bila shaka wana jukumu kubwa la kutumia mbinu thabiti ili kuhifadhi maana na faida ya uhakiki. Katika kazi hii tumejaribu kujenga misingi madhubuti itakayomsaidia mhakiki katika kazi yake ya kuhakiki.

108

SURA YA TANO

TAMATI Katika kazi hii tumejaribu kuendeleza dhana na kauli mbali mbali kuhusu fasihi na kitendo cha kuihakiki. Maoni haya yote yamefinyangwa kutokana na tajiriba yetu katika mazingira maalum ya usomi na katika kipindi maalum cha kihistoria. Baadhi ya kauli tulizozitaja hapa zinafaa kwa wakati huu tu; nyengine zitadumu na kutumiwa na wengi kwa muda mrefu. Tunaishi katika nyakati ambazo zinabadilika kwa kasi mno na hatuna uhakika wa kile kitakachotokea siku za usoni. Lakini ukweli ni kwamba, kitakachotokea, kitaathiri mitizamo, maadili, na mienendo yetu kuhusu maisha na hata jinsi tunavyouona ulimwengu wetu kwa jumla. Athari hizi zitajitokeza katika kazi za sanaa na hususa fasihi. Mitambo ya kuziendeleza kazi hizo itabadilika na kutushurutisha kubadili vigezo vyetu vya kuzitathimini. Kwa mfano wakati ambao watoto wengi wangeutumia kusikiza maoni na hadithi zilizosimuliwa na nyanya na babu unatumiwa kutizama televisheni na sinema. Ni lazima sisi kama wahakiki tuelewe misingi hii na tuweze kudhihiri uketo wa kazi zetu katika miktadah kama hiyo. Kwa mfano twaweza kutumia mtambo huo huo wa televisheni kuwasilisha kazi zetu lakini ziwe kazi ambazo zitawashika hadhira kama inavyofanya sinema. Tumetaja katika sura ya kwanza kuhusu kuja kwa taaluma ya uandishi na uchapishi na athari zake kwa fasihi. Wakati huu wa sasa ni wakati ambapo teknolojia imerahisisha jinsi ya kutenda kazi nyingi za mwanadamu. Vile vile imewawezesha wengi kufanya nakala za kazi za fasihi na hivyo kuzishushia ile thamani ya asili. Kila kipindi cha kihistoria huja na mabadiliko haya. Wakati Marx alipoendeleza maoni yake ambayo yalikuja kujulikana kama nadharia ya Umarx, alipata malighafi yake kutokana na tajiriba zake na maoni yake kuhusu mambo yatakavyokuwa siku zambeleni. Alipohakiki mfumo wa ukapitolisti kwa mfano, mfumo huo ulikuwa katika uchanga wake na hivyo aliweza kujenga nadhararia yake kwa kurejelea misingi ya kuchipuka kwa ukapitolisti. Aliweza pia kubashiri hali itakavyokuwa katika mfumo huo. Mbali na kuuona kama

109

utakaonyonya mfanyakazi kwa kasi mno na kumwondolea thamani ya kujihusisha na alichozalisha, alibashiri kuwa mfumo huo utahimili misingi ambayo itauangamiza kabisa. Hapo ndipo alifanya taksiri. Ukapitolisti unaendelea kujijenga kwa njia changamano sana na hivyo basi kuathiri sura zote za maisha ya wanadamu. Kule kubadilika kwa muundo-kuu ambako huchukua muda mrefu kuliko muundo-kati, kumechukuwa zaidi ya nusu karne kudhihiri mabadiliko ya hali ya uzalishaji katika tanzu zote za utamaduni. Ni katika wakati huu tulio nao ambapo twaweza kuona kweli umbo lililochukuliwa na mabadiliko hayo. Twaona hivi sasa uzito haupo katika kiini cha sanaa ya wafanyakazi pindi wachukuapo hatamu za uongozi au ile ya jamii isiyokuwa na matabaka [kama alivyobashiri Marx] bali kipo katika sura za maendeleo ya sanaa katika hali ya kisasa ya uzalishaji. Ndiposa tunakariri wazo kuwa maoni yetu kuhusu masiha ni zao la tajiriba zetu katika wakati tuishio na ni maoni ambayo haywezi kubashiri kwa udhati yale yatakayotokea siku za baadaye. Ama kwa hakika tunachoweza kubashiri kwa udhati ni kwamba patakuwepo mabadiliko. Sanaa katika mfumo wa unakilishi (reproduction) ambapo kazi moja yaweza kunakiliwa na kusambazwa, huwa ina udhaifu fulani. Ni kwamba sanaa hiyo hupoteza baadhi ya nguzo zake muhimu ambazo ziliipa muundo kabla ya mfumo huu. Nguzo hizo ni kama vile ubunilizi (creativity), thamani ya milele, na hali ya upekee. Hivyo basi sanaa haihusishwi na anayeiumba, utaratibu wa kuiumba, na muktadha inamoibukia (mambo ambayo aliyagusia Marx). Sanaa inakuwa bidhaa ambayo soko lake ndilo linaloongoza utunzi wake. Hatutaki kutoa ishara kwamba unakilishi wa kazi za sanaa umeletwa na ukapitolisti. Kazi za sanaa tangu zilipoanza kutungwa zilitoa uwezo wa kunakiliwa. Kwamba yule aliyechonga angeigwa na mchongaji mwingine, wanafunzi walifanya nakala za kazi ya mwalimu wao kama njia moja ya kujifundisha, halafu wengine walinakili kazi za sanaa kwa minajili ya kujipatia faida. Haya yote yanaonekana duni yakilinganishwa na unakilishi-makania. Maendeleo ya mfumo huu yanajulikana wazi wazi; athari za mabadiliko yaliyoletwa na uchapishi (ambao kwa hakika ni unakilishimekania wa uandishi)sote twayafahamu. Isitoshe, mabadiliko yaliyoikumba sanaa ya tamthilia na drama kwa kuja kwa filamu na sinema pia twayafahamu. Kwa majilio ya sinema, kiini cha muigizi kilichukuliwa na mpiga picha. Ambapo jicho lake na mahali

110

kamera imeezekwa ndiyo nguzo muhimu katika sanaa hiyo. Uwezo aliokuwa nao muigizi, wa kuchukuana na hadhira kwa kupima hali yao halisi anapokuwa jukwaani na uwezo wake wa kuwasilisha kitendo chake mwenyewe jukwaani unachukuliwa na kamera. Hapo ndipo twaona kwamba mkazo unatiliwa yanayofanywa na kamera badala ya kitendo chenyewe cha kuigiza. Vile vile muigizi hawezi kujifunga na matarajio ya hadhira yake jukwaani. Kazi tunayoipata ni ile ambayo imepitiwa na mhariri ili kutoa picha fulani maalum. Hata hivyo mfumo wa unakilishi una mema yake. Unatuwezesha kupata sanaa kutoka kwa jamii ambazo hatuishi karibu nazo na pia kutuletea mambo yaliyopita japo kwa kuzingatia ubunifu na kumbukumbuku zilizoko. Kazi ya sanaa katika mfumo huu kama ilivyo na tanzu fulani za fasihi katika vipindi vilivyopita ina uwezo wa kutoa athari kwa wengi kwa wakati mmoja; na hicho kinachoifanya kuwa yapendeza wengi. Wakati watu wanapoitizama sinema huweza kupata athari fulani pamoja; na ndivyo ilivyo na mchezo wa kuigiza jukwaani au masimulizi ya shairi kwa hadhiria kubwa. Tofauti na sanaa ya unakilishi na hiyo ya awali ni kwamba ya kisasa yaweza kutamalakiwa na mtu binafsi ambaye ataitumia wakati na mahali anapochagua. Mtu aweza kununa sinema akaiona katika usiri wa nyumba yake. Shughuli hii ndiyo inayoathiri thamani na maana ya kazi ya sanaa. Na ni juu ya mhakiki wa sanaa na fasihi kujikita ujuzi wa mambo haya ili kuweza kufanya kazi yake huku akifahamu ni kazi nyingine zipi zinazoathiri upokezi wa kazi yake na anayoihakiki na vile vile ni vipi mfumo huu unavyoathiri watunzi na hadhira. Mengi yamesemwa kuhusu nafasi ya fasihi katika ulimwengu wetu huu. Wengine wamelalamika kuhusu ukosefu wa ari ya kusoma vitabu na hivyo basi wengi wa waandishi wetu kuamua kuandika vitabu ambavyo wanajua vitatumiwa shuleni na vyuoni kama masomo ya kutahiniwa. Hii ni njia moja ya kuua ubunilizi kwani kutunga ili kazi iweze kununuliwa ni kufinya mtunzi na kuiga sanaa mamboleo (popular art) ambayo huongozwa na kununuliwa kwake. Maoni yetu ni kwmba michezo ya kuigiza imepata ari mpya hasa katika kpindi hiki ambapo wengi wanaitumia kama mtambo wa kuwaelimisha wengi kuhusu haki zao. Hili ni jambo la kutia moyo sana na twatarajia litaendelzwa ipasavyo.

111

MAREJELEO Abrams, M.H (1981) A glossary of Literary Terms (4th Edn) Holt Rinhart and Winston, U.S.A. Althusser, L. (1971) Lenin and Philosophy and other Essays. London: New Left Books Ameir, I.H (1983) Misingi ya Nadharia ya Uhakiki. Dar es Salaam: Tuki. Coombes, H, (1953) Literature and Criticism. Chatto and Windus, Australia. Derrida, J. (1973) Speech and Phenomenon. Evanston: Northwestern University Press. ................. (1976) Of Grammatology. Baltimore: John Hopkins University Press Dorsch, T.S (1965) Classical Literary Criticism. Penguin Books Foucault, M. (1978) I Pierre Riviere. Harmondsworth: Penguin. .................... (1979a) Discipline and Punishment. Harmondsworth: Penguin .................... (1979b) 'What is an Author', Screen 20 (1) pp. 13-33 .................... (1981) The History of Sexuality, Vol. 1, An Introduction. Harmondsworth:Pelican .................... (1986) The History of Sexuality, Vol 2, The Use of Pleasure. Harmondsworth: Viking. Fowler, R. (1975) Style and Structure in Literature. Basil Blackwell Oxford. Escarpit, R. (1974) Sociology of Literature. London: Frank Cass and Co. Ltd. Gilbert, S. and S. Gubar (1979) The Mad Woman in the Attic: The Woman Writer and the Nineteenth-Century Literary Imagination. New Haven: Yale University Press. Halliday M.A.K na Ruqaiya, H (1976) Cohesion in English. London: Longman Group Ltd. Holman, C.H. (1977) A Handbook of Literature. Odyssey Press inc. U.S.A. Hough, G. (1966) An Essary on Criticism. Great Britain Redwood Pron Ltd. Jacobus, M. Eds. (1979) Women Writing and Writing about Women. London: Crown Helm. Jefferson, A na Robey, D (1982) Wahiriri wa Modern Literary Theory. New Jersey Barnes & Noble Books. Kirumbi, P.S (1975) Misingi ya Fasihi Simulizi. Nairobi:Shugwa ya Publishers Ltd. Kristeva, J. (1981) "Women's Time", Signs 7 (1). Chicago: University of Illinois Press.

112

................. (1984) Revolution in Poetic Language. New York: Columbia University Press. Lacan, J. (1977) Ecrits. London: Tavistoch. Mazrui, A. M. na I. N. Shariff (1994) The Swahili : Idiom and Identity of an African People. New Jersey: World Press, Inc. McGilhrist, I. (1982) Against Criticism. London: Faber and Faber Ltd. Mohamed, S.A (1984) Makala `Kupatana na Riwaya Zangu katika MWAMKO Toleo la 2 chuo kikuu cha Nairobi. Okot, P'Bitek (1973) Africa's Cultural Revolution . Nairobi: Macmillan Books For Africa Olson, E (1965) Mhariri, Aristotles poetics and English Literature. Chicago: The University of Chicago Press. Ohly, R. (1981) Progressive prose. Dar es Salaam:TUKI. Polome, E.C (1967) Swahili Language Handbook, Centre for Applied Linguistics U.S.A. Peck, J na Coyle, M. (1984) Literary Terms and Criticism, Macmillan Edn Ltd. Ramkin, D (1972) Style and Structure. Harcourt Brace Jovanovich inc. Rawlinson, D.H (1979) The Practice of Criticism. Vikas Publishing Hse Pvt Ltd. Vasquez, A.S (1973) Art and Society. New York: Monthly Review Press. Showalter, E. (1977) A Literature of their Own: Women Novelists from Bronte to Lessing. New Jersey: Princeton University Press. Wellek na Warren (1949) Theory of Literature. Penguin Books.

113

Information

UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI

113 pages

Find more like this

Report File (DMCA)

Our content is added by our users. We aim to remove reported files within 1 working day. Please use this link to notify us:

Report this file as copyright or inappropriate

24186


You might also be interested in

BETA
UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI